Bernard Morrison "Nimerudi Kuitungua Simba FA"
0
July 05, 2020
“AMENIAHIDI kufunga bao au kutengeneza nafasi ya kufunga dhidi ya Simba,” hiyo ni kauli ya Kocha wa Yanga, Mbelgiji Luc Eymael akielezea ahadi ya mshambuliaji wake, Bernard Morrison mara baada ya kutua mazoezini juzi.
Jumatatu iliyopita Morrison alitimuliwa kambini na kocha Eymael baada ya awali kuondoka bila ruhusa huku akiripotiwa kuwatisha walinzi waliokuwa wakilinda kambi ya Yanga kwenye hoteli moja pale Mikocheni jijini Dar.
Baada ya tukio hilo, Morrison alionekana ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kuitwa kujadiliana na mabosi wa taasisi hiyo kuhusiana na ishu za kimkataba, juzi Alhamisi alirejea Yanga na kuanza mazoezi ya pamoja na wenzake.
Kumbuka kabla ya hapo, Morrison amewahi kugomea safari ya timu hiyo kwenda mkoani kucheza mechi ya ligi kuu dhidi Mwadui kule Shinyanga na JKT Tanzania huko Dodoma akidai ni majeruhi.
Yanga, leo Jumamosi inacheza na Biashara United ukiwa ni mchezo wa ligi kuu pia ipo kwenye maandalizi ya kuwavaa Simba kwenye nusu fainali ya Kombe la Azam Sports Federation Cup ‘FA’ hapo Julai 12, mwaka huu ambapo mchezo wao wa mwisho Yanga ilishinda bao 1-0 mfungaji akiwa Morrison.
Morrison alijiunga na Yanga, Januari mwaka huu akitokea kwao Ghana, tangu siku ya kwanza alionyesha matumaini makubwa kwa mashabiki hao baada ya kuibuka na staili yake ya kupanda mpira na kupiga pasi kwa manjonjo.
Akizungumza na Championi Jumamosibaada ya kurejea, Morrison alisema atahakikisha anatoa burudani ambayo haijawahi kutokea kwenye michezo yote iliyobaki ya ligi kuu na FA.
“Namshukuru Mungu kwa kuendelea kunisimamia na kuwa mzima, kubwa watu watambue kuwa nipo Yanga kwa ajili ya kazi na kuhakikisha natoa burudani zaidi kwa mashabiki wetu, jambo ambalo nilianza nalo wakati najiunga nayo.
“Baada ya kuwepo na maneno ya hapa na pale sasa naomba niwaahidi mashabiki na wana Yanga wote kuwa kwenye michezo iliyosalia watafurahi roho yao kwa burudani nitakazokuwa nikizitoa uwanjani,” alisema Morrison.
Kwa upande wake, Eymael ameliambia Championi kuwa, tayari amemalizana na Morrison na suala lake limebakia kwa uongozi baada ya kuomba msamaha kwa kile ambacho alikifanya Jumatatu usiku kambini saa chache kabla ya mchezo wa Kagera Sugar, Jumatano.
“Katika kikao changu na yeye nimeongea na Morrison kwa muda mrefu sana juzi, kwa upande wangu nimemalizana naye na sina kinyongo naye na nikimuhitaji katika mchezo ujao dhidi ya Kagera Sugar basi nitautaarifu uongozi ili wamlete ajiunge na wenzie.
“Morrison kaniahidi mengi sana makubwa na kikubwa yupo hapa kuisaidia timu yake ya Yanga na atalithibitisha hilo siku ya mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA dhidi ya Simba SC, kwani ameniahidi kufunga bao au kutengeneza nafasi ya kufunga katika mchezo huo.”Imeandikwa na Wilbert Molandi, Said Ally, Mussa Mateja na Joel Thomas.
Tags