Kadhalika watu zaidi ya milioni nne wameachwa bila makazi kutokana na mafuriko hayo katika jimbo la Assam lililoko kaskazini mashariki mwa India, na kusini mwa nchi jirani ya Nepal.
Waziri wa Maji katika jimbo la Assam nchini India, Keshab Mahanta ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, watu milioni 2.7 katika eneo hilo wamepoteza makazi yao baada ya jimbo hilo kushuhudia mawimbi matatu ya mafuriko tangu mwishoni mwa Mei hadi sasa.
Aidha watu zaidi ya 80 wamepoteza maisha baada ya kusombwa na mafuriko hayo, huku makumi ya wengine wakitoweka.
Katika nchi jirani ya Nepal, watu zaidi ya 110 wameaga dunia kutokana na mafuriko na maporoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa za masika zinazoendelea kunyesha katika maeneo ya kusini mwa nchi.
Afisa wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nepal, Murari Wasti amesema yumkini idadi hiyo ya vifo ikaongezeka kwa kuwa watu 48 hawajulikani waliko baada ya kujiri majanga hayo ya kimaumbile.
Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya serikali ya China kutangaza kuwa watu takriban 140 wameaga dunia baada ya nchi hiyo kuathiriwa na mafuriko mabaya zaidi kuwahi kuikumba China katika kipindi cha zaidi ya miaka 30 nchini humo.