KATIKA historia ya muziki nchini, tuliona wanaume ndiyo waliamka na kuitengeneza tasnia hii katika nyanja mbalimbali.Wanamuziki wakali wa kiume waliibuka enzi hizo na kuikuza sanaa ya burudani kwa kutoa kazi kali katika uwanda wa Bongo Fleva, Hip Hop na nyingine nyingi.Baada ya hapo wanawake nao wakaamka na kuanza kufanya maajabu, katika kujifua vipaji vyao.
Kama tunavyojua, wanawake wakiwezeshwa wanaweza, kauli hii ikawafanya wajitume sana katika kazi zao na kuipiga teke kauli ya kwamba muziki ni wa wanaume tu.Miaka ya 2000, kuna baadhi ya wasanii wa kike waliitangaza vilivyo tasnia ya muziki hapa Bongo kwa kutoa kazi kali na kuzitangaza kimataifa zaidi.
Mbali na vipaji vyao, pia majina yao yalikua kwa kasi sana na kuweza kupenya kila kona ya Afrika Mashariki na kujizolea mashabiki lukuki.
Lakini baadaye, kuna kirusi kikaingia ndani yao na kuwatafuna vilivyo, kiasi kwamba kuwayumbisha katika muziki wao ambao walikuwa tayari wameshatoboa.Kirusi chenyewe si kingine, bali ni mapenzi. Mapenzi yanatajwa kuwa ni kirusi hatari kinachowamaliza wanamuziki wa kike hapa Bongo katika kazi zao.
Msemo wa kwamba huwezi kutumikia mabwana wawili au mafahari wawili hawakai zizi moja, unathibitisha kabisa hiki ninachokisema.Makala haya yanakuletea orodha ya wanamuziki wa kike walioyumbishwa na kirusi hiki;JIDEKomando mwenyewe na mkongwe kwenye Bongo Fleva, Judith Wambura ‘Jide’.
Ni mwanamuziki wa kike ambaye alitikisa mno miaka ya 2000, kwa kuwika ndani na nje ya Tanzania.Jide alifanya poa sana kwa kutoa album kama Machozi mwaka 2000, Binti mwaka 2003, Moto mwaka 2005, Shukrani mwaka 2007, The Best of Lady Jaydee ya mwaka 2012, Nothing But The Truth ya mwaka 2013 na Woman ya mwaka 2017.
Licha ya kufanya poa kiasi hicho na kimataifa zaidi, kipo kilichokuja kumkwamisha na kuwa ‘slow’ tofauti na mwanzo.Baada ya kuanza migogoro ya kifamilia na aliyekuwa mumewe; mtangazaji maarufu Gardner Habash, ambaye walidumu kwenye ndoa kwa muda mrefu na baadaye kuachana.
RAY C
Rehema Chalamila ‘Ray C’ na wengine humuita Kiuno Bila Mfupa. Yeye pamoja na Jide, walikuwa ni mfano wa kuigwa na wasanii wanaochipukia.Ray C alipeperusha vizuri bendera ya Bongo Fleva na vibao kama Mapenzi Yangu, Uko Wapi, Sogea Sogea, ngoma zote zikiwa ndani ya album ya Mapenzi Yangu mwaka 2003, Na Wewe Milele mwaka 2004, Sogea Sogea mwaka 2006 na Touch Me mwaka 2008.
Alifanya poa na kufika kimataifa zaidi, baadaye akaja kuyumba kwa kutopea kwenye matumizi ya dawa za kulevya.Akarudi kundini baada ya kupata matibabu na kuachia Ngoma ya Unanimaliza, akazamia ughaibuni baada ya kupata mchumba ambaye ni Raia wa Uingereza.
NAKAAYA
Kwa wapenzi wa muziki, watakua wanakumbuka ngoma ya Mr Politician kutoka kwa mwanamama Nakaaya Sumari.Ni dada wa aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 2005, Nancy Sumari. Mwaka 2008 Nakaaya alitikisa na ngoma yake ya Malaika, japo ujio wa Mr Politician ulifanya poa sana na kumpatia Tuzo ya Mwanamuziki Bora wa Kike mwaka huo.
Aliendelea kufanya poa na ngoma ya Ni Wewe kisha baadaye akatulia baada ya kuingia kwenye majukumu ya ndoa na kulea.
K-LYNN
Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi almaarufu kama K-Lynn, aliwahi kuwa Miss Tanzania mwaka 2000.Aliamua kujiingiza kwenye muziki na kufanya vizuri na Ngoma ya Nalia kwa Furaha akiwa na mwanamuziki Maxmilian Ruta ‘Bushoke’.
Ngoma hiyo ilifanya poa na kutengeneza album iliyokwenda kwa jina la Nalia kwa Furaha na baada ya miaka mitatu akaachia album iliyokwenda kwa jina la Crazy Over You.Baada ya kuingia kwenye ndoa na aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, marehemu Dk Reginald Mengi, K-Lynn akapotea kwenye muziki mpaka sasa
MAUNDA ZORRO
Hiki ni Kipaji kikali kutoka katika familia ya muziki. Maunda Zorro, pia ni dada wa mwanamuziki mkubwa hapa Bongo, Banana Zorro.Maunda ni kati ya wasanii wa kike waliotikisa miaka ya 2000, kwani Ngoma ya Mapenzi ya Wawili, ilimuweka vyema kwenye ramani.
Aliendelea kufanya poa na ngoma kama Niwe Wako, Daladala na Nafurahi, lakini baada ya muda akapotea na kutumikia majukumu ya ndoa na malezi.
RUBY
Hellen George ‘Ruby’ ni kipaji kingine kilichopita kwenye mikono ya marehemu Ruge Mutahaba ndani ya Nyumba ya Vipaji (THT). Ruby amefanya poa na ngoma kama Na Yule, Forever, Alele, Kelele, Ntade na nyingine, ila baada ya kuingia katika uzazi na kupitia changamoto za kiuhusiano, mwanadada huyu ameyumba.
VANESSA
Vanessa Hau Mdee ‘V-Money’ hivi karibuni ametangaza kuacha muziki.Aliwika na ngoma kama Never Ever, Come Over, Siri, Niroge, Hamjui na nyingine kibao.Inasemekana sababu kubwa ya kuacha muziki ni mapenzi. Hii ni baada ya kuanzisha uhusiano na mwanamuziki mwenye asili ya Nigeria, Olurotimi Akinosho ‘Rotimi’ na kwa sasa wanaishi wote mjini Atlanta, Marekani.
Japo yeye anakiri kuyumbishwa na msongo wa mawazo (depression), lakini suala la mapenzi linadaiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa.Wengine ni Mwanahawa Abdul ‘Queen Darleen’ ambaye ameolewa hivi karibuni, Estelinah Sanga ‘Linah’, Dayna Nyange na wengine kibao.U
SHAURI
Wanamuziki wa kike wasilalamike kuwa wako nyuma kwenye muziki, badala wao wenyewe wanatakiwa kujiongeza kama wanamuziki wakubwa duniani wenye familia zao, lakini bado wanakomaa kwenye muziki na kufanya vizuri.