Rais Rouhani: Iran itaibuka Mshindi Katika vita vya Kiuchumi vya Marekani
0
July 14, 2020
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema ushirikiano na mshikamano uliopo miongoni mwa mihimili mitatu ya dola, bila shaka utaipelekea Iran kuibuka mshindi katika vita vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya taifa hili.
Rais Rouhani alisema hayo jana Jumatatu katika mkutano wa Baraza Kuu la Uratibu wa Uchumi la Wakuu wa Mihimili Mitatu ya Serikali na kuongeza kuwa, ushindi unakaribia licha ya vikwazo na janga la corona.
Amekumbusha kuwa, baraza hilo la uchumi liliundwa baada ya Marekani kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kurejeshwa vikwazo shadidi dhidi ya Iran.
Rais wa Iran amesema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekuwa akisisitiza kuwa, kuna haja ya kushirikiana vimbajengo vyote vya taifa hili mkabala wa ugaidi wa kiuchumi wa Marekani. Dakta Rouhani ameeleza bayana kuwa, wananchi wa Iran wataendelea kushuhudia ustawi na maendeleo hapa nchini licha ya janga la corona na mashinikizo ya maadui wa taifa hili.
Rais wa Iran amesisitiza kuwa, kutokana na kusimama kidete taifa hili, njama za maadui za kutaka kuipa Iran pigo na kuipigisha magoti kupitia mashinikizo zitafeli tu.
Rais Donald Trump aliiondoa Marekani katika mapatano ya kimataifa ya JCPOA mnamo Mei mwaka 2018, na kutangaza kurejesha vikwazo vyote vya kidhalimu vya dola hilo la kibeberu dhidi ya taifa hili.
Tags