MAMBO yanazidi kuwa mabaya kati ya uongozi wa Yanga dhidi ya kiungo wao mshambulizi Bernard Morisson baada ya wanachama wa klabu hiyo maarufu kama Makomandoo kulazimika kutimua mbio wakidhani ameshika kisu.
Timbwili kubwa liliibuka kati ya Yanga na Makomandoo hao na Morrison ambaye alikuwa akitaka kuondoka kambini akisema atarejea baada ya muda mfupi.
Makomandoo hao walimzuia na kuanza kumsukuma kuhakikisha hatoki, jambo lililomkasirisha na kuamua kukimbilia eneo la jiko katika kambi ya Yanga kwenye Hoteli ya Regency, Mikocheni jijini Dar es Salaam.
“Ulikuwa mzozo wa kama dakika tano hivi usiku mnene, lakini Morrison alisukumwa sana mwisho akakasirika na kuchukua ule upawa wa kutolea chips, makomandoo wakakimbia wakidhani ni kisu,” kilieleza chanzo.
“Baada ya pale akaingia kwenye gari na kuondoka, baada ya muda kama nusu saa hivi akarudi akiwa na begi akaingia ndani. Nasikia wale Makomandoo waliondoka na kwenda Polisi, sasa sijajua kama wamefungua kesi,” kilisisitiza chanzo.
“Leo (jana) asubuhi nimesikia kocha amemuondoa hapa kambini, sasa sijajua kama ameondoka au vipi.”Juhudi za kumpata Morrison zilifanyika jana na Morrison akasema:“Walini sukuma sana wale watu, walikuwa sita. Nilipoona wanazidi kunisukuma, nikakimbia na kuchukua upawa. Nafikiri kutokana na kiza wao wakadhani ni kisu, wakakimbia.
“Nilipoona wamekimbia, nikaingia kwenye gari, nikaenda kuchukua kiatu lakini asubuhi kocha akaniambia natakiwa kuondoka kambini, basi nikaondoka na kurejea nyumbani,” alisema Morrison.Jana, Morrison hakuonekana uwanjani wakati Yanga ikiivaa Kagera Sugar katika mechi ya Kombe la Shirikisho kutokana na mgogoro huo.
Taarifa nyingine za uhakika zinaeleza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limemuita Morrison kwenda kuhojiwa kuhusiana na suala lake la mkataba.Taarifa zinaeleza Morrison atakwenda TFF kwa ajili ya mahojiano ingawa haijawekwa wazi kama atahojiwa kuhusiana na jambo lipi.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa timu hiyo, Hassani Bumbuli kuzungumzia hilo simu yake ya mkononi iliita bila ya mafanikio ya kupolewa. Aidha, alitafutwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela naye alisema kuwa; “Nipo kwenye semina ya La Liga, hivyo sipo katika nafasi nzuri ya kuzungumzia hilo.
”Jana jioni mara baada ya taarifa hizo kuzagaa, Yanga kupitia mitandao yake ya kijamii ilitoa tangazo la kutotumia picha za Mghana huyo katika matangazo yanayohusu klabu hiyo huku wakitangaza suala lake linaendelea kushughulikiwa na uongozi na hivi karibuni watatoa taarifa.
Tokea Morrison amesema ana mkataba wa miezi sita, uhusiano kati yake na uongozi wa Yanga umeyumba na tayari uongozi huo ulifafanua mkataba wake ni wa miaka miwili.
(Waandishi Wetu, Dar es Salaam)
OPEN IN BROWSER