Msichana wa Miaka 12 Aokolewa Baada ya Kuozwa kwa Wanaume Wawili ndani ya Mwezi Mmoja


Msichana wa miaka 12 aokolewa baada ya kuozwa kwa wanaume wawili ndani ya mwezi mmoja
Bongo5 · Ally Juma · 2 hours ago
Msichana wa miaka 12 ameokolewa nchini Kenya na mamlaka baada ya kuozwa wanaume wawili katika kipindi cha mwezi mmoja.



Babake msichana huyo anayeishi katika kaunti ya Narok iliopo magharibi mwa mji mkuu wa Nairobi alimlazimisha kufunga ndoa na mwanamume mwenye umri wa miaka 51.

Alitoroka na baadaye kuozwa mwananume mwengine mwenye umri wa miaka 35 kabla ya kuokolewa na maafisa wa haki za watoto na maafisa wa serikali.

Nchini Kenya kufunga ndoa na mtu aliye chini ya umri wa miaka 18 ni uhalifu.


Mwanaharakati wa haki za watoto alisema kwamba alipashwa habari kuhusu msichana huyo wakati alipokuwa katika harakati za kumuokoa msichana mwengine.

Babake alimuoza kwa mzee huyo, hivyobasi hakuwa na chaguo bali kuolewa na kijana huyo, Joshua Kaputah kutoka kwa shirika la Muungano wa amani Narok aliambia BBC.

Bwana Kaputah aliongezea kwamba ufukara na kufungwa kwa shule kutokana na mlipuko wa virusi vya corona umesababisha ongezeko la visa vya ndoa za watoto.

”Baadhi ya familia zinakabiliwa na njaa na uwezekano wa kupokea ng’ombe mbili au tatu za mahari unawavutia wengi”, alisema.

Je suala la ndoa za watoto ni jambo la kawaida Kenya?
Kuwaoza wasichana wadogo ni suala linalozua hofu kubwa miongoni mwa jamii ya Maasai ambao wanaishi katika kaunti ya Narok, kulingana na mwandishi wa BBC Peter Mwai.

Anaongezea kwamba wasichana wa Maasai huonekana kama ‘utajiri’ na huozwa kwa mtu anayechaguliwa na baba baada ya kupewa ng’ombe kama mahari.

Serikali imekuwa ikikabiliana na utamaduni huo lakini unaendelea kusheheni kutokana na utekelezwaji duni wa sheria .

Je kuna yeyote aliyekamatwa?
Gazeti la The Standard nchini Kenya limeripoti kwamba mwanamume wa kwanza alilipa ng’ombe nne kama mahari, na kwamba msichana huyo alikataa kuolewa lakini alipigwa na binamu zake wa kiume.


”Nilitoroka na kwasababu sikuweza kurudi kwa baba yangu kwa hofu ya kukaripiwa , niliamua kuishi na mwanamume mwenye umri wa mika 35 ambaye alikuwa ameoa”, alinukuliwa akisema na gazeti la The Standard.

Bwana Kaputah alisema kwamba babake msichana huyo baadaye alimpata na kumrudisha kwa mwanamume mwenye umri wa miaka 51.

Wakati bwana Kaputah alipowasili na maafisa wa serikali, mtu huyo tayari alikuwa ametoroka.

Maafisa wa polisi wanamsaka baba yake na wanaume hao wawili ambao walikuwa wamemuoa msichana huyo ambao wamekwenda mafichoni, kulingana na vyombo vya habari.

Iwapo watapatikana na hatia huenda wakahukumiwa kifungo cha hadi miaka mitano ama kupigwa faini ya hadi $10,000.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad