Niyonzima Ashusha Presha Yanga SC


AKIUKOSA mchezo wa jana Jumatano wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar, kiungo mchezeshaji fundi wa Yanga raia wa Rwanda, Haruna Niyonzima, ameibuka na kutamka kuwa mashabiki waondoe hofu kwani anaendelea vizuri kiafya na Mungu akijaalia atakuwepo sehemu ya kikosi kitakachowavaa Simba.

 

Kiungo huyo alishindwa kumaliza mchezo wa ligi dhidi ya Biashara United baada ya kuchezewa vibaya dakika ya kumi na kusababisha apate jeraha la goti ambalo limemuweka nje na kuzua hofu ya kuukosa mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Azam Sports Federation utakaochezwa Jumapili hii.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Niyonzima alisema kuwa hivi sasa anaendelea vizuri huku akiendelea na matibabu ya majeraha yake ili kuhakikisha anakuwepo sehemu ya kikosi cha timu hiyo kitakachocheza dhidi ya Simba.



Niyonzima alisema kutokana na matibabu anayoendelea kuyapata, ana uhakika mkubwa wa kucheza pambano hilo, hivyo mashabiki waondoe hofu, kikubwa waendelee kumuombea ili apone vizuri.“Nafahamu umuhimu mkubwa wa mchezo wetu wa nusu fainali dhidi ya Simba ambao ni lazima tupate matokeo mazuri ya ushindi.

 

“Ninaamini matokeo mazuri ya ushindi yatatutengenezea rekodi na kubwa zaidi kwetu wachezaji ni kufuzu hatua ya fainali na hatimaye kulichukua kombe hilo ili tushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

 

“Wachezaji wote malengo yetu ni kuhakikisha tunalichukua kombe hilo ili tucheze michuano ya kimataifa kwa ajili ya sisi wachezaji tujitengenezee soko nje ya nchi ambayo ndiyo malengo yetu,” alisema Niyonzima.

 

Wakati Niyonzima akitoa kauli hiyo, kuna hatihati ya nyota wengine wa Yanga kukosekana katika mchezo huo ambao ni Juma Abdul na Papy Tshishimbi, huku Balama Mapinduzi akikosekana rasmi. Hawa wote ni majeruhi.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad