Mahakama moja nchini Ufaransa jana ilimhukumu mpiganaji mmoja wa jihadi kwenda jela miaka 30 kwa uhalifu alioufanya Syria kati ya mwaka 2013 - 15 ikiwa ni pamoja na kutekeleza mauaji ya wafungwa wawili wakati akiwa mtu wa ngazi ya juu katika kundi la itikadi kali la Dola la Kiislamu.
Tyler Vilus, mwenye umri wa miaka 30, ambaye alipatikana na hatia kwa mashitaka yote, pia anashutumiwa kwa kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi, kuongoza kundi la wapiganaji wa Dola la Kiislamu pamoja na kufanya mauaji ya kinyama.
Mwendesha mashitaka wa serikali Guillaume Michelin hapo mapema aliiomba mahakama kumhukumu mtuhumiwa huyo kifungo cha maisha, bila kuwa na uwezekano wa kupata msamaha kwa miaka 22.
Michelin amesema Vilus hajabadilika hata kidogo tangu alipojiunga na kundi hilo la Dola la Kiislamu.