Kina Samatta Mikononi Mwa Man United Leo


MANCHESTER United inaweza ikachochea vita ya nafasi ya nne leo Alhamisi pale itakapoivaa timu inayopambania kubaki Ligi Kuu ya England ‘Premier’, Aston Villa pale Uwanja wa Villa Park.

Villa ambayo anacheza Mtanzania Mbwana Samatta, imekuwa na matokeo mabovu kwenye Premier na leo itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya United iliyo kwenye kasi yake chini ya kiungo, Bruno Fernandes.


Mara ya mwisho Villa inayonolewa na Kocha Dean Smith kupata ushindi Premier ilikuwa Januari 21, mwaka huu dhidi ya Watford, tangu hapo imekuwa ikipata vipigo au kuambulia sare.


Hii ni mechi ngumu kwa Villa ambayo inapambana kuhakikisha inabaki Premier kwani mpaka sasa iko nafasi ya tatu kutoka mwisho wakati United wako nafasi ya tano na wanapambania kucheza  Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

United itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kutopoteza mechi 16 mpaka sasa wakati Villa katika mechi sita zilizopita wametoa sare mbili na kuchapwa nne.Mechi iliyopita United waliwachapa Bournemouth mabao 5-2 na Villa walipigwa 2-0 na Liverpool.

Mchezo wa mwisho baina ya United na Villa ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2.Kama United watashinda leo basi watakuwa wamebakiza alama moja tu ya kutinga top four na Villa wakishinda basi watakuwa wamebakiza alama moja kutoka kwenye mstari mwekundu walipo sasa.


Katika mchezo wa leo, Villa wanaweza kuwakosa Wesley, Tom Heaton na Matt Targett lakini huyu anaweza kuwepo wikiendi hii dhidi ya Crystal Palace.

Kwa upande wa United, beki Victor Lindelof alicheza kwa kipindi kimoja wikiendi iliyopita dhidi ya Bournemouth lakini inaonekana hakuwa na tatizo kubwa hivyo anaweza kurejea tena leo kuungana na pacha wake, Harry Maguire eneo la kati.Axel Tuanzebe na Phil Jones pia hawatakuwepo kwenye mchezo wa leo kutokana na kutokuwa kwenye fomu.


Villa wamekuwa wakiangushwa na makosa kadhaa ikiwemo kushindwa kucheza mashambulizi ya kushtukiza, kulinda goli pindi wanapotangulia kufunga, kuzuia faulo jirani na lango na kutumia nafasi za kufunga.

United kwa sasa wako moto kwani wameshinda kwa wastani wa mabao matatu katika michezo mitatu iliyopita na ni wazuri kulinda bao pindi wanapotangulia kufunga.

BIRMINGHAM, England
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad