Hii Ndio Historia ya Muuza Madawa ya Kulevya Nguli Duniani PABLO ESCOBAR Aliyejijengea Gereza
0
July 20, 2020
Katika milima inayotazamana na mji wa MedellÃn nchini Colombia, yapo majengo ya kifahari kabisa ndani ya milima hiyo ambayo kwa sasa majengo haya yanatumika kama nyumba ya watawa wa Kanisa Katoliki lakini kabla ya watawa hawa kupewa majengo haya mwaka 2007, majengo haya yalikuwa ni gereza ambalo lilijengwa mwaka 1991 kumuhifadhi mfungwa maalumu raia wa Colombia.
Gereza hili lilikuwa ni tofauti kabisa na magereza yote ambayo umewahi kuyasikia kwani gereza hili licha ya kuwa mali ya serikali lakini michoro yake ilichorwa na kubuniwa na mfungwa mwenyewe.
Si hivyo tu, bali hata maaskari magereza ambao walikuwa wanalinda gereza hili walichaguliwa na mfungwa mwenyewe na hata polisi wa nchi ya Colombia walikuwa hawaruhusiwi kusogolea gereza hilo hata umbali wa maili 12. Kama hiyo haitoshi gereza hili lilikuwa na uwanja wa mpira wa miguu, lilikuwa na bafu lenye Jaccuzi, lilikuwa na bar, lilikuwa na maporomoko ya maji (water falls) yaliyobuniwa kiustadi, na pia chumba (selo) alicholala mfungwa huyu kilikuwa na kitanda kikubwa cha duara chenye kuzunguka pamoja na televisheni kubwa.
Kama hii haitoshi kwenye gereza hilo pia kulikuwa na chumba maalumu cha michezo ya watoto maalumu kwa ajili ya watoto wa mfungwa huyo pindi akitembelewa na familia yake. Na pia ndani ya gereza kuliwekwa darubini kali (Telescope) ya kumuwezesha mfungwa huyo kuangalia katika mji wa MedellÃn ambako familia ya mfungwa huyu iliishi na kila siku jioni walitoka nje kibarazani kuongea naye kwenye simu huku akiwatazama kwa darubini.
Gereza hili lilijulikana kama La Catedral (the cathedral) na lilimuhifadhi mfungwa muhimu zaidi duniani na binadamu aliyeifinyanga na kuifanya biashara ya mihadarati iwe jinsi ilivyo hivi leo. Marafiki zake wa karibu walipenda kumuita El Patrón (The Boss) au El Zar de la CocaÃna (The Tsar of Cocaine) lakini alipozaliwa wazazi wake walimuita Pablo Emilio Escober Gaviria au kwa kifupi Pablo Escobar kama ulimwengu wote ulivyomtambua.
The Boss
Akiwa mtoto wa tatu kwenye familia ya watoto saba ambapo baba yake alikuwa ni mkulima na mama yeke mwalimu wa shule ya chekechea, Pablo Escobar alikuwa ni mwenye kutamani mambo mazito na mwenye maono makubwa tangu angali mtoto.
Akiwa bado kwenye umri wa makumi (teenage) Pablo mara kwa mara aliwaambia ndugu zake na marafiki zake kuwa anataka awe na utajiri wa kiasi cha Peso Milioni 1 za Colombia (COL$ 1 Million) atakapofikisha umri wa miaka 22.
Ndoto hizi zilimfanya ashindwe kumaliza Chuo kikuu alipokuwa anasoma (Universidad Autónoma LatinoAmericana of MadellÃn) na kujiingiza katika biashara za halali na haramu na hatimaye aliacha masomo chuoni. Moja ya biashara zake haramu za kwanza kabisa akiwa kijana chini ya miaka 21 ilikuwa ni kutengeneza vyeti bandia vya stashahada vya chuo alichokuwa anasoma na kuwauzia watu waliohitaji kwa ajili ya kwenda kupata ajira.
Pamoja na biashara hiyo pia Pablo alijihusisha na kusambaza mizigo ya sigara zilizokuwa haziruhusiwi nchini Colombia (Marlboro), pia alifanya kazi kama mlinzi binafsi (bodyguard) pamoja na wizi wa magari.
Moja ya matukio muhimu ya ujana wa Pablo yaliyochangia kuamsha ari ndani yake na kumfanya atamani kuwa moja wa manguli wa biashara haramu lilikuwa ni tukio ambalo alipofikisha miaka 26 alifanikiwa kuweka benki (Cash Deposit) kiasi cha Peso Millioni 100 za Colombia (COL$ 100 Million).
Mafanikio haya yaliwasha taa ndani yake na kuamsha ari ya kutaka kuwa 'Papa' katika 'Dunia' ya siri ya ulimwengu wa biashara haramu.
Katika miaka ya 1970 mamlaka ya kupambana na matumizi mabaya ya madawa nchini marekani (US Drug Enforcement Agency) waliwahi kutangaza kuwa wamewekeza zaidi rasilimali zao kupambana na matumizi na uingizaji wa dawa aina ya Heroin nchini marekani na kwa maoni yao walisema kuwa wanadhani madawa aina ya Cocaine hayakuwa na uwezo wa kuleta uteja (addiction) au kufanya mtumiaji kuwa muhalifu tofauti na dawa aina ya Heroin. Hivyo basi walielekeza nguvu zao zote na rasilimali kupambana na biashara ya usafirishaji wa Heroin kama kipaumbele cha kazi zao.
Hili lilikuwa ni kosa kubwa sana kwa upande wao. Kwani kijana Pablo aliona mwanya huu na udhaifu huu upande wa DEA au pengine tusema kwamba Pablo alifahamu zaidi kuhusu ulimwengu wa mihadarati kuliko DEA.
Kitu kikubwa ambacho Pablo alikiona na watu wakiwemo DEA hawakukiona ilikuwa ni uwezekano (potential) ya kuifanya Cocaine kuwa moja ya madawa yenye soko zaidi Amerika ya Kaskazini. Katika kipindi hiki kulikuwa na watumiaji wachache sana wa Cocaine nchini marekani lakini Pablo aliona fursa ya kuifanya mihadarati hiyo kuwa moja ya madawa yenye kuhitajika sana nchini marekani na ulimwenguni kiujumla.
Kutokana na uzoefu wake wa ulimwengu wa kihalifu, Pablo aligundua kuwa zao la Coca linalimwa nchini Bolivia ambalo linatumika kutengeneza Cocaine ni bora zaidi kuliko Coca inayolimwa nchini kwake Colombia. Hivyo basi Pablo akadhamiria kuwa kama anaingia kwenye biashara hii ya kusafirisha Cocaine ni lazima mihadarati yake iwe tofauti na bora zaidi kuliko Cocaine nyingine watu waliyozoea kutumia. Akadhamiria kufanya Cocaine yake iwe daraja la kwanza ili kuvutia watumiaji na kufanya soko likue kwa haraka.
Kama sehemu ya mkakati wake wa kuingia rasmi kwenye biashara ya kusafirisha mihadarati aina ya Cocaine, mwaka 1975 kijana Pablo alisafiri mpaka nchini Bolivia kukutana na Roberto Suaréz Goméz ambaye marafiki zake walipenda kumuita El Padrino (The Godfather) kiongozi wa Genge lililoitwa La CorparacÃon (The Corporation). Suaréz alikuwa ndiye mtu pekee anayeendesha na kuratibu uzalishaji wa zao la Coca katika nchi ya Bolivia na Peru. Kipindi hiki Suaréz tayari alikuwa na mtandao mkubwa katika America ya kusini na alikuwa na jina kubwa, ushawishi na nguvu ya kijeshi hivyo haikuwa kazi rahisi kwa kijana Pablo kumshawishi Suaréz akubali kufanya naye biashara.
Huyu bwana Suaréz alikuwa na nguvu kiasi kwamba alikuwa na jeshi lake binafsi la anga (Air force) na wanajeshi wa miguu 1,500 ambao walipatiwa mafunzo nchini libya.
Pablo alitumia uwezo wake wa kujieleza na uzoefu wake wa ulimwengu wa kihalifu kumshawishi Suaréz na kumueleza kuhusu mkakati wake wa kuiteka biashara ya mihadarati ya Cocaine nchini marekani na akamdadavulia jinsi ambavyo yeye Suaréz atapata utajiri wa kupindukia kama atakubali kufanya nae biashara.
Pia Pablo alimpa wazo Suaréz kuwa atumie ushawishi wake alionao serikalini (Suaréz alikuwa amefanikiwa kumpenyeza Mdogo wake serikalini na kuwa Waziri wa mambo ya ndani) ahakikishe wanakutana na kiongozi wa Cuba Fidel Castro ili wamuombe kuwa mshirika wao katika mambo kadhaa.
Suala hili lilifanikiwa kwani Pablo na Suaréz walipata fursa adhimu na wakakutana na Fidel Castro na ombi lao kubwa kwake lilikuwa ni kuwaruhusu kupitisha mizigo yao nchini kwake Cuba na nchi za jirani pasipo bugudha. Pia walimuomba aruhusu ndege zao za mizigo zitue kwenye viwanja vya ndege vya Cuba na kujaza mafuta pale inapobidi kufanya hivyo.
Castro akawakubalia kwa masharti mawili, moja ni kwamba atakuwa anawachaji mamilioni ya dola za marekani kwa huduma hizo na pili mihadarati hiyo isiuzwe ndani ya Amerika ya Kusini bali isafirishwe na kuuzwa Marekani ambapo Fidel Castro alisisitiza kuwa atafurahi akiona vijana wa Mabepari wakiharibika na mihadarati.
Masharti yote mawili haya yakakubaliwa na Pablo na Suaréz kisha wakarejea Bolivia. Baada ya kufanya mazungumzo juu ya namna watakavyo fanya biashara hatimae Pablo na Suaréz walifikia muafaka na kwa mzigo wake wa kwanza alioununua nchini Bolivia kutoka kwa Suaréz ulikuwa ni kilo 14 za unga gafi za Cocaine.
Baada ya unga gafi kufikishwa nchini Colombia kwenye mji wa MedellÃn, Pablo alikuwa ameandaa jengo maalum la ghorofa mbili ambalo alilitengeneza kuwa maabara maalumu ambapo Cocaine gafi kutoka Bolivia ilichanganywa na maligafi nyingine na kuboreshwa zaidi kikemia na hatimaye kupata Cocaine daraja la kwanza aliyoihitaji tayari kusafirishwa nchini Marekani kwa 'walaji'.
Baada ya Cocaine kutoka kwa Pablo kuingia kwenye soko la Marekani uhitaji na biashara ya mihadarati ya Cocaine ilipaa kwa kasi ya ajabu na Pablo Escobar akaanzisha rasmi genge lake la biashara ya mihadarati na akaliita MedellÃne Cartel.
Pablo akatengeneza mtandao madhubuti wa wasambazaji wa mihadarati yake katika miji ya Florida na California pamoja na majimbo mengine ya Marekani.
Pia akabuni njia mpya ya kupitisha mihadarati kupitia Bahamasi katika kisiwa cha Norman's Cay takribani kilomita 350 kusini mashariki mwa pwani ya Florida.
Ili kufanikisha zaidi azma yake Pablo Escobar alinunua nusu ya ardhi ya kisiwa cha Norman's Cay na nusu nyingine ikanunuliwa na swahiba wake wa kimarekani aliyeitwa Robert Vesco ambaye pia alikuwa ndiye anashughulikia masuala yake ya kibenki na uhasibu.
Katika Kisiwa hiki Pablo alitengeneza uwanja wa ndege, bandari, hoteli, nyumba za kuishi pamoja na ghala kubwa la jokofu maalumu kwa ajili ya kuhifadhi mizigo ya Cocaine kabla ya kuisafirisha kwenda marekani. Kwa kifupi hapa ndipo kilikuwa kitovu cha kibiashara cha Genge lake la MedellÃne Cartel.
Pablo Escobar alikuwa amepania haswa kuliteka soko la Cocaine Amerika ya Kaskazini na hii ilijidhihirisha kutokana na juhudi zake alizozifanya kibiashara ili mda wote awe hatua kadhaa mbele tofauti na washindani wenzake kibiashara.
Pablo Escobar alikuwa amepania haswa kuliteka soko la Cocaine Amerika ya Kaskazini na hii ilijidhihirisha kutokana na juhudi zake alizozifanya kibiashara ili mda wote awe hatua kadhaa mbele tofauti na washindani wenzake kibiashara.
Ili kufanikisha usafirishaji wa mizigo yake kwa ufasaha na uhakika Pablo alinunua ndege za mizigo 15 za ukubwa wa kati na helikopta 6. Pia alinunua Nyambizi ndogo mbili (submarines) kwa ajili ya kusafirisha mizigo mikubwa ya mihadarati.
Hadi kufikia mwaka 1985 Pablo alikuwa anasafirisha takribani tani 70 mpaka 80 za Cocaine kwa mwezi na alikuwa ameshikilia asilimia 80 (80%) ya soko la mihadarati la Marekani.
Na katika kipindi hiki Genge lake la MedellÃne Cartel lilikuwa linaingiza kipato cha cha Dola Milioni 70 kwa siku (Shilingi Bilioni 140 za Kitanzania) na mapato yao kwa mwaka mzima yalifikia Dola Bilioni 21.9. (Shilingi Trilioni 46 za Kitanzania).
Katika miaka ya 1990 utajiri wake binafsi ulifikia kiasi cha Dola za kimarekani Bilioni 30 ambazo ni sawa na Dola Bilioni 54 kwa hesabu za sasa (Shilingi Trilioni 110 za kitanzania)
Ni katika kipindi hiki ambacho Jarida maarufu la Forbes lilimuorodhesha Pablo Escobar kama mtu namba 5 tajiri zaidi ulimwenguni na muhalifu tajiri zaidi katika historia ya Ulimwengu.
Kutokana na nguvu na ushawishi alionao, Pablo aliteuliwa na serikali kama mjumbe wa baraza la wawakilishi la Colombia (Chamber of Representatives of Colombia) kupitia chama cha Kiliberali Cha Colombia (Colombia Liberal Party).
Moja ya majukumu muhimu aliyoyafanya akiwa kama Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kilikuwa ni kwenda kuiwakilisha Serikali ya Colombia katika sherehe za kuapishwa kwa Waziri Mkuu mpya wa Uhispania Bw. Felipe González mwaka 1982 ambapo Pablo alitumia nafasi hii ya Safari ya kiserikali nchini Uhispania kuanzisha tawi jipya la Genge lake la MedellÃne Cartel katika nchi ya Uhispania.
Hacienda Nápoles: Pepo Juu ya Uso wa Dunia
Kutokana na utajiri uliopitiliza wa Pablo Escobar alithubutu kutengeneza makazi ya kuishi ambayo namna pekee ya kuyaelezea ni kana kwamba alijitengenezea 'pepo' akiwa duniani.
Katika mji mdogo wa Puerto Triunfo, takribani kilomita 150 kutoka katika mji wa MedellÃn, Pablo alinunua eneo lenye ukubwa wa Kilomita za mraba 20 na kujenga makazi yake na familia yake na akayaita makazi haya Hacienda Nápoles (Naples Estate).
Licha ya majengo ya kifahari ya kuishi yeye na familia yake pia makazi haya yaliwekwa anasa lukuki zisizomothirika. Ndani ya makazi haya kulikuwa na Uwanja wa ndege binafsi (private airport), bustani maalumu ya sanamu za kuchonga na kufinyanga (Sculpture Park), kulikuwa na sehemu maalumu ya kuhifadhi magari ya kifahari na pikipiki za kifahari kwa ajili ya kutazama tu (collection), kulikuwa na uwanja wa mbio za magari magogo (kart racing track), kulikuwa na uwanja wa mapigano ya ng'ombe (Bullring), na pia ndani ya makazi haya kulikuwa na mbuga ya wanyama ya kutengeneza (Zoo) ambapo Pablo alikusanya aina mbali mbali za wanyama kutoka kila kona ya dunia na kuwaweka humo.
Katika geti la kuingia kwenye 'pepo' ya Pablo sehemu ya juu ya geti ilininginizwa ndege (ndege halisi) kama urembo. Ndege hii aina ya Piper PA-18 Super Cub yenye namba ya mkia HK-617-P hii ndio ilikuwa ndege ya kwanza aliyoitumia Pablo kuingiza mzigo wake wa kwanza wa Cocaine nchini Marekani.
Hapa katika 'pepo' hii ndipo ambapo Pablo Escobar aliishi yeye na familia yake.
Plata o Plomo
Moja ya vitu muhimu vya kihalifu alivyovifanya Pablo na kufanikiwa kuibuka kama kinara wa uhalifu Amerika ya kusini ilikuwa ni kutekeleza sera yake aliyoianzisha yeye mwenyewe ili kuidhibiti serikali na vyombo vya ulinzi ambapo sera hii aliita "Plata o Plomo" (silver of lead (fedha au risasi)). Akiwa na maana kwamba kama wewe ni mtu wa serikali na ikitokea mmesigana basi atakupa fedha (rushwa) kama ukikataa kupokea fedha basi anakupiga risasi.
Sera hii ilimfanya Pablo aogopwe na watendaji wa serikali pamoja na vyombo vya usalama na ikapelekea wengi kukubali 'Plata' (silver (fedha)) wakihofia kupoteza maisha endapo wangekataa fedha kutoka kwa Pablo. Hii ilimsaidia Pablo Escobar kuwa na vibaraka wengi katika serikali na vyombo vya ulinzi na usalama.
Lakini sera hii iligharimu maisha ya watu wengi sana wale ambao walikataa kupokea fedha kutoka kwa Pablo na mojawapo ya matukio mawili yanayokumbukwa sana ya utekelezaji wa sera ya 'Plata o Plomo' ni haya:-
Mosi; Uvamizi wa Mahakama Kuu ya Colombia 1985.
Mwaka 1985 baada ya mabishano ya muda mrefu bungeni kuhusu vifungu vya kikatiba vinavyokataza raia wa nchi ya Colombia kukabidhiwa kwa nchi ya kigeni akiwa kama muhalifu hatimae serikali ikafungua kesi ya kikatiba mahakama kuu ya Colombia ikitaka ruhusu ya kukabidhi baadhi ya wahalifu kwa serikali ya Marekani ikitokea wakikamatwa.
Suala hili lilikuwa linamlenga moja kwa moja Pablo Escobar kwani serikali ya Colombia ilikuwa inapewa shinikizo kubwa na Marekani kuwa wafanye marekebisho ya katiba ili iruhusu raia wa nchi hiyo ambaye ni muhalifu kukabidhiwa kwa nchi ya kigeni. Haya yalikuwa ni maandalizi endapo ikitokea Pablo Escobar akikamatwa.
Pablo akajitahidi kwa juhudi zake zote kuhonga serikalini na hata kutoa onyo kuwa mabadiliko hayo ya kikatiba yasifanyike lakini serikali iliendelea na mchakato kutokana na shinikizo walikuwa wanapata kutoka kwa marekani.
Inajulikana kwamba Pablo mara kwa mara alikuwa akiapa mbele za watu wake wa karibu kuwa kamwe hatokubali kufungwa katika nchi ya marekani na alikuwa na msemo anaoupenda kuusema kwamba "ni heri kuwa kaburini Colombia kuliko kuwa hai kwenye gereza la Marekani".
Baada ya juhudi zake zote za kuionya serikali kutobadili katiba kushindikana hatimaye Pablo akakodi kikundi cha wapiganaji wa msituni kilichoitwa M-19 ili wasaidie kumaliza tatizo lake.
Siku ya Novemba 6, 1985 majaji 25 wa mahakama kuu walikuwa katika vikao vya mwisho kujadili na hatimae waweze kuridhia mabadiliko hayo ya katiba lakini kabla ya kumaliza vikao vyao na kuridhia mabadiliko hayo walivamiwa na wapiganaji wa kikundi cha M-19.
Wapiganaji hawa walivamia na kuteka mahakama kuu kwa muda wa siku mbili na zaidi ya nusu ya majaji waliuwawa na waliosalia walichukuliwa mateka.
Majaji hawa waliochukuliwa mateka walikuja kutumiaka kama sharti muhimu la kuibana serikali waache kurekebisha katiba ili waweze kuachiwa. Baada ya serikali kukubali kuacha kubadili katiba hasa kipengele cha kukabidhi wahalifu kwa nchi ya kigeni, majaji wote waliotekwa wakaachiwa.
Pili; Mauaji Mgombea Urais Luis Carlos Galán
Tukio la pili linalokumbukwa sana la utekelezaji wa sera ya 'Plata o Plomo' lilikuwa ni mauaji ya mgombea Urais wa Colombia aliyeitwa Luis Carlos Galán. Galán alikuwa anaongoza kwenye kura za maoni nchi nzima na alikuwa anatarajiwa kushinda kwenye uchaguzi mkuu wa urais wa Colombia wa mwaka 1990.
Moja ya sera kubwa aliyokuwa anaihubiri kila kona ya nchi ilikuwa ni kupambaa na Magenge ya Mihadarati hasa hasa akililenga Genge la MedellÃne Cartel na kiongozi wake Pablo Escobar.
Pablo alimtumia barua kadhaa ambazo ziliwekwa nje ya nyumba yake kwenye kisanduku cha barua akimuonya na kumtaka aachane na sera hiyo ya kumsakama yeye pamoja na washirika wake wa MedellÃne Cartel lakini Bwana Galán alionekana dhahiri amezamilia kutekeleza sera hiyo endapo angechaguliwa kuwa rais wa Colombia.
Akiwa katika kampeni Bwana Galán alifanikiwa kufika kwenye mji wa MadellÃn ambapo Pablo alikuwa na ushawishi mkubwa na wapo wananchi waliojaribu kumuua Galán kwa kumrushia guruneti la kutupa kwa roketi (Rocket Propelled grenade) lakini kwa bahati nzuri Bwana Galán akisalimika.
Baada ya hapo Pablo akakodi wadunguaji maalumu kufatilia nyendo za Galán na akawapa amri ya kumpiga risasi mara tu wakipata upenyo wa kufanya hivyo.
Wiki kadhaa baadae akiwa kwenye kampeni katika mji wa Saocho Kiranga alipokwenda kuhutubia wafuasi wake wapatao 10,000 waliokusanyika wakisubiri kumsikia na mara baada ya kuwasili na kupanda jukwaani kuhutubia kabla hajatoa hata salamu kwa wafuasi wake alidunguliwa na risasi na kupoteza maisha papo hapo.
Tukio hili lilizua taharuki nchi nzima na imekuwa skendali yenye utata mpaka leo hii nchini Colombia kwani kuna tetesi kuwa viongozi wa serikali, polisi, pamoja na mashushushu walishirikiana na Pablo Escobar kutekeleza mauaji haya.
Licha ya Pablo kuonekana kama adui namba moja nchini marekani na baadhi wa watendaji wa serikali ya Colombia hali ili kuwa tofauti kwa raia masikini wa Colombia ambao wengi wao walimuona kama shujaa wao na katika mji aliozaliwa na kushi wa MedellÃn anaonekana zaidi ya shujaa kwani mpaka leo hii wanamuona kama ni aina fulani hivi ya masihi walipewa.
Hii inatokana na umahiri wa Pablo Escobar katika mahusiano na jamii iliyokuwa inamzunguka.
Pablo alikuwa ni mtu mwenye kusaidia masikini nchini Colombia pengine kuliko hata serikali yenyewe.
Pablo alijitolea kweli kweli katika kuboresha huduma za jamii kama vile kujenga mahospitali, shule, nyumba za wazee, nyumba za kuishi kwa ajili ya masikini na akawekeza fedha nyungi kujenga miundo mbinu ya Kanisa Katoliki na nyumba za kuabudia. Pia Pablo alijenga vya kuendeleza watoto katika mpira wa miguu, alifadhili klabu mbali mbali za wakubwa za mpira wa miguu na alijenga viwanja vya kisasa kabisa vya mpira na michezo mingine.
Ilifikia hatua mpaka Pablo alikuwa anawapa fedha taslimu wananchi wa MadellÃne ili waweze kujikimu kimaisha.
Mambo haya yote yalifanya wananchi wampende na kufumbia macho uhalifu wote aliokuwa anaufanya.
Kwa mfano katika mji wa MadellÃn ilifikia hatua kana kwamba wananchi wote walikuwa ni walinzi wake binafsi kwani walikuwa wakimtonya kila walipoona polisi wageni wakiingia hata kwa siri kwenye mji huo. Au wakati mwingine walikuwa wakitoa taarifa za uongo au kukataa kusema chochote pindi wakiulizwa na vyombo vya ulinzi kuhusu nyendo za Pablo.
Hii ilimfanya Pablo azidi kujizatiti na kuongeza mahaba kwa wakazi wa MedellÃn na raia wa Colombia kwa ujumla.Pablo ataendelea kua na mahusuano mazuri na wananchi.
VITA KUU YA KWANZA YA MAGENGE YA MIHADARATI.
Kuna msemo wanasema 'adui wa adui yako ni rafiki yako'! Swali: je, inakuwaje pale adui wa adui yako akitishia maslahi yako??
Adui wa Adui yako (Kikao cha Kwanza)
Hapo baadae nitaeleza kwa kifupi kuhusu kuibuka kwa genge lingine ambalo nalo lilishamiri katika biashara ya Cocaine lililoitwa Cali Cartel hivyo kufanya kuwe na uwepo wa magenge mawili yanayoshindana kibiashara yaani MedellÃn Cartel chini ya Pablo Escobar na Cali Cartel.
Licha ya ushindani wao wa kibiashara mwaka 1983 iliwabidi washirikiane kwa sababu za msingi kabisa. kuliibuka kikundi cha wahuni waliokuwa wanateka watu na kudai fedha kutoka kwa ndugu ili wawaachie. Baada ya kuteka ndugu kadhaa wa viongozi wa serikali wahuni hawa wakaanza kuteka ndugu wa mabosi wa Cartels na kudai pesa.
Moja ya watu muhimu waliowateka alikuwa ni Marta Nieves Ochoa dada wa moja ya mabosi wa Cali Cartel na watekaji walikuwa wanataka wapewe dila milioni 10 ili wamuachie. Hii ndio ilikuwa sababu kubwa ya mabosi wa Cali Cartel na MedellÃn Cartel kukutana ili kuweka mkakati maalumu ambao utapeleka ujumbe kwa wahuni na watekaji wote kuwa familia za mabosi wa Magenge ya mihadarati ni mwiko kuzigusa.
Katika kikao hiki cha kwanza MedellÃn Cartel na Cali Cartel waliunda kikosi kazi maalumu walichokiita Muerte a Secuestradores (Death to kidnappers (Kifo kwa Watekaji)) au kama kilivyojulikana kwa kifupi MAS.
Kila Genge lilichangia fedha, vifaa (silaha), na askari kwa ajili ya kikosi kazi cha MAS.
Kesho yake baada ya kikundi hiki kuundwa ndege ilipita juu ya uwanja wa mpira wa miguu kuliko kuwa na mechi kubwa ikifanyika na kumwaga vipeperushi kuhusu kutangaza zawadi nono kwa yeyeto atakayetoa taarifa kuhusu kufahamu lolote juu ya wahuni wanaoteka watu na kushinikiza wapewe hela. Jioni ya siku hiyo taarifa muhimu kutoka kwa wananchi zikaanza kuletwa na kikosi kazi cha MAS mara moja kikaanza kukamata wahuni wa vikundi vya utekaji na kuwatesa huku wakiwarekodi na kuwatumia wenzao wanaoshikilia dada wa bosi wa Cali Cartel.
Ndani ya siku tatu Marta Naives dada wa bosi wa Cali Cartel aliachiwa akiwa salama salimini na huo ndio ukawa mwisho wa magenge ya wahuni kuteka wanafamilia wa mabosi wa magenge ya mihadarati.
Kama ni rafiki yako, anaweza kuwa mshirika wako: Kikao cha Pili
Licha ya ushindani wa kibiashara kuendelea kuwepo kati ya Medellin Cartel ya Pablo Escobar na Cali Cartel lakini kufanikiwa kwa mkakati wa MAS kuliwapa moyo kuwa yako maeneo mengine mengi wanayoweza kufanya kwa kushirikiana na yakawa na faida kwa pande zote mbili.
Sehemu ya kwanza ambayo waliona inaweza kuwa na faida kwa pande zote mbili ilikuwa ni Cali Cartel kukubali Pablo Escobar aweze kupitisha fedha zake haramu katika benki ya First InterAmericans Bank ambayo ilikuwa inamilikiwa na maswahiba wa mabosi wa Cali Cartel. Hii ilikuwa na faida kwa kubwa kwa Pablo kwani ilikuwa ni njia rahisi na salama kwake kuweza kusafisha fedha zake haramu lakini pia ilikuwa na faida upande wa wamiliki wa benki maswahiba wa mabosi wa Cali Cartel kwani nao wangepata faida kwa kutoa huduma hiyo kwa Pablo kutokana mabilioni ya dola ya dola ambayo atakuwa anayapitisha kwenye benki yao.
Sehemu ya pili waliyokubaliana kushirikiana ilikuwa ni namna ya kuratibu bei ya Cocaine mtaani, kuratibu viwango vya ubora wa uzalishaji na njia salama za kusafirisha mizigo.
Sehemu ya tatu walikubaliana kuhusu kugawana soko. Cali Cartel wakakubaliwa kuendesha biashara kwenye jiji la New York na MedellÃn Cartel ya Pablo Escobar wakapewa Florida na Miami. Jiji la Los Angels likaachwa kama sehemu huru ambayo yeyote anaweza kufanya biashara.
Kwa pamoja wakasonga na biashara ikashamiri.
Rafiki yako anapotishia maslahi yako: Vita Kuu ya Kwanza (Pablo Escobar VS Cali Cartel).
Biashara ya madawa ya kulevya katika America ya Kusini na duniani kote kwa miaka yote imetawaliwa na vita kati ya magenge yanayopambana ili kumiliki na kujipatia ushawishi zaidi katika soko. Lakini katika historia hakuna vita ya magenge ya mihadarati iliyotisha na kuitikisa Marekani na Amerika ya Kusini kama vita kati MedellÃn Cartel ya Pablo Escobar dhidi ya Cali Cartel.
Vita hii ilitishia hata usalama wa uwepo wa Taifa la Colombia na kuleta aibu kubwa kwa serikali za Colombia na Marekani.
Lakini kabla sijaeleza chochote kuhusu vita hii, nieleze kwa ufupi tu kuhusu Cali Cartel.
The Cali Cartel
Cali Catel ilianzishwa mwishoni mwa miaka ya 1970 kikiwa kama kikundi maalumu cha wapiganaji kilichokuwa kinatumiwa na Pablo Escobar na kilijulikana kama Las Chemas.
Moja wapo ya kazi walizozifanya kwa mafanikio ilikuwa ni utekaji wa raia wawili wa nchi wa uswisi na wakalipwa kiasi cha dola laki saba.
Baada ya malipo haya washirika wa kikundi cha Las Chemas wakajitenga na Pablo Escobar na kukimbilia kusini mwa nchi ya Colombia katika mji wa Cali na wakatumia fedha hiyo kuanzisha biashara yao ya mihadarati na wakafahamika kama The Cali Cartel.
Baada ya biashara yao kuanza kukua wakafanikiwa kuwashawishi wanajeshi kadhaa waasi na kujiunga nao katika biashara na wakafanikiwa kuwapata wengi.
Uwepo wa wanajeshi katika Cali Cartel unadhihirishwa na mfumo wao wa kibiashara pamoja na uwezo wao wa kufanya upelelezi na ushushushu (counterintelligence).
Kwa mfano mfumo wao wa kibiashara ulikuwa tofauti na MedellÃn Cartel ya Pablo Escobar ambayo yenyewe ilikuwa ni genge linalomilikiwa na mtu mmoja (Pablo) ambapo Cali Cartel wenyewe walikuwa ni muunganiko wa wafanyabiashara wanaojitegemea wanaounda genge/mtandao mmoja wa mihadarati (Cali Cartel).
Kwa upande wa ushushushu na upelelezi walikuwa mahili kiasi kwamba katika baadhi ya ripoti za CIA walikuwa wanawaita kwa jina la utani "Cali the KGB", wakiwafananisha na shirika la upelelezi la Urusi ya kipindi hicho.
Turejee kwenye...'Vita Kuu'
Ushindani mkubwa wa kibiashara kati ya magenge haya mawili unaweza kuwa sababu kubwa ya wao kuingia vitani lakini hii iliepushwa kutokana na vikao vya makubaliano walivyokaa awalinkuhusu kugawana soko.
Sababu kubwa zaidi na ya msingi iliyochochea vita hii ilikuwa ni Pablo kuamua kuacha kuheshimu makubaliano akiyoingia na Cali Cartel kutokana na genge hili kujihusisha na vitendo ambavyo Pablo alivipinga kwa nguvu zote.
Haijulikani ni kichaa gani kiliwapata viongozi wa ngazi za juu wa Cali Cartel lakini ilipofika miaka ya kati kati ya 1980 Cali Carteli wakaanza kujihusisha na imani zenye utata za "Kusafisha Kizazi/jamii" (Social Cleansing). Cali Cartel walisimamia mauaji ya mamia ya watu kwenye mji wa Cali pasipo sababu ya msingi wakidai kuwa watu hao wanaichafua Cali.
Mauaji yao yaliwalenga walemavu, machangudoa, watu wanajihusisha na mapenzi ya jinsia moja, watoto wa mitaani, na watu wasio kuwa na makazi.
Baada ya kuwaua waliwaandika maandishi kifuania "Cali limpia, Cali linda" (Clean Cali, beautiful Cali (Cali nadhifu, Cali inayopendeza)
Vitendo hivi vilimkera Pablo na ikampa sababu ya kutokuheshimu makubaliano yake na Cali Cartel kuhusu kugawana soko na akaamuru watu wake wafanye biashara nchini marekani katika mji wowote ule wanaojisikia.
Kitu hiki kikiwakera viongozi wa Cali Cartel na ili kumuonyesha kuwa wamechukizwa wakaanza kutoa ufadhili kwa kikundi cha wapiganaji kilichokuwa kinajiita Los Pepes amacho ni kifupi cha Los Perseguidos por Pablo Escobar (People Persecuted by Pablo Escobar (watu walioumizwa na Pablo Escobar)).
Kikundi hiki kilikuwa kinaundwa na ndugu za watu waliouawa na Pablo au Wapambe wake na walikuwa wamejiapiza kumsaka na kumuua Pablo popote alipo. Kitendo cha mabosi wa Cali Cartel kuanza kukipa ufadhili kikundi hiki kilichochea moto wa vita ya magenge amabao haukuwahi kuonekana hapo kabla.
Katika kipindi hiki Colombia ilishuhudia mauaji ya kutisha ambapo wafuasi wa magenge yote mawili walikuwa wakitafutana usiku na mchana. Mauaji haya yaliwahusu mpaka marafiki, ndugu na wanafamilia wa makundi yote mawili. Katika mwaka 1988 pekee idadi ya vifo ilifikia zaidi ya watu 21,000 na mwaka 1989 idadi iliongezeka mpaka vifo zaidi ya 28,000.
Hiki kilikuwa ni moja ya vipindi vigumu zaidi kiusalama kwa Pablo kwani alikuwa na lundo la maadui waliokuwa wakimtafuta. Kulikuwa na serikali ya marekani inamtafuta, serikali ya Colombia inamtafuta, Kikundi cha Los Pepes kinamtafuta, na genge la Cali Cartel linamtafuta. Kutokana na suala la usalama kuwa tete mno ilimlazimu aame kutoka katika 'pepo' yake ya Hacienda Napolés na kwenda kujificha katika nyumba za maficho juu ya milima ya mji wa MadellÃn.
Ilikuwa inambidi abadili makazi mpaka mara nne kwa siku moja. Nyumba zake nyingi hizi za juu ya milima alikuwa anazitumia kuhifadhi pesa na silaha na ilitokea siku walienda kwenye nyumba yake iliyopo karibia kabisa na kilele cha mlima na ilikuwa iko ndani ya msitu mnene.
Siku hii kulikuwa na baridi lisilomithirika na kutokana na nyumba hii kujengwa maalumu kwa ajili ya kuhifadhi fedha na silaha haikuwa na mfumo wa joto wala umeme. Ilifikia kipindi cha usiku baridi lilizidi na kupitiliza kiwangi cha kawaida mpaka ikaanza kutishia afya ya mtoto wake wa kike aliyekuwa naye pamoja na familia yake.
Kutokana na kutokuwepo na namna nyingine yeyote ya kupasha moto nyumba hiyo ili kupunguza baridi, ili mbidi Pablo achome moto maburungutu ya fedha usiku kucha ili kuipatia joto familia yake na hasa mtoto wake wa kike ambaye alionekana kuathiriwa zaidi na baridi. Mpaka asubuhi kunakucha na baridi kupungua kufikia kiwango cha kawaida Pablo alikuwa ameteketeza maburungutu ya hela ya kiasi cha dola milioni mbili za kimarekani.
Baada ya Juhudi za Cali Cartel kumpata Pablo kutozaa matunda, walitoa kandarasi kwa Jorge Selcado ambaye alikuwa ni muhandisi na Mwanajeshi. Jorge alikuwa maarufu kwa kuandaa timu maalumu za mauaji ya kuratibiwa kiumakini (assassination teams) na mara zote mipango yake inakuwa ya mafanikio.
Baada ya Jorge kupewa 'ofa' hii na mabosi wa Cali Cartel aliwasiliana na watu wake ambao walikuwa ni wanajeshi wa kukodi (mercenaries) kutoka nchini uingereza ambao walikuwa wamewahi kutumikia katika jeshi la Uingereza kitengo maalumu cha Anga (SAS - Special Air Services).
Timu hii ilikuwa na watu kumi mbili na iliwasili Colombia na kufanya mazoezi kwa miezi kadhaa ili kujiandaa na zoezi lililopo mbele yao. Walifahamu kuwa kwa kipindi hicho Pablo alikuwa amejificha mahali kusiko julikana kwenye milima, hivyo walisubiri wapate taarifa kuwa amerejea kwenye 'pepo' yake ya Hacienda ili wafanye shambulio la kushitukiza.
Siku hiyo haikuchelewa sana kwani timu ya Mpira ambayo Pablo alikuwa anaishabikia na kuifadhili ilifanikiwa kuchukua ubingwa wa ligi kuu ya Colombia. Hivyo Pablo alirejea jijini MedellÃn ili ajumuike kusherehekea ushindi huo.
Kikosi hiki kilichotumwa kumuua Pablo walijiandaa na Chopa mbili za kivita zilizobeba silaha nzito na mpango wao ulikuwa wamshitukize Pablo nyakati za asubuhi na kufanya shambulizi nyumbani kwake Hacienda Napolés.
Ili mpango huu uwe na ufanisi walikubaliana kuwa washambulie kutokea nyuma ya milima na chopa ziruke katika mfumo maalumu wa kijeshi wa usawa wa chini chini kabisa (nap-to-earth) ili wasiweze kuonekana kutokea mbali.
Keshi yake chopa ziliruka kuelekea Hacienda Napolés kama walivyopanga wapitie nyuma ya milima huku zikiruka chini chini, lakini wakiwa kwenye milima hiyo kwa bahati mbaya chopa moja ilimshinda rubani kutokana na kuruka chini chini na ikagonga kwenye mlima na kudondoka.
Zoezi ambalo kilipangwa kuwa la kwenda kushambulia na kumuua Pablo likageka kuwa ni zoezi la uokoaji na mpango huu ukaishia hapo hapo.
Zoezi ambalo kilipangwa kuwa la kwenda kushambulia na kumuua Pablo likageka kuwa ni zoezi la uokoaji na mpango huu ukaishia hapo hapo.
Baada ya kufeli kwa zoezi hili serikali ya Colombia iliwasiliana na Pablo kujaribu kumuomba ajisalimishe.
Waliharibu kumbembeleza kwa kila namna ambayo waliweza na kumuahidi watakubaliana na masharti yoyote atakayoyasema. Serikali ilifikia kipindi walikuwa 'desperate' kutokana na aibu waliyokuwa wanaipata kimataifa kwa kushindwa kumdhibiti muhalifu mmoja aliyeifanya nchi yao ya Colombia mpaka kubatizwa jina la 'Capital of death' (mji wa kifo). Hivyo matamanio yao ilikuwa tu kuutangazia ulimwengu kuwa wamemkamata Pablo.
Baada ya Pablo kutafakari kwa kina na kuona jinsi usalama wake na familia yake kuwa ni mdogo kutokana na maadui wanaomzunguka kila kona akakubali ombi la serikali kujisalimisha lakini akawapa masharti matatu.
Moja, kipindi hicho serikali ilikuwa imefanya mchakato na kubadili kifungu cha katiba kuruhusu kukabithi raia wake kwa nchi za kigeni (extradition). Pablo akawaeleza waitishe kikao maalumu cha Bunge na kurudisha kifungu cha zamani kinachokataza raia wa nchi hiyo kukabidhiwa kwa nchi za kigeni. Serikali ikakubaliana na sharti hili. Kikaitishwa kikao maalumu cha bunge na kifungu hicho cha katiba kikarejebishwa.
Pili, Pablo aliwapa sharti kuwa anataka atengenezewe gereza maalumu katika sehemu atakayoichagua yeye na yeye na wahandisi wake ndio watakaochora michoro ya namna gereza hilo anavyotaka liwe. Serikali wakakubaliana na sharti hili na gereza kikajengwa kama ambavyo Pablo aliamuru.
(Tafadhali rejea aya ya kwanza ya makala hii kuhusu namna ambavyo gereza hili likikuwa tofauti na gereza lingine lolote duniani).
Gereza hili lilipo malizika Pablo mwenyewe alilipa jina La Catedral (The Cathedral) lakini watu wengi walilipa jina la utani 'Club Escobar' na wengine waliliita 'Hotel Cathedral'.
Sharti la tatu aliwaambia serikali yeye ndiye atakaye chagua askari wa kumlinda. Serikali ikakubali pia sharti hili.
Baada ya masharti yote kukamilika yakafanyika makubakiano maalumu ya kisheria ambapo Pablo Escobar licha ya uhalifu wa kutisha alioufanya kwa miaka karibia ishirini alipewa adhabu ya kifungo cha miaka mitano pekee.
Baada ya makubaliano. Pablo alijisalimisha na kupelekwa kwenye makazi yake mapya, gereza la La Catedral.
Baada ya Pablo kujisalimisha mwaka 1991 serikali ilitangazia ulimwengu kwa mbwembwe zote kuwa wamemkamata Pablo Escobar na amehifadhiwa katiba gereza la siri.
Ikikuwa ni kweli kuwa Pablo alikuwa gerezani lakini ulimwengu mzima walifichwa ukweli halisi kwani katika gereza hilo Pablo aliishi kama mfalme na aliendelea kutoa maagizo kwa wafuasi wake na kuendesha biashara yake ya miahadarati akiwa ndani ya La Catedral. Tena kwa sasa Pablo inawezekana alifurahi zaidi kwani alikuwa uhakika wa usalama wake kutokana na kulindwa na jeshi la serikali ambao wao walimuona kama mfungwa huku yeye akiwaona kama walinzi wake binafsi.
Kitendo hiki kiliwaumiza sana Cali Cartel ambao walihangaika usiku na mchana wafahamu hili gereza lilipo. Baada ya mwaka mkoja wakapata taarifa kuhusu mahala ambapo gereza anahifadhiwa Pablo. Kutokana na ulinzi mkali wa kijeshi waling'amua fika kuwa hawataweza kuvamia gereza hilo na kumuua Pablo hivyo mshauri wao wa masuala ya kijeshi akawashauri Jorge Selcado akawashauri kuwa namna pekee ya kumuua Pablo ndani ya La Cathedral ni kulipua gereza hilo kwa mabomu mazito kwa kutumia ndege maalumu ya kivita.
Cali Cartel wakanunua ndege ya kivita aina ya A-37 Dragonfly na wakaweza kupata dili la magendo kuuziwa mabomu mazito ya kivita ya uzito wa paundi 500 kutoka kwa generali wa jeshi ka El Salvador.
Hivyo Jorge akarusha ndege na kuelekea El Salvador katika uwanja wa ndege wa kiraia asubuhi alfajiri ili kuchukua mabomu.
Kwa bahati mbaya mabomu hayo yalikuwa kwenye maboksi makubwa manne na ndege aliyoenda nayo Jorge ilikuwa ndogo isingeweza kubeba maboksi yote hayo. Wakahangaika kunga'aniza maboksi yaenee ndani ya ndege lakini maboksi matatu pekee ndiyo yalienea. Zoezi hilo la magendo lililopaswa kuchukua dakika chache tu likatumia zaidi ya dakika ishirini ambapo palianza kupambazuka na watu kufika uwanjani hivyo ikambidi Jorge aruke na maboksi matatu na kulitelekeza boksi moja uwanjani hapo.
Baada ya raia kushikwa na butwaa kuhusu walichokiona hatimae polisi walifika na baada ya masaa machache walipewa taarifa za siri kuhusu mpango huo wa Cali Cartel kununua mabomu hayo ili kulipua La Catedral. Skandali hii iliteka vyombo vya habari siku hiyo na ikapekekea Cali Cartel kuachana na mpango huo wa kulipua La Catedral waliamini kuwa taarifa hiyo itakuwa imemfikia Escobar na ameshachukua tahadhali.
KIFO CHA PABLO El Mágico
Licha ya serikali kufahamu kuwa Pablo alikuwa anaendelea na biashara zake licha ya kuwa ndani ya gereza serikali ilifumfumbia macho kadiri ambavyo ulimwengu ulivyo amini kuwa Pablo Escobar yuko gerezani anajutia.
Lakini uvumilivu huu uliisha mara baada ya kuzuka skendali katika vyombo vya habari kwamba Pablo aliwaita marafiki zake wa kibiashara wanne walioko uraiani waende akawape maelekezo, walipofika huko aliamuru walinzi wanaomlinda wawapigwe risasi marafiki zake hao kwa madai kuwa wamemdhulumu hela na ilisemekana miili yao ilifukiwa ndani ya gereza.
Skandali hii ilikuwa kubwa kiasi kwamba ilitishia kurudisha tena upya zama za serikali kuumiza kichwa kuhusu Pablo. Ili kuepusha mambo yasiharibike kabisa serikali ikaamua kuwa Pablo inabidi afungwe kwenye gereza maalumu la kijeshi na aishi maisha ya kifungwa kama mfungwa mwingine yeyote.
Kutikana ma makubaliano kuwa polisi wengine isipokuwa wanajeshi wanaomlinda hawaruhusiwi kusogea hata maili 12 karibu na La Catedral, hivyo serikali ikatuma waziri muandamizi na maafisa wengine watatu wa ngazi za juu serikalini kumpelekea taarifa hiyo Pablo kuwa anaamishwa gereza.
Baada ya kupewa taarifa hii Pablo akiwageuzia kibao na kuamuru wanajeshi wanaomlinda waweke chini ya ulinzi vuongozi hao wa serikali. (Kumbuka wanajeshi hawa wanaomlinda aliwachagua yeye hivyo ni dhahiri walikuwa maswahiba wake wakikuwa tayari kumtii Pablo kuliko rais wa nchi)
Baada ya taarifa kufika serikalini kuwa Pablo amewaweka chini ya ulinzi viongozi wa serikali waliotumwa kufanya nae mazungumzo juu kuhamishwa gereza. Serikali ikatuma kikosi cha wanajeshi 600 kulizunguka gereza hilo na kumtaka Pablo ajisalimishe.
Pablo akawajibu kuwa wakithubutu hata kukanyaga hatua moja ndani ya uzio wa La Catedral basi ataamuru viongozi hao aliowashikilia mateka wapigwe risasi.
Mabishano haya yalidumu kwa takribani masaa kumi mpaka ambapo giza lilipoingia kikosi cha wanajeshi waliokuwa wamelizunguka gereza walivamia ndani ya La Catedral lakini jambo la ajabu waliwakuta viongozi hao wa serikali wamefugwa kwenye viti na kuzibwa midomo lakini walikuwa salama salimini ila Pablo na wapambe wake hawakuwepo. Na watu waliokutwa ndani ya La Catedral walidai Pablo na wapambe wake hajaonekana/ameondoka kwa taribani masaa manne yaliyopiata.
Ni kwa jinsi gani Pablo aliwatoroka wanajeshi amabo walikuwa wamelizunguka gereza kila kona kitendawili hiki mpaka leo hakuna aliyekitegea. Hakukuwa na njia yoyote ya chini kwa chini wala handaki, hivyo huu utata wa jinsi alivyowatoroka haujapata jibu la kuridhisha mpaka leo.
Kufumba na kufumbua jinamizi la aibu kwa serikali ya Colombia na Marekani kilikuwa limerudi. Na serikali zote mbili ziliapa kwamba sasa imetosha ni lazima walizike jinamizi hili.
Kamandi ya Oparesheni maalumu za kijeshi za marekani (Joint Special Operations Command) kikaunda kikosi kazi maalumu cha kijeshi kilichoelekea nchini Colombia kuungana na kikosi maalumu cha jeshi la Colombia kikichoundwa maakumu kwa ajili ya kumsaka Pablo kilichoitwa 'Search Block' na kwa pamoja wakaanza msako mkali wa kumtafuta Pablo. Pia walishirikiana na kikundi cha Los Pepes kilichoapa kumteketeza Pablo na ukoo wake wote ambao walitumia mwanya wa msako huu kuua watu 300 waliokuwa na uhusiano na Pablo, yaani ndugu zake, marafiki na wafanyabiashara wenza.
Baada ya mwaka mzima wa msako mkali hatimae siku ya desemba 2, 1993 jeshi la Colombia lilifanikiwa kunasa mawasiliano ya simu kati ya Pablo na wasaidizi wake. Wakatumia 'triangulation technology' kung'amua mahali alipo ambapo alikuwa katika mtaa wa Los Olivos katika mji wa MadellÃn. Baada ya kufanikiwa kufahamu nyumba aliyojihifadhi pasipo kupoteza mda wakafanya shambulio la kushitukiza.
Wakati wanawafanyia shambulio hili la kushitukiza Pablo alikuwa yupo na mlinzi wake binafsi mmoja tu Alvaro de Jesús.
Baada ya kuanza kushambuliwa nao wakarudisha mashambulio ya risasi kwa vikosi vya jeshi la serikali. Majibizano haya ya risadi yalidumu kwa dakika kadhaa ndipo Pablo na mlinzi wake wakakubali kuwa hakuna namna wao watu wawili wataweza kuwashinda kikosi kizima cha kijeshi chenye silaha nzito. Hivyo wakaamua warushe risasi huku wakiwa wanakinbilia juu ya paa la nyumba. Lakini kabla hawajafika juu kabisa ya paa la nyumba mlinzi wa Pablo alidunguliwa na risasi na kufariki papo hapo na Pablo mwenyewe alipigwa risasi mguuni na akajikongoja mpaka juu ya paa.
Baada ya wanajeshi wa serikali kuvamia nyumba na kufika juu ya paa walimkuta Pablo amelala chini amefariki akiwa na tundu la risasi aliyopigwa kwenye sikio kwenda ndani ya kichwa.
Haijulikani ni nani alimpiga hii risasi lakini marafiki zake wa karibu pamoja na kaka yake wa kuzaliwa wanasema kwamba siku zote Pablo akikuwa anasema kuwa hatokubali kupigwa risasi ya mwisho na adui yake. Kama ikitokea ameshambukiwa na adui na hana namna ya kujiokoa basi atajipiga risasi sikioni itokee upande wa pili. Serikali haijawahi kupinga au kuthibitisha suala hili la Pablo kujipiga risasi mwenyewe lakini huo ndio ulikuwa mwisho wa Pablo juu ya uso wa dunia.
Mpaka leo hii nchini Colombia hasa katika mji wa MadellÃn kila mwaka wanafanya kumbu kumbu ya kifo cha Pablo kama shujaa wao lakini kwa watu wengi duniani Pablo amebakia kama muhalifu aliyeitesa na kuisumbua dunia kadiri atakavyo.
Binafsi nadhani namna nzuri ya kumkumbuka Pablo ni sentesi moja maridhawa iliyotolewa na Virginia Vallejo aliposema; Amando a Pablo, Odiando a Escobar.! Akimaanisha kuwa lazima kuna upande fulani wa nafsi yako utampenda Pablo kama mtu mwenyenye jitihada, umahiri na uthubutu lakini upande wa pili wa nafsi lazima utamchukia Escobar kutokana na uhalifu wake.
Lakini kwa namna yeyote ile historia ya Dunia itaendelea kumkumbuka Pablo kama binadamu aliyeufinyanga ulimwengu wa siri na hatari wa biashara haramu na kuufanya uwe jinsi ulivyo leo hii. Vizazi vyote vijavyo vitaendelea kusimulia historia ya kusisimua ya Pablo El Mágico. Pablo El Zar de la CocaÃna. Pablo Emilio Escobar
Tags