RAIS John Magufuli amemwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro kuwaondoa kazini mara moja Mkuu wa Polisi Wilaya ya Meru, Afisa Usalama wa Wilaya hiyo na viongozi wengine wa usalama wanaohusika kukumbatia tatizo la bangi wilayani humo.
Magufuli ametoa maagizo hayo leo Jumatatu, Julai 6, 2020 wakati akihutubia baada ya kuwaapisha wakuu wa mikoa na wilaya na viongozi mbalimbali ambao amewateua hivi karibuni huku akimpandisha cheo aliyekuwa Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini, James Kaji, na kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo kutokana na kile alichoeleza kuridhishwa na kazi nzuri anayoifanya.
“IGP nataka Mkuu wa Polisi wa Meru aondolewe, Afisa Usalama wa Meru aondoke. Maana hawakutimiza wajibu wao. OCCID wote watoke, ikiwezekana washushwe cheo maana hatuwezi kwenda kwenye utaratibu huo. Na wewe wa Kitengo cha Madawa (James Kaji) nakuthibitisha leo.
“Vyombo vya ulinzi na usalama navipongeza sana. Jana nilikuona wa madawa ukienda milimani kule. Kijiji kidogo kuna bangi, unapita kwenye mji unakuta magunia ya bangi. Hii inaonesha kuwa wanaonisimamisha kule hawafanyi kazi. Haiwezekani wewe utoke Dodoma ndiyo ukagundue hizo bangi huko milimani Meru, Arusha.
“IGP nataka Mkuu wa Polisi wa Meru aondolewe, na wewe wa madawa leo mimi nakuthibitisha umefanya kazi nzuri. Nataka mambo yaonekane….. Huyu Kamishna wa Madawa ya Kulevya siwezi nikamuapisha hapahapa? Tengenezeni kiapo haraka mkimaliza nimuapishe sitaki kurudi tena hapa.
“Niliowateua mnapaswa kuwashukuru hawa walioomba ruhusa nikawapa maana mmepata nafasi sababu wengine nimewapa ruhusa. Wengine mkasali wengine nao wazidi kuomba ruhusa mpate nafasi pia.
“Anayejisikia kuomba ruhusa aniombe tu. Nina viongozi wengine watatu nikitoka hapa nitaenda kuwapa ruhusa. Anayetaka kuomba ruhusa, hata Wakuu wa Mikoa anayetaka hata sasa aseme tu nitampa ruhusa. Nafahamu wanakoenda huko nako tutashirikiana vizuri.
“Leo tumemuapisha DC na DED wa Mvomero maana yake waliokuwepo kule wote wameondoka. Unawapa nafasi waka-solve matatizo. Wanaona hapatoshi wanataka waka-solve mahali pengine. Ukiwanyima umefanya dhambi mbaya. Kwa hiyo, nimewapa ruhusa.
“Maisha lazima yaendelee. Kazi za Watanzania lazima zifanywe, hatuwezi kusubiri watu tuliowapa ruhusa waende huko ikishindikana warudi tena, hapana lazima kazi ziendelee. Kwa hiyo, hata Mnyeti kama unataka ruhusa sema nikupe. Nilikuwa nauliza mbona wengine hawaombi.
“Huwa nasikitika sana unapopita kwenye Tarafa au Kijiji unakuta wananchi wanakulalamikia shida wakati kuna viongozi pale, hicho huwa kinanisikitisha sana.
“Mkoa wa Kigoma una maendeleo mengi, sasa hivi tunajenga barabara ya kwenda hadi Nyakanazi, Tabora na Katavi. Mkuu wa Mkoa (Thobias Andengenye) nenda kafanye kazi kazunguke na kafanye kazi. Kawatumikie wananchi.
“Ngoja nikwambie umefanya kazi nzuri (Sengati). Wapo waliokutisha wakijifanya wananifahamu sana kuwa wanakuja kukusemea kwa Rais. Ukawaambie tangulieni, mimi nachapa kazi hapa. Nikaona unaweza ndiyo maana tumekupa Tabora, kawatumikie wananchi.
“Nchi yetu hii ina changamoto nyingi sana na sisi tukizisimamia vizuri tutawasaidia Watanzania ambao sasa ni zaidi ya milioni 60. Nasikitika sana ninapokwenda sehemu wananchi wa pale wanakutolea masikitiko wakati viongozi uliowateua wapo pale.
“Kila mtu akaridhike na kile alichokipata. Hata mfano wa Yesu, pengine si mzuri hapa ila wale waliopewa talanta hawakupewa zinazolingana. Mkaridhike na nafasi zenu na kuwaongoza vizuri wananchi. RCs, DCs, RPCs na kila mmoja mnajitahidi kufanya kazi,” amesema Magufuli.