Huyu Hapa Mpigania UHURU Aliyefariki Muda Mfupi Baada ya Uhuru



MIAKA 50 iliyopita, Septemba 17, mwaka 1962, Hamza Kibwana Bakari Mwapachu, baba yake na Harith Bakari Mwapachu, Rahma Mwapachu, Juma Volter Mwapachu, Wendo Mtega Mwapachu, Tunu Mwapachu na Jabe Jabir Mwapachu, alifariki dunia mkoani Dar es salaam. Alifariki katika umri mdogo wa miaka 49, wakati huo alikuwa Katibu Mkuu Msaidizi katika Wizara ya Mambo ya Ndani.

Akiwa amezaliwa Tanga, marehemu Hamza alisoma elimu yake ya shule ya msingi na sekondari mkoani Tanga baada ya darasa la nne, wakati huo ikiwa ni elimu ya sekondari ya kiwango cha juu Tanganyika.

Baada ya hapo alisomea mafunzo ya utabibu, katika Shule (Hospitali) ya Uganga ya Sewa Haji, mkoani Dar es Salaam na kuhitimu cheti cha mganga msaidizi, mwaka 1935. Mwaka 1937 alipelekwa kuwa mwalimu wa shule ya uganga mkoani Mwanza iliyokuwa ikifundisha wafanyakazi wasaidizi wa uganga. Akiwa Mwanza alikutana na Juliana Volter ambaye alifunga naye ndoa mwaka 1938.

Akiwa mwenye malengo makubwa ya kufanikiwa, alijiunga na Chuo cha Makerere, mwaka 1943 kusomea stashahada ya udaktari. Wakati huo, Makerere hawakuwa wakitoa shahada ya aina yoyote.

Kama historia ilivyojionyesha, Hamza na Julius Nyerere walijiunga na Chuo cha Makerere wakati huo na kuanzisha safari yao ya urafiki wa karibu pamoja na uhusiano kisiasa, bila kujali tofauti ya umri wa miaka tisa kati yao.

Wakiwa Makerere wawili hao walianzisha urafiki na Andrew Tibandebage, mwanafunzi mwingine aliyekuwa akisomea kozi ya ualimu akiwa mwaka mmoja mbele yao chuoni na watatu hao walianzisha umoja wa kupigania ustawi wa kisiasa wa wanafunzi kutoka Tanganyika, mwishoni mwa mwaka 1943.

Waliomba umoja wao utambulike kuwa na uhusiano na Tanganyika Africa Association (TAA), maombi ambayo hayakujibiwa na makao makuu Dar es salaam.

Mara baada ya kuhitimu mafunzo yao mwaka 1945, wote Hamza Mwapachu na Julius Nyerere walikutana tena mkoani Tabora, wakati Hamza akiwa ni mtumishi wa Hospitali ya Serikali na Nyerere akiwa mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Maria, Tibandebage akiwa ni mwalimu tayari.

Watatu hao walijiunga na Chama Cha TAA, tawi la Tabora na ilipofika mwaka 1946, walitwaa uongozi wa TAA, Hamza akiwa Mwenyekiti, Nyerere Katibu na Tibandebage Mweka Hazina.
Ni wakati huo ambapo Hamza alijikuta taaluma yake ya utabibu ikishindwa kumpa nafasi pana ya uelewa uliohitajika kuhusu mienendo yenye mabadiliko ya kisiasa na kikatiba, ili kuweza kumudu mashambulizi ya wakoloni kwa wakati huo.

Hivyo basi mwaka 1947, aliachana na fani ya utabibu na kujiunga katika Chuo Kikuu cha Wales ya Kusini huko Cardiff, kusomea Stashahada ya Kazi ya Kijamii.

Wakati akiwa Uingereza, Hamza alivutiwa sana na siasa za Chama Cha Labour na Usoshalisti baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Vilevile alijiunga na jamii ya Fabian, wakati huo ikijulikana kama Fabian Colonial Bureau na akaanzisha mtandao wa marafiki wa karibu ambao mpaka Hamza anafariki ndiyo waliokuwa mara kwa mara wakimpelekea vitabu na machapisho mbalimbali ambayo yalimjengea uwezo wa kisiasa.

Aliporudi Tanganyika mwaka 1949, Hamza alipangiwa kufanya kazi ofisi ya Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, kama afisa msaidizi mambo ya ustawi wa jamii.

Mzee Rashid Mfaume Kawawa, ambaye alikuwa amehitimu elimu ya darasa la nane wakati huo mkoani Tabora mwaka 1948, alifanya kazi na Hamza kama msaidizi wa ofisi.

Huku akiwa na uelewa wa elimu ya sheria na mambo ya kikatiba na siasa, bila kupoteza muda, akarejesha uhusiano na rafiki yake Nyerere mkoani Tabora, ambaye wakati huo Nyerere alikuwa ndiye Rais wa TAA Tawi la Tabora, lakini pia akijiandaa kwenda Edinburgh kwa masomo ya shahada baadaye mwaka huo, hivyo Hamza alibaki kuwa ndiye sauti thabiti ya siasa za TAA, mkoani Dar es Salaam.

Huku akiungana na Abdulwahid Kleist Sykes, mtu ambaye alikuja kuwa kama kaka wa damu wa Hamza, walitengeneza kikundi cha utekelezaji wa mabadiliko ndani ya TAA, kutoka taasisi ya ustawi wa jamii na kuwa moja kwa moja taasisi ya kisiasa.

Waliowaongeza ndani ya kundi lao akina Dk. Lucian Tsere, Dk. Vedast Kyaruzi, Stephen Mhando na John Rupia. Mapema mwaka 1950, Abdul na Hamza kwa mikono yao walivamia makao makuu ya TAA, Dar es Salaam wakitumia ngumi na kurusha viti na kuongoza mapinduzi ya uongozi wa TAA.

Walimweka madarakani, Dk. Tsere kuwa Rais wa mpito wa TAA. Hata hivyo, kutokana na Dk. Tsere kupewa uhamisho kwenda Tanga, TAA ilifanya uchaguzi rasmi wa uongozi. Dk. Vedast Kyaruzi alichaguliwa kuwa Rais, Abdulwahid Sykes Katibu Mkuu, John Rupia Mweka Hazina, Hamza alichaguliwa kuwa Katibu wa Uchumi na Stephen Mhando akawa Katibu wa Elimu.

Uongozi mpya wa TAA uliendelea kupitia upya Katiba ya TAA katikati ya mwaka 1950 na kuipa taswira ya chama cha kisiasa. Kazi ya kwanza kubwa ya uongozi huo mpya ilikuwa kutayarisha makubaliano yaliyowasilishwa Umoja wa Mataifa, yaliyokuwa na dhamana ya kuisimamia Tanganyika mwishoni mwa mwaka 1950, ambayo yalidai mwelekeo wa wazi kuelekea Uhuru wa Tanganyika. Makubaliano hayo yalikuwa ni taarifa ya pamoja ya uongozi wa TAA, lakini mtayarishaji mkuu wa hati alikuwa Hamza Mwapachu.

Kutokana na uwasilishaji wa hati hiyo, Gavana Edward Twining, wakati huo aliwatenganisha watu wawili kuepusha madhara ambayo yangeipata serikali ya kikoloni. Dk. Kyaruzi alihamishiwa kutoka Hospitali ya Sewa Haji, wakati huo ikiwa ndiyo iliyokuwa Hospitali ya Taifa na kupelekwa Kingolwira - Zahanati ya Gereza mkoani Morogoro, kuwatibu wafungwa.

Hamza Mwapachu alipelekwa "uhamishoni" Kisiwa cha Ukerewe, kilichopo katikati ya Ziwa Viktoria. Dk. Kyaruzi aliutafsiri uhamisho huo kama "kifungo chenye sura iliyojificha".

Hamza kwa upande mwingine aliuona uhamisho huo kama fursa nyingine ya kuwa karibu na mahali ambapo siku zote aliamini ni kitovu cha chemchem ya siasa za Tanganyika, Kanda ya Ziwa Victoria.

Kwa mfano, mapema akimuandikia Nyerere huko Edinburgh mwishoni mwa mwaka 1951, Hamza alionyesha furaha yake alipomgundua kijana makini Paul Bomani, mkoani Mwanza ambaye angekuwa "mtaji muhimu katika mapambano ya kisiasa".

Mbali na hilo, nyumba ya Hamza ilitumika kama mahali ambapo vikao vya kisiasa vilifanyika kipindi chote tangu mwaka 1952 hadi 1954 ambapo yalifanyika mazungumzo juu ya namna ya kumfanya Nyerere achukue uongozi wa TAA, mwaka 1953 na baadaye kuundwa kwa TANU.

Hali hii ilisababisha serikali ya kikoloni wakati ule kumnyima Hamza ruhusa ya kusafiri kutoka Kisiwa cha Ukerewe kwenda Dar es Salaam, kuhudhuria mkutano ulioanzisha TANU hapo Julai 7, mwaka 1954. Kwa vyovyote vile, Hamza alikuwa ni mwanzilishi na muasisi wa TANU ingawaje hakuhudhuria tukio lile.

Mapema mwaka 1955, aliteuliwa kuwa Afisa Msaidizi Tukuyu, Wilaya ya Rungwe, nafasi iliyoonekana kama ni kupandishwa cheo lakini ilikuwa chini sana ya aliowatangulia, tena sehemu ya mbali ya Tanganyika na ambayo ni mbali na vitovu vya siasa za kizalendo.

Hata hivyo alipokuwa Tukuyu, aliungana na Yatuta Chisiza, wakati huo akiwa Mkuu wa Polisi, na siasa za kupigania uhuru wa Malawi ziliamsha ari ya wapigania uhuru hao wawili.

Baadaye Chisiza alihamishiwa mkoani Iringa, mahali ambapo kijana wake (Hamza), Juma Mwapachu, alikuwa akifikia akiwa safarini kwenda Shule ya Bweni Morogoro akitokea Tukuyu, mwaka 1957.

Chisiza alikuwa Waziri wa kwanza mzalendo akiongoza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Malawi huru. Aliuawa akiwa kwenye jaribio la kupindua utawala wa Kamuzu Banda, Rais wa Malawi aliyekuwa kibaraka wa serikali ya kikaburu ya Afrika Kusini.

Mwaka 1958, alihamishiwa Dar es Salaam kutoka Shule ya Serikali za Mitaa Mzumbe, Morogoro, mahali ambapo alikuwa rafiki wa karibu sana na Khalfan Mrisho Kikwete, pamoja na Cecil Kallaghe.

Alikuwa ni Msaidizi wa kwanza wa Nyerere akiwa Waziri Kiongozi. Mambo hujurudia! Nyerere alimtaka rafiki yake aliyemwamini awe ndiye mshauri wake mkuu baada tu ya uhuru wa Tanganyika.

Mara balaa likaanza. Hamza alianza kuonyesha hali mbaya ya ugonjwa wa moyo katikati ya mwaka 1960. Hamza alikuwa ni mvutaji mkubwa wa sigara kipindi chote cha maisha yake.
Na mpaka Hamza anafariki dunia, Nyerere alifanya aliloweza kuokoa maisha ya rafiki yake. Hamza alipelekwa hospitali bora duniani ya Hammersmith Post Graduate, London, huko alifanyiwa upasuaji wa moyo.

Hata hivyo, Septemba 1962, moyo wake ulikuwa dhaifu na kushindwa kuhimili mikikimikiki ya kazi za mfululizo ambazo alikuwa nazo katika kulitumikia taifa lake jipya huru. Hamza alifariki dunia akiwa Hospitali ya Princess Margaret, sasa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Septemba 17, mwaka 1962.

Akimuandikia mke wa marehemu Bibi Juliana Mwapachu, Septemba 28, mwaka 1962, ikiwa ni majuma mawili baada ya kifo cha Hamza, Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Dunstan A. Omari, kwa maneno machache aliweza kusema: "Nimemfahamu Hamza kama rafiki yangu kwa miaka mingi na nisingeweza kutamani rafiki mwingine mwenye haiba na ushirikiano zaidi ya yeye. Kifo chake ni pigo lisiloweza kuzibika."

Mungu aendelee kuilaza roho yake mahali pema peponi. Amin.

Post a Comment

4 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Mm! Kwa kweli huu uhuru kamwe tusiuchezee. Maana uliwagharimu wazee wetu waliotutangulia. Nimejifunza mengi juu ya taifa letu kipenzi kupitia toleo hili. Ingawa Hamza hakujaliwa kuishi miaka mingi, ametuachia urithi wa alichokuwa akikipigania yeye pamoja na wenzake. Leo tunatembea hadi ukerwe kwa uhuru tofauti na ilivyokuwa katika wakati wa ukoloni. Ukoloni ni mbaya. Ukoloni mkongwe na ukoloni mamboleo visipewe milango tena. Nimefurahi kujua kumbe Hospital ya muhimbili zamani iliitwa Princess Margaret Hospital. Aliyeandika toleo hili, atuandikie na kitabu. Ili sisi na vizazi vifuatavyo tujue tulikotekea na tuyajue waliyokutana nayo wazee wetu ili kuikomboa Tanganyika kutoka kwenye mikono ya wakoloni.

    ReplyDelete
  2. Labda ningependa kuongeza kidogo huyu Mwapachhu ndiyo wenyefikira na chama cha TAA Hataa kbla ya mwalimu J.K hajaanza kuingia katika haraka mpakaalipopewaBarua na wenzake kuileta Daresalam kwa kina Fundiira na mwapachu.

    Histoia yetuni bora na vizuri tuiandike vizuri vilivyo wakati bado tuko hai.

    Agwe Kabudi, to uwalonjele wadodo , waimanyile viswano. kina Joni Rpia na kina Tewa ,JOBUU Lusinde na wengitulio kuwa nao mtaa wa Tandamti.

    Ukiizungumia historia yetu mwalimu anakujja baadae hata mama Maria anaijua vizuri.

    LONG LIVE TANZANIA

    ReplyDelete
  3. Kweli tukiwa bado hai mnsoijua historia mujikusanye muiandike. Wengi wanajua tu tulipata uhuru bila kumwaga damu. Lakini hawajui hadha gani waliyopitia wazee hao hadi kufikia uamuzi wa kudai uhuru. Pengine, dhana ya bila umwagaji wa damu inaweza kufanya wengi wafikirie tumepata uhuru wetu kirahisi na hivyo ni jambo rahisi sana kupata uhuru wa nchi. Nafikiri hii inaweza kuwafanya watu wenye tamaa wasione umuhimu wa kuutunza uhuru wa taifa, sababu ni jambo jepesi kulipata endapo litatuponyoka. Kuna wazee Mwalimu aliwahi kuwataja kwenye hotuba zake kwamba ndio walikuwa mstari wa mbele Katika kudai uhuru. Naomba kuuliza wana historia na watu wa mambo ya kale, zipo wapi statues za watu hao? Kule Songea zipo statues za mashujaa wa kingoni walionyongwa na wajerumani na kuzikwa kaburi moja. Naomba kuuliza serikali ya Tanzania ina Mpango gani kuidai ujerumani kwa maonezi hayo? Mbona Kenya wsmeshalipwa fidia kwa wale wa maumau? Mbona wayahudi waliouwawa halaiki huko Poland na wajerumani nasikia waneshalipwa na serikali ya ujerumani? Wajerumani wanapaswa kuomba radhi kwa walichokifanya. Lakini nani mhusika hapa tz wa kuogansizi hilo?

    ReplyDelete
    Replies
    1. Nakubaliana na wewe Mdau mwenzangu. hatuto itendea haki historia ya nchi yetu vilivyo

      ikiwa kina Mzee Mtenvu, Mzee Takadiri, Mzee Sykes, Mzee Mwinyimvua , Mzee Maragande, Mzee Mlapakolo, Mzee Mapalala, Mzee Iboni, Paulo Bomani, Rashidi Kawawa, Mzee Komanya na sisi tuliobaki mwisho wa Umuri,
      na wengine wengi ambao tunawasahau.

      Inshallah tuombeane mungu tuiandike historia yetu vizuri na wajuku na vitukuu vyetu waisome na kuijua ili iwajenge
      UZALENDO WA NCHI KTK MIOYO YAO.

      LONG LIVE TANZANIA

      Delete

Top Post Ad

Below Post Ad