Nilikuwa Nauza Mwili Wangu Nipate PESA Wakati nipo Kwenye Ndoa



Kila anapokumbuka alikotoka maishani, Purity Wanjiru hudondokwa na machozi asijue la kufanya.

Purity ambaye ni mama wa watoto wawili anasema hakuwahi kufikiria kwamba kuna wakati angeuza mwili wake.

Lakini ilikuwaje hadi akajipata katika maisha hayo?

Maisha ya utotoni
Purity anakumbuka kuwa maisha yake ya utotoni alikuwa mtukutu mno kiasi cha kutoweza kuketi sehemu moja kwa muda mrefu.

Kwahivyo hata akiwa shule ya msingi kila mara alikuwa anatoroka ili kwenda madukani kuzurura zurura tu.

Haikuchukua muda kwa wakuu wa shule ya msingi kufahamu tabia zake.

Na matokeo yake akafukuzwa shuleni akiwa darasa la 5 kwa kuwa walimu waliona ni vyema akae nyumbani kwa muda ajirekebishe.

Lakini cha kusikitisha ni kwamba badala ya kunyooka, alizidi kupotea. Purity alijihisi kutengwa na shule na jamii pia.

"Tumezaliwa tukiwa watoto 12 kwetu, mimi ndio kitinda mimba. Siku moja ndugu zangu wakubwa na mama yangu walishirikiana kunipa kichapo cha mbwa baada ya wao kugundua kwamba sikuwa nikienda shuleni," Purity anakumbuka.

''Kichapo hicho kilinifanya nijawe na hasira nikiwa na miaka 13, na nikarotoka nyumbani."

Hapo ndipo Purity alipoanza kuishi mitaani. Anasema kuwa wakati mmoja alikamatwa na polisi na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kurandaranda na pia kwa kuwa kahaba.

Alifungwa gerezani miezi miwili.
Purity anasema kipindi hicho na magumu aliopitia kulimfanya kuwa mkakamavu hata zaidi kuhimili anayokumbana nayo maishani akiwa peke yake.

Na baada ya kumaliza kifungo hicho, aliamua kutorudi nyumbani tena.

Jaribio lake la kuishi na mama mmoja aliyekubali kumpa mahali pa kujistiri liliambulia patupu kwani kulingana na Purity alifanyishwa kazi zote za nyumba hio.

Akaamua ni kheri kuishi mtaani kwenye uhuru kuliko utumwa wa nyumbani.

Na akiwa kwenye pilkapilka za maisha, Purity alikutana na mwanamume mmoja ambaye walianza uchumba.

Dhiki kwenye ndoa
Purity anakiri kuwa yeye na mpenzi wake walikuwa hawajakomaa kwasababu wote walikuwa vijana waliokuwa wanaanza kubaleghe.

Licha ya hayo walianza kuishi pamoja kama mume na mke. Hata hivyo, ndoa yao ilianza kwa panda shuka nyingi.

Kwanza alishika ujauzito haraka mno na pili yule mume wake alimgeuka na kuanza kumdhulumu na kumchapa kila wakati bila sababu zozote.

Purity anakumbuka: "Huyo aliyekuwa mume wangu alikuwa anakunywa pombe na kutafuna miraa, hakuwa anaacha chochote nyumbani."

''Alikuwa ananitusi mno na kuniambia kuwa yeye hana nia ya kunioa wala hanipendi. Alikiri kuwa alichohitaji kwangu ni kunitumia tu".

Matamshi hayo yaliyozidi kumkera Purity wakati huo akiwa na ujauzito wa miezi 6.



Wasichana waliokuwa marafiki zake walianza kumshauri kuhusu njia mbadala ya kutafuta pesa na chakula.

Hapo ndipo alipofundishwa kuhusu ukahaba.

Purity alianza kuuza mwili wake kwa wanaume waliokuwa tayari kushiriki ngono na mwanamke mjamzito.

Purity anasema kuwa ni kazi alioifanya hadi alipojifungua mtoto msichana.

Wakati huo mume wake alikuwa anafahamu fika kazi ya ukahaba anayoifanya, lakini kulingana na Purity mume alikuwa hamjali kabisa.

Kulingana na Puritiy, mume wake akirejea nyumbani, alichotaka kuona ni chakula tu lakini mahitaji ya Purity aliweka wazi kwamba hiyo sio shida yake.

"Cha kushangaza zaidi ni kuwa wakati ninafanya kazi ya ukahaba, baba ya watoto wangu ndiye aliyekuwa anatunza watoto usiku, huku mimi nikitoka kufanya ukahaba," Purity anaeleza.

'Ninaporejea asubuhi alikuwa ananiuliza kazi ilikuwa vipi, na ni pesa ngapi nilizopata usiku huo."

Purity anasema yeye binafsi hakupenda maisha ya ukahaba hata kidogo, kwasababu kila wakati alikuwa anajihisi mchafu na mwanamke ambaye ni wa kutumiwa tu kimwili.

Purity anakumbukumbu mwanamume mmoja ambaye alimchukua usiku mmoja, akiwa na ujauzito wa mtoto wa pili, ila Purity hakumueleza mteja wake kuhusu hali yake.

Akiwa kwenye gari yule mwanamume aligundua ujauzito wa Purity.

"Aliponipapasa tumbo na kufahamu hali yangu, aliniuliza mbona ninajiuza kimwili ilhali nina mimba," Purity anasema.

''Unajua kuwa nimemuacha mke wangu mjamzito kwa kuwa kila nikitaka kushiriki naye amekuwa akiniambia amechoka, kwani wewe huchoki?" mteja alimuuliza Purity.

Purity alimjibu kuwa yeye hawezi kuchoka kwasababu anatafuta hela za kumuwezesha kukidhi mahitaji yake.

Purity anakumbuka kuwa yule mwanamume alikataa kushiriki naye ngono na badala yake akampa fedha dola 100 na kumshauri arejee kwake nyumbani kwa kuwa hakustahili kufanya kazi kama hiyo.

Hapo ndipo Purity alipoanza kuyafikiria tena maisha yake na kushangaa ni kwanini mume wake hakuwa na tatiizo anapotoka kwenda kuuza mwili wake ilhali baadhi ya wanaume waliona ni kazi asiyostahili kufanya.

Haikuchukua muda, Purity akaamua kuachana na ndoa hiyo. Yeye na mumewe wakatengana na Purity akaanza maisha mapya na watoto wake wawili ila kazi alioendelea kuitegemea maishani ni hiyo hiyo ya ukahaba.

Kituko makaburini
Purity anakiri kuwa kazi ya ukahaba ni hatari mno, kwani mwanamke kahaba hajui nia ya mwanamume ambaye anamchukua.

Anasema kwamba maisha ya mwanamke kahaba huwa yumo mikononi mwa 'mteja'.

Hii ina maana kuwa mwanamume anaweza kumdhulumu atakavyo kwasababu huduma anayopaya anailipia.

Anakumbuka wakati mmoja kuna mwanamume alimchkukua usiku wa manane na kumuahidi fedha nyingi zaidi ya dola mia mmoja na kumi na tano.

Hata hivyo, mteja huyo aliomba kuwa waende hadi kwake nyumbani kwa kuwa hakupendelea kuwa kwenye chumba cha kulala.

Purity aliridhia kutokana na fedha alizokuwa analipwa kama walivyokubaliana.

"Tulianza safari na moja kwa moja akaanza kuelekea eneo maarufu la makaburi ya Langata mjini Nairobi. Aliliendesha gari lake ndani kabisa ya makaburi hayo huku akifoka na kunitusi matusi mabaya, makubwa makubwa. Wakati huo pia akawa ananitishia kunitoa uhai wangu huku ananipiga kichapo cha mbwa. Aliniamrisha kuvua nguo zangu zote na ghafla akaondoka na kuniacha katikati ya makaburi".

''Nilipigwa na butwaa nisijue la kufanya, Purity anasema.

Kilichotokea ni kwamba

Kwa kuwa amesikia simulizi nyingi kuhusu maajabu ya makaburini alianza, kukata mbio huku akiwa uchi wa mnyama asijue la kufanya.

Alipofika barabrani walinzi walipomuona nao wakaanza kukata mbio. Mmoja wao aliangusha shuka la kimaasai alilokuwa amejifunika akiwa mbioni, na hapo Purity akaanza kuona neema ya Mungu imemshukia ghafla.

Aliokota shuka lake taratibu huku akimshukuru maulana na miujiza yake na kujistiri.

Kuacha ukahaba
Tukio hilo ni moja ya yaliyomfanya Purity atake sana kuachana na ukahaba kwa kuwa maisha yake yaliendelea kuwa hatarini.

Kupata fedha katika njia ambayo jamii inaiona kuwa chafu kulimfanya kukosa usingizi na vile vile alihisi ikiwa watoto wake watakuja kujua kile anachofanya kupata pesa basi ingekuwa aibu.

Purity anakiri kwamba ukahaba ni moja wapo ya sababu ambazo huchangia ndoa nyingi kuvunjika.

Na pia kwa kipindi kirefu, alihisi yeye kama kahaba amechangia kuvunjika kwa ndoa nyingi hasa kwa wanaume walioko wanakuja kutafuta huduma kwake.

Purity anasema usiku mmoja walipokuwa kazini walikamatwa na polisi na kupelekwa kituoni na kulipokucha akajitazama jinsi alivyokuwa amevaa, binafsi aliona aibu na kuanzia hapo akatamani kubadilika na siku hiyo hiyo alipotoka polisi, akajikuta kanisani alipopata ukombozi pamoja na kupokea msaada mkubwa kutoka kwa wanawake ambao walimshauri na kumsaidia kuachana na ukahaba.

Purity anasema kuwa maisha ya ukahaba yanamdunisha mwanamke na kumfanya akose ukakamavu na hata sauti katika jamii kwasababu ni kazi ambayo ni kinyume na maadili ya jamii.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad