CCM Bagamoyo Yawaonya Ambao Kura Hazijatosha



Na Omary Mngindo, Bagamoyo

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, kimewataka wanachama wake ambao kura za maoni hazikutosha, kupeleka malalamiko yao ndani ya chama ili yafanyiwekazi badala ya kwenda TAKUKURU.

Chama hicho kimesema kuwa kina Kamati mbalimbali zinazoshughulikia masuala yahusuyo chama na wanachama wake, zikiwemo zinazoshughulikia malalamiko kutoka kwa walengwa hao, hivyo amekerwa na baadhi ya walioshindwa kwenda TAKUKURU.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa chama hicho Abdul Sharifu, akizungumza na wana-CCM hao kabla ya kuanza kwa kura za maoni za kuwapata madiwani wa Viti Maalumu, ambapo alielezea kusikitishwa kwake kwa vitendo vya baadhi yao kwenda kulalamika kuwa wenzao walitumia mchezo mchafu.

"Tunatambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kipambana na Rushwa TAKUKURU, kwani kwa muda mrefu suala la rushwa linapungua siku hadi siku, lakini wanaokwenda kulalamika baada ya kura za maoni walikuwa wapi, kwanini wasingekwenda kabla?," alihoji Sharifu.

"Hapahapa nilipo nimepigiwa simu naambiwa wanachama wangu wamejaa TAKUKURU, wanadaiwa walijihusisha na mchezo mchafu wakati wa kuelekea kwenye zoezi la kura za maoni, hili jambo linanisikitisha sana, sisi viongozi hatuna taatifa hiyo," aliongeza Mwenyekiti huyo.

Aliongeza kwamba hawana lengo la kuwaingilia TAKUKURU, kwani ni chombo cha Serikali kinachotekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria ya nchi, lakini wanawaomba kuwa malalamiko yanayopelekwa kilindi hiki baada ya kumalizika kwa michakato ya kichama wayarudishe ndani ya chama.

"Chama hatuna nia ya kuwaingilia katika kazi zao isipokuwa tunawaomba hao watu waturejeshwe ndani ya chama, ili hatua za kinidhamu ziweze kuchukuliwa kwa wahusika, kwani baada ya kura za maoni tunaelekea kwenye uchaguzi Mkuu, hofu yetu hii hali isije ikatuletea mifatakano," alisema Sharifu.

Alimalizia kwa kuwataka wana-CCM kutambua kwamba wanapoingia katika chaguzi zozote watambue kwamba kuna kupata na kukosa, hivyo matokeo yote wayakubali na si kushinda tu wanaposhindwa wanaleta nongwa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad