Bernard Morrison "Kocha Nipange Niwaonyeshe Kazi"


SAA chache kabla ya watani wa jadi wakubwa nchini Simba na Yanga kukutana katika nusu fainali ya Kombe la FA, mambo yanaendelea kuwa makubwa na sasa kuna kauli nzito imetolewa na nyota wa Yanga.

Anaitwa Bernard Morrison, huyu ni kiungo mshambuliaji wa Yanga, kuelekea mchezo huo, ametoa kauli kwa kumwambia kocha wake: “Nipe nafasi ya kucheza niwaonyeshe (Simba) kile ambacho kimenifanya mimi niwepo Yanga.

”Morrison ambaye alikuwa na mvutano wa kimkataba na masuala ya nidhamu na baadhi ya viongozi wa klabu yake, alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kufunga bao pekee la ushindi dhidi ya Kagera Sugar, juzi kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.

Yanga ilipata ushindi huo wa Ligi Kuu Bara (VPL) huku Morrison akifunga bao zuri kwa kumalizia pasi ya David Molinga.Akizungumza katika mahojiano maaluma na Championi Ijumaa, Morrison alisema: “Nikipata nafasi ya kucheza nitaendelea kulinda heshima yangu na ya klabu, muhimu naomba Mungu niwe na afya njema kisha kocha anipe nafasi ya kucheza.


“Ninachohitaji ni sapoti ya mashabiki ambao wamekuwa wakiniunga mkono tangu nimefika hapa Tanzania, kama timu tunataka kuendelea pale tulipoishia.

”Kauli hiyo ya tulipoishia inaweza kutafsiriwa kwa nuru ya mchezo wa timu hizo uliopita uliomalizika kwa Yanga kushinda bao 1-0 mfungaji akiwa huyohuo Morisson ambaye amekuwa ni kipenzi cha mashabiki wa timu yake.

“Katika mchezo dhidi ya Kagera (juzi) sikutegemea kama ningekuwa na mchezo mzuri kama ilivyokuwa, sababu nilikuwa na muda sijapata nafasi ya kucheza muda mrefu kama ilivyokuwa,” alisema Morrison.

Kuhusu mchezo huo dhidi ya Simba, Mghana huyo aliongeza kwa kusema: “Tunahitaji matokeo mazuri ili kupata nafasi ya kucheza michuano ya kimataifa msimu ujao, muhimu naomba kocha anipe nafasi kama nitakuwa fiti kiafya kisha mashabiki watuunge mkono katika mchezo huo muhimu.


”Tangu aifunge Simba katika mchezo wa Machi 8, mashabiki wengi wa Yanga wamekuwa na imani na Morrison wakiamini uwepo wake utasaidia timu yao kupata matokeo mazuri katika mchezo huo wa Jumapili utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad