Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Wankyo Nyigesa amesema kuwa, bado wanachunguza ili kujua nini chanzo halisi kilichopelekea 'House Boy' kuwaua watoto wawili kwa kuwakatakata mapanga kwa madai ya kwamba, alikuwa na ugomvi na mama wa watoto hao ambaye na yeye alimjeruhi vibaya.
Kamanda Nyigesa amesema kuwa mara baada ya mwanaume huyo kufanya unyama huo na yeye aliuawa na wanachi, tukio ambalo limetokea Julai 8, 2020 katika Kitongoji cha Kivungwi Kwazoka mkoani humo.
"Mtu mmoja anayeitwa Yassin Abdallah "House boy", alikuwa anafanya kazi nyumbani kwa Wema Sinziye aliwaua watoto wawili kwa kuwakatakata mapanga ambao ni Rehema Makoro (5) na Aboubakar Makoro (5), baada ya kufanya tukio hilo alikamatwa na wananchi na kufungiwa kwenye Ofisi ya Kijiji cha Kwazoka na alijaribu kutoroka na wananchi wakamkamata na kumshambulia, chanzo inadaiwa alikuwa na ugomvi na mama wa watoto hao" amesema Kamanda Wankyo.
Aidha Kamanda Wankyo ameongeza kuwa, hata hivyo hali ya mama wa watoto hao siyo nzuri na amelazwa katika Kituo cha Afya cha Mlandizi.