Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Tundu Lissu amesema kuwa wiki ijayo siku ya Julai 27, 2020, atakanyaga rasmi ardhi na udongo wa Tanzania akitokea nchini Ubelgiji alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana mwaka 2017.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Julai 21, 2020, wakati akizungumza mubashara kupitia channel ya Youtube ya chama hicho na kueleza kuwa licha ya kwamba ameamua kurudi nchini lakini bado yuko kwenye hatari zaidi kwa kuwa wale waliomshambulia na kumjeruhi bado hawajulikana hivyo anayo imani kwamba bado wapo.
"Baada ya miaka karibu mitatu ya matibabu, wakati wa mimi kurudi nyumbani umewadia, kwa mara ya kwanza tangu Septemba 7, 2017, nitakanyaga ardhi na udongo wa Tanzania siku ya Jumatatu, Julai 27, 2020, Mjini Dar es Salaam, majira ya saa 7:20 mchana na nitaingia na Ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia" amesema Tundu Lissu.