BENCHI la Ufundi na Bodi ya Wakurugenzi wa Simba kwa pamoja wamekubaliana kumbakisha kiungo wake mkabaji raia wa Brazil, Gerson Fraga.
Kiungo huyo ni kati ya wachezaji waliokuwa wakihusishwa kuachwa Simba katika kuelekea msimu ujao akiwemo na Mbrazili mwenzake, Tairone Santos ambao walijiunga pamoja mwanzoni mwa msimu huu.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, kiungo huyo hataachwa kama ilivyokuwa imepangwa na badala yake ataendelea kukipiga tena kwenye msimu ujao.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kiungo huyo amebakishwa baada ya kuona kiwango kikibadilika kila siku kadiri anavyoendelea kucheza mechi ikiwemo na watani wao wa jadi, Yanga ambayo Mbrazili huyo alifunga bao.
Aliongeza kuwa wakati kiungo akibakishwa, mwenzake Tairone yeye ataachwa kwenye usajili wa msimu ujao kwa kuusitisha mkataba wake wa miaka miwili aliousaini.
“Fraga kadiri siku zinavyokwenda anaonekana kuzidi kubadilika kwa kuonyesha kiwango kikubwa, mfano mzuri mchezo wetu na Yanga alicheza kwa kiwango kikubwa ambacho kiliwashtua viongozi.
“Hivyo, basi kutokana na kiwango hicho alichokionyesha wamekubaliana viongozi na benchi ka ufundi kuendelea naye katika msimu ujao,” alisema mtoa taarifa huyo.Alipotafutwa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Senzo Mazingisa kuzungumzia hilo alisema kuwa: “Muda wa usajili bado, hivyo wachezaji wapya tutakaowasajili na tutakaowaacha tutatangaza mara baada ya ligi kumalizika.”