Breaking News: Bernard Membe ajiunga rasmi ACT Wazalendo


Ni rasmi sasa, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Bernard Membe amejiunga na chama cha upinzani ACT- Wazalendo

Uanachama wake mpya katika ACT- Wazalendo umetangazwa leo na kiongozi wa chama hicho Zitto Kabwe katika mkutano wa wanahabari wadau wengine kutoka ulimwenguni kote uliofanyika katika mtandao wa Zoom.

Membe amesema amejiunga kama mwanachama wa kawaida lakini yuko tayari kutumikia chama hicho kwa ngazi na namna yoyote ile.

"Kilichonivutia katika chama cha ACT-Wazalendo ni katiba ya chama hicho na itikadi yake ya kutaka kuleta mabadiliko," amesema Membe

Aidha bwana Zitto Kabwe amemtia moyo Membe kuchukua fomu kuwania nafasi ya uongozi.

Membe aliitikia kwa kuahidi kwamba atakuwa tayari kushiriki katika kinyang'anyiro cha uchaguzi.

"Watanzania watafurahia uchaguzi huu ujao," ameahidi Membe.

Kuhusu vyama vya upinzani kuungana na kuweka mgombea urais mmoja, Kabwe alisema mazungomzo baina ya vyama bado yanaendelea

Awali Kabwe alielezea mazingira ya uchaguzi ujao kuwa hayatapelekea uchaguzi ulio huru na wa haki akitaja pamoja na mambo mengine kutoamini uhuru wa tume ya uchaguzi na weredi wa jeshi la polisi

BBC ilipomuuliza kwanini bado wataendelea na uchuguzi ilihali hawaamini mazingira kupelekea uchaguzi huru na wa haki Kabwe alisema kutokushiriki pia uchaguzi si jawabu la changamoto kwa demokrasia Tanzania.

"Tumeona katika uchaguzi uliopita visiwani Zanzibar na mahali pengine duniani ambapo vyama vya upinzani vilisusia uchaguzi lakini hakuna mabadiliko yoyote yaliyotokea. Hivyo kususia uchaguzi si jawabu" alisema Kabwe

Tanzania inaelekea katika uchaguzi mkuu mnamo mwezi Oktoba mwaka huu. Tayari chama tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekwisha teuwa wagombea wake wa urais kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad