Jaji nchini Kenya ameamuru kiasi cha dola za kimarekani milioni 12 zilipwe kwa jamii iliyoathirika na sumu itokanayo na madini ya risaisi (lead) kutoka kwenye Betri ya vinu vya uchakataji.
Uamuzi huo ni matokeo ya kazi iliyofanywa na Phyllis Omido, mkazi wa maeneo duni ya Owino Uhuru, ambayo yako pwani ya nchi hiyo, Mombasa.
Akiwa muajiriwa kwenye vinu hiyo, alishawishika kuchukua hatua hiyo baada ya mtoto wake kubainika kuwa aliathirika na sumu itokanayo na madini ya risasi.
Kijana wake mdogo aliugua sana baada ya yeye kufanya kazi katika vinu hivyo kwa miezi mitatu.
Baada ya vipimo, madaktari waligundua kuwa alikuwa na sumu mwilini ambayo ilimpata kwa njia ya kunyonyeshwa na mama yake.
Alibaini kuwa watu wa jamii ile walikuwa na matatizo hayo hayo hatimaye aliweza kufanikiwa katika mpango wa kuvifunga vinu hivyo mwaka 2014.
Lakini Bi Omido alikwenda mahakamani mwaka 2016 kwa ajili ya kuitaka serikali ilisafishe eneo hili na kulipa fidia kwa familia za wale waliopoteza maisha au kuugua kutokana na athari za madini hayo.
Mbali na fedha, Jaji Ann Omollo ameziamuru mamlaka kuondoa madini ya risasi yaliyosalia, gazeti la Daily Nation la Kenya limeripoti.