ISIS Watumia ‘Lockdown’ Kujiunda Tena, Wapanga Mashambulizi Nchi Hizi
0
July 25, 2020
Umoja wa Mataifa umeonya kuwa kundi la kigaidi la ISIS limepanga kufanya mashambulizi katika nchi za Magharibi, baada ya kujiunda upya katika kipindi cha amri ya watu kukaa ndani kuepuka maambukizi ya virusi vya corona.
Imeeleza kuwa kundi hilo la kigaidi linaamini kuwa virusi vipya vya corona (covid-19) vimepunguza nguvu za adui zao.
Ripoti iliyowasilishwa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imeeleza, “ISIS imepata nafasi ya kujiunda upya katika kipindi cha ‘lockdown’, na kama itakitumia vizuri kipindi hiki kwa lengo la kuajiri wapiganaji wapya na kutoa mafunzo, inawezekana maeneo ambayo yameanza kuondoa zuio la lockdown yataanza kushuhudia mashambulizi kadhaa.”
Idadi ya mashambulizi ya ISIS nchini Iraq na Syria imeongezeka katika mwaka 2020, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwaka uliopita, kwa mujibu wa UN.
Hata hivyo, wataalam wa masuala ya kijeshi wameeleza kuwa zuio la kuwepo kwa mikusanyiko mikubwa limesababisha kundi hilo la kigaidi kukosa maeneo wanayolenga kushambulia.
Ripoti hiyo imeeleza pia faida na hasara ya kipindi cha virusi vya corona kwa kundi hilo la kigaidi.
“Makundi ya kigaidi nayatumia kipindi hiki kusambaza kwa kasi zaidi propaganda na kuchangisha fedha,”
“Wakati huohuo, mlipuko huu umesababisha zoezi la kuvuka mipaka kuwa gumu zaidi, na maeneo yanayolengwa zaidi na magaidi hasa yenye mikusanyiko imepungua sana.” Imeeleza Ripoti hiyo.
Oktoba 27, 2019, Rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza kuimaliza ISIS katika jiji la Baghdad, baada ya jeshi la Marekani kumuua kiongozi wa kundi hilo, Abu Bakr al Baghdadi.
Tags