Wizara ya sheria Marekani imesema kwamba aliyekuwa rais wa Gambia Yahya Jammeh alitumia pesa alizopata kwa njia ya ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma kununua jumba la kifahari huko viungani mwa Washington alipokuwa madarakani.
Kulingana na nyaraka zilizowasilishwa kama sehemu ya juhudi za kutwaa jengo hilo katika mji mkuu wa Marekani, Bwana Jammeh alinunua jumba hilo lenye thamani ya dola milioni 3.5 za Marekani sawa na (£2.8m) miaka 10 iliyopita.
Inasemekana kwamba alinunua jumba hilo kupitia mke wake Zineb Jammeh.
Bwana Jammeh alitoroka nchi baada ya kushindwa kwenye uchaguzi wa 2017 na sasa hivi anaishi nchini Equatorial Guinea.
Yahya Jammeh ni nani?
Alizaliwa Mei 1965
Aliingia madarakani baada ya mapinduzi mwaka 1994
2013, aliapa kuendelea kusalia madarakani ”miaka bilioni” iwapo Mungu atampa Umri
Pia aliagiza hukumu ya kifo dhidi ya wahalifu na wapinzani wake wa kisiasa
Mwaka 2007, aliahidi kwamba anaweza kutibu ukimwi na ugumba kwa kutumia dawa za mitishamba.
2008, alionya kwamba wapenzi wa jinsia moja watahukumiwa kifo
Pia alikanusha kwamba majajusi wake wa usalama walimuua Deyda Hydara, 2004
Yahya Jammeh
Yahya Jammeh alikataa kuondoka madarakani baada ya kushindwa kwenye uchaguzi mkuu na rais wa sasa Adama Barrow.
Bw Jammeh mwanzoni alikubali alikubali kushindwa lakini baadaye akapinga matokeo hayo.
Mbona Jammeh alikataa kuondoka madarakani?
Bw Jammeh awali alikubali kwamba Bw Barrow alishinda uchaguzi lakini baadaye akabadili msimamo wake na kusema hangeachia madaraka.
Alitangaza hali ya tahadhari ya siku 90 na kuhimiza “amani, utulivu na kufuatwa kwa sheria” baada ya kile alichosema ni udanganyifu uchaguzini.
Alisema tume ya uchaguzi ilifanya makosa mengi, na baadhi ya wafuasi wake walizuiwa kupiga kura vituoni.
Tume hiyo baadaye ilikubali kwamba baadhi ya matokeo yaliyotangazwa yalikuwa na makosa, lakini ikasema makosa hayo hayangeathiri ushindi wa Bw Barrow.
Bw Jammeh amesema atasalia madarakani hadi uchaguzi mpya ufanyike.
Hatua yake ya kuendelea kung’ang’ania madaraka itahakikisha kwamba hashtakiwi kutokana na makosa aliyoyatenda wakati wa utawala wake.
Yaya Jammeh akiwapungia mkono watu alipokuwa akiabiri ndege Banjul
Yaya Jammeh akiwapungia mkono watu alipokuwa akiabiri ndege Banjul
Ecowas, Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, iliipa Senegal jukumu la kuhakikisha Bwana Jammeh anaondoka madarakani kwa sababu taifa hilo linaizunguka Gambia.
Kanali Abdou Ndiaye, msemaji wa jeshi la Senegal, amesema Ecowas iliamua kumuwekea Jammeh makataa ili kujaribu kupata suluhu ya kidiplomasia.
Wakati huo, hofu ya kisiasa ilikuwa imetanda nchini humo kiasi cha raia wake wengi kutorokea nchi jirani wakihofia kuzuka kwa maigano.
Mataifa ya Afrika Magharibi yaliwatuma wanajeshi Gambia na kutishia kumuondoa Jammeh madarakani kwa nguvu.
Hata hivyo, Gambia Yahya Jammeh aliyeiongoza Gambia kwa miaka 22 alikubali kung’atuka na kuondoka nchini humo baada ya kwamba rais Adama Barrow ameapishwa.
Adama Barrow alitangaza kupitia ukurasa wake wa Twitter, baada ya mazungumzo ya saa kadha yaliyonuiwa kumshawishi Bw Jammeh kukubali matokeo ya uchaguzi.
Siku moja baada ya kuachia madaraka kwa Adama Barrow, Yahya Jammeh aliwasili nchini Equatorial Guinea.