CHADEMA yatoa ratiba ya Uchukuaji wa Fomu




Na Thabit Madai,Zanzibar. 

CHAMA  Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Zanzibar, kimewaomba wanachama wake wenye sifa za kuwania nafasi mbalimbali za Uwongozi wajitokeza kwa akili ya kuchukua Fomu ya kuwania nafasi Urais wa Zanzibar, Uwakilishi, Ubunge na Udiwani kwa wadi za Unguja na Pemba kuanzia Julai 04 mwaka huu. 

Pia kimewataka Wananchama wa Chama hicho kutokubali kutumika kisiasa kwa lengo la kuwaharibu chama pamoja na kuepuka makundi katika kipindi chote cha kupitisha wagombea na kipindi cha Uchaguzi  Uchaguzi mkuu.  

Wito huo umetolewa Jana na  Naibu katibu Mkuu wa Chama hicho Zanzibar, Salum Mwalimu wakati akizunguma na Waandishi wa Habari katika Ofisi za Chama hicho zilizopo Kikwajuni Mjini Unguja. 

Salumu Mwalimu alisema kuwa Mchakato wa Uchukuaji wa Fomu kwa Sasa upo wazi hivyo wanachama wa chama hicho wanapaswa kujitokeza kuchukua Fomu kwa ajili ya kuomba ridhaa kwa chama kuwapisha kuwa wagombea wa nafasi ya Urais wa Zanzibar, Ubunge, Uwakilishi na udiwani kupitia Chadema. 

Alisema Chadema imejipanga kikamilifu katika kushiriki uchaguzi mkuuu wa mwaka huu 2020 ambapo itasimamisha wagombea kwa nafasi zote zinazogombaniwa ukilinganisha na chaguzi zote zilizpita. 

"Sisi Chadema tunashiriki Katika Uchaguzi wa Mwaka huu kwa ukamilifu kwa nafasi zote hivyo wagombea wajitokeza wachukue fomu maana Mchakato tayari umeanza na ofisi zitakuwa wazi kuanzia saa mbili hadi kumi alasili. 

Salum Mwalimu alieleza kwamba Mchakato huo wa uchukuaji wa fomu utakuwa kwa awamu ambapo kuanzia Julai 04 hadi 19 nafasi ya Urais, Julai 04 hadi 10 kwa nafasi ya Uwakilishi na ubunge huku Julai 11 hadi 17 uchukuaji wa fomu kwa nafasi ya Udiwani. 

Alisema mara baada ya wagombea kujitokeza kuchukua fomu na zoezi hilo kufungwa kamati maalumu ya Chama hicho itakaa kwa kupitia majina hayo pamoja na kukaa kwa ajili ya kupitisha jina la Mgombea Urais ambapo itaanza baada hapo majina ya wagombea wa nafasi nyingine watapitishwa. 

"kuanzia Julai 22 hadi 29 hapo kamati kuu itakaa kwa ajili ya kupitia majina ya wagombea wa Urais wa Zanzibar na kupendekeza wagombea pamoja na kumteuwa mgombea wa nafasi hiyo, huku Ubunge na uwakilishi kamati itaanza kukaa kuanzia Julai 25 na kamati kuu Julai 30 au 31 kwa ajili ya kuteuwa wagombea hao," alisema Salum Mwalimu. 

Katika Maelezo yake Salum Mwalimu aliwataka wagombea wa nafasi hizo kutokubali kutumika kisiasa na vyama vingine kwa lengo la kuwaharibu wao Chadema pia aliwataka wawe wamoja katika kipindi chote cha Mchakato wa kuwatafuta wagombea na kipindi cha Uchaguzi Mkuu. 

"Mimi nataka niwaambie kuwa ndani ya Chadema haturuhusu Makundi, haturuhu mtu kuja kwa lengo la kutuharibu tupo vizuri na kwa yoyote tutakae mbaini hata akitoa rushwa hatua kali za kisheria atachukuliwa na Chama," alieleza Salum Mwalimu. 

Aidha Salum Mwalimu alisema kwa nafasi ya Udiwani mara baada ya zoezi la uchukuaji wa fomu 11 hadi 17 kukamilika kutafuatwa na kura za maoni na kamati tendaji kanda kuanzia Julai 20 hadi 23  na Julai 24 kamati tendaji kuteuwa wagombea wa nafasi hiyo. 

Katika hatua nyingine Salum Mwalimu alisema kwamba Chama Cha Demokrasia na Maendeleo wamejipanga Katika kuwatumikia Wazanzibar kwa nafasi zote na kwa uwaminifu Mkubwa na Uzalendo wa hali ya juu. 

"Mwisho nataka niwaambie ndugi zangu Waandishi wa Habari kuwa Chadema tumejipanga kwa asilimia kubwa iwe Jimbo,wadi na hata Taifa tutawatumikia kwa Uzalendo Mkubwa" alisema Salum Mwalimu.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad