Takriban watu sita wameripotiwa kufariki baada ya bomu kulipuka katika mgahawa mmoja uliopo mji wa kusini wa Somalia wa Baidoa.
Watu wengine kadhaa wamejeruhiwa. Ndani ya mji mkuu wa Mogadishu maafisa wa polisi wanasema kwamba walimpiga risasi mlipuaji wa kujitoa muhanga alipokuwa akiendesha gari lake katika kituo kimoja cha kukagua magari nje ya Bandari ya Mogadishu.
Takiban watu saba walijeruhiwa katika shambulio hilo.
Kulingana na mwandishi wa BBC Somalia Rage Hassan wote waliofariki katika mgahawa walidaiwa kuwa raia waliokuwa wakila kifungua kinywa, wakati bomu hilo lilipolipuka.
Maafisa wa usalama wa Somalia walikuwepo katika eneo hilo lakini hawakujeruhiwa.
Katika shambulio hilo Polisi waliambia BBC kwamba mlipuaji huyo wa kujitolea muhanga aliekuwa akiendesha gari hilo alijaribu kushambulia kituo cha kukagua magari barabarani mbele ya bandari lakini maafisa wa polisi walifanikiwa kumpiga risasi na gari hilo likalipuka.
Maafisa wawili wa polisi na raia watano walijeruhiwa, Milipuko ya mabomu pamoja na mashambulizi ya kigaidi yamekuwa kitu cha kawaida mjini Mogadishu.
Hakuna mtu aliyedai kwamba alihusika na shambulio hilo, Lakini kundi linalohusiana na lile la al-Qaeda limekuwa likijaribu kuiangusha serikali inayoungwa mkono na Muungano wa Afrika na hivyobasi kutekeleza mashambulio kama hayo.