Hotuba Ya Mgombea Wa Urais Wa Zanzibar Dk Hussein Ali Hassan Mwinyi ,kisiwani Pemba

Top Post Ad



Nianze kwa kumshukuru Mwenyezimungu, mwingi wa rehma kwa kutuwezesha kukutana hapa hii leo. Kuwashukuru wananchi wa Pemba kwa mapokezi makubwa sana. Napata faraja kazi yetu sasa itakamilika mapema sana.

Nashukuru chama kwa kumaliza uteuzi wake kwa kwa haki, na sasa sote tumekua wamoja, hakuna timu Mwinyi wala timu Mbarawa, na lengo letu sasa ni moja kushika dola.

Kabla ya yote tuwaombee wale waliopata maafa Mwenyezi Mungu awarehemu, na wengine waliopata ajali ya kuezuliwa mapaa nyumba zao Mungu awafariji.

Sitosema mengi. Muwe na hakika nitaenzi Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964. Nitadumisha Muungano wetu ni wa aina yake, na unatiliwa mfano duniani kote.

Kuna suala kubwa, nalo ni suala la amani na ndio maana tunapata maendeleo. Nchi nyingi za jirani zetu hakuna amani. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais Dk.Ali Mohamed Shein kwa kuongoza nchi kwa amani.

Jukumu langu ni kuhakikisha amani inadumu. Lazima tudumishe umoja wetu. Kusiwe na Upemba na Uunguja, kusiwe na ukusini na Ukaskazini.

Sote ni Wazanzibari. Suala la ajira tutalishughulikia hasa kwa vijana. Niwapongeze hasa Rais Dkt. Shein na viongozi wote wa serikali na chama.

Nihakikishe alipoachia yeye nitaendeleza. Nitaendeleza miundombinu, huduma za jamii, ustawi wa watu, maendeleo ya jamii, afya, elimu, na yote yanayogusa watu. Nitahakikisha Mzazibari anakua  na maisha bora.

Ukitaka kuyafanya hayo, lazima uwajibike. Huwezi kuwa na program kukawa na wala rushwa, wabadhirifu, Wazembe. Sitokua na huruma kwa wenye tabia hizo. Serikali itafanya kazi kwa maslahi ya Wazanzibari wote.

Wapo wanaosema Mwinyi ni mpole. Mimi Nasema wataniewa.

Nasema haya kwa sababu pengine hamjanisikia nikiongea sana kwenye vyombo vya habari. Sababu kubwa ni kwamba Wizara ya Ulinzi huko mambo yetu ni ya siri hatufanyi hadharani. Siwezi kusema ila kwa wale wabadhirifu,wala rushwa, wazembe, wasiowajibika, hao watawajibika.

Nitasimamia maslahi ya Zanzibar kwenye Muungano, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya za Kimataifa.

Nikwambieni nimeamua nigombee na ili  nitakaposhinda dhamira yangu ni moja kuwatumikia Wazanzibari wote.

Tukishika dola, tutakuja na miradi ya kusaidia Wazanzibari ikiwemo ajira kwa wote bila ubaguzi.

Panapo dhamira njema Mwenyezi Mungu atatupa neema.

Mwaka huu, tunataka tupate ushindi wa kishindo usiwe mwembemba tukapata malalamiko. Na niliyoyaona Unguja na hapa Pemba kwa sasa sina shaka ushindi ni mkubwa. Sina shaka ushindi utakua ni mkubwa.

Nasema tena kwamba ‘Yajayo yanafurahisha.’ Ni ahadi naichukua mbele ya Mungu na mbele yenu. Nitahakikisha nawahudumia wananchi.

Sasa na wakati huu nina hakika tunafanya  mambo mazuri kwa maisha yetu yawe mazuri . Kazi iliyobakia ni kwenda kushika dola na si vyenginevyo. Kwa sasa lililobakia ni umoja mshikamano na ushirikiano ndani ya CCM.

Katika risala ya mikoa miwili ya Pemba ya Kusini na Kaskazini salamu nimezipokea na kuondoka Pemba nikiwa na faraja kubwa hivyo hayo yanaonekana ni mapenzi ya dhati ninaahidi kuitumikia Zanzibar kwa moyo wangu wote. Ihsani hulipwa kwa Ihsani .

Maneno yanayosemwa na wagombea kama wametumwa na Hussein , nataka kuwaambia hapa leo, sijamtuma mtu, kila mtu apambane na hali yake, maana wengine wanasema eti wachaguliwe ili nitakapounda Baraza la
Mawaziri, niwateuwe, nawaambia sijamtuma mtu.

Nataka kurudia maneno aliyosema Kama Makamu Mwenyekitu wetu Rais Dkt Shein kuwa tutumie uchaguzi huu ndani ya Chama kupata wagombea bora.

Baada ya kusema hayo sasa naomba nimalizie kwa kuwashukuru wana CCM na wananchi wote waliojitokeza katika mapokezi yetu na hapa uwanjani.

 Zanzibar ni njema atakae aje

Below Post Ad

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.