JENIFER Kanumba siyo jina geni kwenye masikio ya mashabiki wa Bongo Movies.
Jina lake halisi ni Hanifa Daudi. Ni kipaji kikubwa kilichovumbuliwa na aliyekuwa kinara wa Bongo Movies, marehemu Steven Kanumba aliyetangulia mbele ya haki Aprili 7, 2012.
Akiwa na Kanumba, Jenifer alicheza sinema kama This Is It ambayo ilimtambulisha rasmi na kumuweka kwenye ramani ya Bongo Movies.
Jenifer alipasua anga na filamu nyingine kama Uncle JJ, After Death, Without Daddy, Zena na Betina. Kwa sasa anafanya poa kwenye Tamthiliya ya Huba kwenye Maisha Magic ya DSTV.
Gazeti la IJUMAA WIKIENDA, limekaa meza moja na Jenifer ambapo anafunguka mengi ikiwemo ishu ya kulipa fadhila kupitia mama mzazi wa Kanumba, Flora Mtegoa ‘Mama Kanumba’ kwa mchango wa mwanaye katika kufichua kipaji chake;
IJUMAA WIKIENDA: Kuna kipindi wewe na mwigizaji mwenzako, Othman Njaidi ‘Patrick’ mlikuwa kimya kwenye sanaa, kulikoni?
JENIFER: Tulikuwa bize na masomo na si kingine.
IJUMAA WIKIENDA: Je, kwa sasa unagawa vipi muda wa masomo na sanaa?
JENIFER: Kwa sasa nipo chuo, hivyo muda ni mwingi. Zamani nilikuwa boarding school na hata niliporudi likizo, muda ulikuwa ni mfupi mno, hivyo ilikuwa ngumu kufanya sanaa.
IJUMAA WIKIENDA: Umecheza kwenye Tamthiliya ya Huba, je, kuna projekti nyingine mashabiki waitarajie?
JENIFER: Projekti zipo nyingi zinakuja, mashabiki wangu wasubiri tu.
IJUMAA WIKIENDA: Kwa upande wako unaona tofauti gani kati ya sanaa ya sasa na kipindi ukiwa na Kanumba?
JENIFER: Sioni tofauti sana, labda kwa sababu zamani nilikuwa mdogo. Na sasa mfumo umebadilika, siyo kama zamani watu walikuwa wakitumia CD.
IJUMAA WIKIENDA: Kwa upande wako unamzungumziaje Kanumba?
JENIFER: Kanumba alikuwa wa kipekee kwenye maisha yetu, ni zaidi ya baba, sitaweza kumsahau.
IJUMAA WIKIENDA: Ni maneno gani alikuwa akikuambia ambayo mpaka sasa unayaishi?
JENIFER: Alikuwa akinisisitiza nisome sana. Pia alikuwa anataka nije kuwa msanii mkubwa na mimi nayaenzi yote hayo.
IJUMAA WIKIENDA: Je, mama Kanumba ana mchango gani kwenye kazi zako?
JENIFER: Yule ni bibi yetu, ni mzazi wetu na ana mchango mkubwa sana kwa sasa, kwani amekuwa mwanafamilia. Anatusapoti hata kwenye kazi zetu.
IJUMAA WIKIENDA: Ulishawahi kuwaza kulipa fadhila kwa Kanumba kupitia mama yake?
JENIFER: Ndiyo, tena sana tu, vipo vitu vingi japo nilishawahi kufanya vidogo. Ila muda bado upo, nawaza kufanya vikubwa.
IJUMAA WIKIENDA: Ni msanii gani wa kiume unadhani anafika levo za Kanumba?
JENIFER: Mimi namuona Patrick.
IJUMAA WIKIENDA: Kwa nini Patrick na si msanii mkongwe?
JENIFER: Naona ana mwelekeo huo wa kufanana na Kanumba kwenye sanaa.
IJUMAA WIKIENDA: Umeonekana kuwa karibu na Gabo, je, kuna kazi inakuja?
JENIFER: Ukaribu wetu na Gabo ni mjomba kama ilivyokuwa kwa Kanumba, maana siyo mimi tu, hata Patrick na kazi zikiwepo zitaonekana tu.
IJUMAA WIKIENDA: Je, Gabo ana mchango gani kwenye kuendeleza kazi zenu?
JENIFER: Hatuko naye karibu sana kama ilivyokuwa kwa Kanumba, mara nyingi tunakutana kwenye kazi na vikao.
IJUMAA WIKIENDA: Mipango yako kwenye kazi za kimataifa iko vipi?
JENIFER: Kama ikitokea nitafanya. Ni kumuomba Mungu tu.
IJUMAA WIKIENDA: Je, uko chini ya menejimenti?
JENIFER: Hapana, siko kwenye menejimenti.
IJUMAA WIKIENDA: Uhusiano wako na wasanii wengine ukoje?
JENIFER: Sina mazoea sana, mara nyingi tunakutana kwenye kazi tu.
IJUMAA WIKIENDA: Ni changamoto gani unapitia kwenye kazi zako?
JENIFER: Ni za kawaida ambazo zinaepukika.
IJUMAA WIKIENDA: Kwa upande wako unafanyaje ili jina lako lisipotee?
JENIFER: Kawaida tu kwa kuhakikisha nafanya vizuri kwenye sanaa yangu.
IJUMAA WIKIENDA: Wewe ni mrembo, je, unakutana na vishawishi gani na unajilindaje?
JENIFER: Hakuna usumbufu ninaokutana nao, ni kawaida tu na wananiona ni mdogo.
IJUMAA WIKIENDA: Je, uko kwenye uhusiano?
JENIFER: Hapana, sina uhusiano.
IJUMAA WIKIENDA: Skendo zako na Patrick zilisambaa sana, je, huoni kama ni mbaya kwa kazi zako?
JENIFER: Hakuna kitu kama hicho, watu wanaongea tu. Patrick ni kaka yangu.
IJUMAA WIKIENDA: Je, kwa upande wa Dullvan, uhusiano wenu ukoje?
JENIFER: Wote hao ni kaka zangu, uhusiano wetu ni kama ndugu na wananipenda kama mdogo wao.
IJUMAA WIKIENDA: Umejipatia umaarufu ukiwa na umri mdogo, je, kwa upande wa wazazi wanachukuliaje vitu vya mitandaoni vinavyokuandama?
JENIFER: Mimi nikiwa nafanya kitu chochote, naangalia wazazi watachukuliaje. Sijawahi kufanya kitu mpaka wazazi wangu washtuke.
IJUMAA WIKIENDA: Mbali na kazi ya sanaa, una malengo gani?
JENIFER: Mipango yangu ni mingi, namuomba Mungu ikae sawa.
IJUMAA WIKIENDA: Unajivunia mafanikio gani kupitia sanaa yako?
JENIFER: Mafanikio ni mengi ikiwemo kujulikana, maana hicho ni kitu kikubwa kwangu.
IJUMAA WIKIENDA: Unawashauri nini mabinti wenye rika kama lako na wanatamani kuingia kwenye sanaa?
JENIFER: Sanaa ipo na itaendelea kuwepo, kama wana vipaji wavitumie ili kufikia malengo yao.