RAIS John Magufuli amesema saa chache kabla ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, kuaga dunia, alizungumza naye kwa njia ya simu akamtoa hofu na kumhakikishia kuwa anaendelea vizuri.
Magufuli amesema hayo leo, Julai 28, 2020 wakati akihutubia waombolezaji na Watanzania wote katika Uwanja wa Uhuru kwenye zoezi la kuaga kitaifa mwili wa Mkapa kabla ya kupelekwa nyumbani kwao Lupaso, Masasi, mkoani Mtwara ambako anatarajiwa kuzikwa kesho.
“Binafsi niliongea na Mzee Mkapa kwa simu saa chache kabla hajafariki, nakumbuka aliniambia “John usiwe na wasiwasi naendelea vizuri”. Sikujua yale maneno yalikuwa ya kuniaga, namshukuru Mungu kwa zawadi ya Mzee Mkapa ya kuwa naye pamoja.
“Mzee Mkapa alikuwa na sifa ya kulea vipaji vya uongozi na kuvikuza, yeye ndiye aliniibua mimi lakini kama mtakavyokumbuka alimchagua mzee Kikwete kuwa Waziri wa Mambo ya Nje miaka kumi ambaye baadaye alikuja kurithi kiti chake cha urais.
“Mzee Mkapa ni shujaa wangu, hata nilipopatwa na shida Mzee Mkapa hakuniacha kamwe, hakutaka nianguke, alinilea kama mtoto wake, saa nyingine machozi yanakuja lakini hata Kikwete nilimuona siku ile analia kwa hiyo msinishangaeshangae.
“Watanzania wanamkumbuka Mzee Mkapa kwa mageuzi ya uchumi, wakati anaingia madarakani nchi yetu ilikuwa na matatizo ya kiuchumi, na wakati huo alianza kulipa madeni na kuanza kuzishawishi taasisi za kifedha pamoja na nchi wahisani kufuta madeni yake.
“Mzee Mkapa amefariki dunia ikiwa imepita miezi nane tu tangu azindue kitabu chake cha My life, My purpose tarehe 12 Novemba 2019, ambapo ndani ya kitabu hicho ameeleza kwa kirefu sana historia ya maisha yake.
“Julai 23, taifa letu lilipatwa na pigo kubwa la kuondokewa na aliyekuwa rais wetu wa awamu wa tatu, kifo chake kimeacha majonzi na simanzi kubwa, siyo kwa familia yake na nchi yetu lakini katika eneo letu la Afrika Mashariki na dunia kiujumla.
“Alikuwa jasiri, shupavu, mzalendo, mcha Mungu, mwenye msimamo usioyumbishwa na mpenda amani ni baba wa demokrasia,” amesema Magufuli.