WAKATI wadau wa burudani na Watanzania kwa ujumla wakipigwa butwaa na ‘memba’ mpya wa Lebo kubwa ya muziki Wasafi Classic Baby (WCB), Zuhura Kopa ‘Zuchu’, ambaye amekubalika vilivyo kwenye ‘game’ ndani ya muda wa miezi mitatu, Mnajimu Maalim Hassan Yahya Hussein, amefichua kile kinachompandisha chati mlimbwende huyo.
Zuchu ambaye ni mrembo wa pili kuwepo katika Lebo ya Wasafi, baada ya kutanguliwa na Queen Darleen, amezidi kung’ara kutokana na sauti yake ya ‘kumtoa nyoka pangoni’ huku akiwaacha watu midomo wazi pale alipofanikiwa kutoboa katika kipindi kigumu cha wimbi la janga la maambukizi ya Virusi Vya Corona.
Ndani ya miezi michache, amefanikiwa kutoa ‘Extended Playlist’ yake (EP) inayokwenda kwa jina la ‘I AM ZUCHU’, na kupokelewa vizuri na mashabiki zake, kitu ambacho kimekuwa ni maajabu ya aina yake kwenye tasnia ya muziki.
Mbali na kufanya vizuri kwenye kazi zake, pia amekuwa ni msanii ambaye kwa sasa yuko karibu sana na Bosi wa Lebo hiyo ambaye ni mwanamuziki mkubwa barani Afrika; Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.
Watanzania wanamtazama Diamond kama kaka ambaye amempa sapoti na kumuinua vilivyo Zuchu.
Zuchu ambaye amezaliwa Novemba 22, mwaka 1994 anasimamiwa na nyota aina ya Nge.
UTABIRI UNASEMAJE?
Akizungumza na IJUMAA WIKIENDA, kuhusu nyota hiyo ya Nge ambayo ndiyo nyota aliyonayo Zuchu, Mtabiri maarufu Afrika Mashariki, Maalim Hassan alisema kuwa wenye nyota hii ni wale waliozaliwa kati ya tarehe 23 Oktoba na 21 Novemba ya mwaka wowote na wana uwezo na uvuto katika mambo yao.
“Wenye nyota ya Nge wana uwezo mkubwa wa uvuto au kuvutia watu katika mambo yao.
“Ni watu wenye uelewa mkubwa na ni majasiri katika kukabiliana na matatizo ambayo wengine yamewashinda.
“Ni wenye tabia ya kutilia mkazo mambo yao, tena kwa ukali na ikibidi kutumia ukatili ili jambo litimie, wao wako tayari.
“Ni watu wenye tabia ya siri na wanapenda kufanya mambo yao kwa siri sana, wenye nyota hii kama ilivyo alama yao, hawaogopi kiza.
“Wana uwezo na kipaji cha asili cha kutekeleza mambo yao na wakafanikiwa.
“Ni watu wenye akili nyingi, werevu na wepesi sana kuelewa mambo.
“Watu wa Nge vile vile wana tabia au wanaweza kujidhuru wao wenyewe mambo yanapowawia magumu,’’ alisema Maalim.
Aidha aliongeza kuwa, watu wenye nyota ya Nge, wanashirikiana na nyota zingine ambazo wanaendana nazo.
“Nyota za watu ambao anaelewana nao ni nyota za Kaa na Samaki.
“Nyota za watu ambao haelewani nao ni nyota za Ng’ombe, Simba na Ndoo.
“Nyota inayomsaidia kikazi ni nyota ya Simba, nyota inayomsaidia kihisia ni nyota ya Ndoo.
“Nyota inayomsaidia kipesa ni nyota ya Mshale, nyota inayomsaidia katika Ubunifu ni nyota ya Samaki.
“Nyota bora ya Mapenzi, Ndoa na Ushirikiano ni nyota ya Ng’ombe.
“Nyota bora ya Kujifurahisha ni nyota ya Samaki ambapo nyota ambazo zinamsaidia katika mambo ya kidini na kiroho ni nyota za Kaa na Mizani,’’ aliongeza.
Mbali na tabia hizo, pia kuna aina za mavazi ambazo watu wenye nyota hiyo wanatakiwa kuvaa au hupendelea kuvaa.
“Nge wanatakiwa wavae nguo zenye rangi inayong’ara, zenye kuonekana na maridadi, zilizo katika hali ya suti au mbili kwa pamoja, nguo ziwe za rangi nyekundu au shati jekundu au skafu nyekundu.
“Kitambaa kiwe cha sufi au cha fulana au chenye kumeremeta na mavazi yaendane na kofia na wanawake wapendelee sana kuvaa suruali,’’ aliongeza.