Polisi yafanikiwa Kumkamata Dereva Aliyesababisha Ajari ya Watu 10 Mlima Kitonga


JESHI la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani mkoa wa Iringa limefanikiwa kumkamata dereva wa basi la Prezdar Said Abas Said (30) aliyesababisha ajali eneo la mlima Kitonga iliyopelekea vifo vya watu 10 na majeruhi 36.

Akizungumza na wanahabari ofisini kwake kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Iringa, Juma Bwire alisema kuwa mara baada ya ajali hiyo dereva huyo alifanikiwa kukimbia na kwenda kujificha kwa baba yake mdogo maeneo ya Rujewa wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.

Alisema kuwa Juni 27 katika mlima Kitonga wilaya ya Kilolo kulitokea ajali ya basi lenye namba za usajili T 326 CSX aina ya Yutong linalojulikana kwa jina la kibiashara Prezdar likifanya safari zake Iringa kwenda Dar na kusababisha vifo vya watu 10 na kujeruhi watu 36.

Kamanda Bwire alisema kuwa basi hilo liliacha njia kwenye mlima Kitonga na kutumbukia bondeni ambapo dereva wa basi alikimbia mara baada ya ajali hiyo na jeshi la polisi kumtaka mmiliki wake Neechi Msuya kuwapa ushirikiano wa kumpata dereva huyo.

Alisema kuwa mmiliki wa basi hilo, Neechi Msuya   (40) mkazi wa Dar es Salaam alijisalimisha kituoni Juni 30 mwaka huu ambapo jeshi la polisi liliendelea na msako wa kumtafuta dereva huyo hadi kumpata akiwa amejificha wilaya ya Mbarali.

Aliongeza kuwa jeshi la polisi mkoani hapa linaendelea na upelelezi na pindi ukikamilika sheria itachukua mkondo wake na kutoa wito kwa madereva kuwa makini wawapo barabarani na kufuata sheria za usalama barabarani.

Naye Mkuu wa Kikosi cha usalama Barabarani  Mkoa wa Iringa Yusuph Kamota amewataka madereva kufuata sheria za usalama barabarani hasa wanapokuwa katika katika mkoa wa Iringa na kuomba msaada kwa jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani kupata maelekezo pindi wakiona hawaelewi kuhusu mlima Kitonga.

Alisema kuwa madereva wanatakiwa kutii sheria bila shuruti na endapo ikitokea ajali wajisalimishe kwa kifungu cha sheria za usalama barabarani namba 57 hata kama dereva  alikuwa amechanganyikiwa kiasi gani anapewa masaa 12 kuweza kujisalimisha.

Alisema kuwa mtu yoyote ambaye ni dereva asipojisalimisha ndani ya masaa kumi na mbili atakamatwa tu kwani jeshi lina mkono mrefu na macho makali kuweza kubaini wanaokimbia kama ambavyo wameweza kumkamata dereva wa basi la Prezdar.

Kamota alisema kuwa kwa upande wa kikosi cha usalama barabarani wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutoa elimu ambayo imepunguza matukio ya ajali mkoani hapa na kufanya doria za barabarani usiku na mchana kwa lengo la kukabiliana na ajali.

Alisema kuwa vyanzo vya ajali viko vingi lakini makosa ya ajali yanasababishwa na makosa ya kibinadamu ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangia asilimia 76 ya ajali hivyo vyanzo kama mwendo kasi, ulevi, kutofata sheria za usalama barabarani kwa ujumla vinadhibitiwa na jeshi hilo kwa njia ya doria.

‘’ Sisi kama jeshi tumejipanga vyema kabisa natoa wito kwa madereva wawe na tahadhari katika maeneo hatarishi kama mlima kitonga na bora uwe makini kuuliza kuliko kwenda kusababisha ajali ambazo zinasababishwa na madereva wazembe’

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad