Leo ningependa tujifunze kitu juu ya hili suala la nidhamu ya fedha na ninatumai mtapata mawili matatu ya kujifunza na hata kubadilika.
Kuna watu umeanza nao kazi, au hata biashara lakini ukiangalia walipofikia unashangaa, huamini unaona wana maendeleo mpaka unadhani labda wao wana kitu cha ziada, kuna sehemu nyingine ambayo inawapatia pesa.
Umekata tamaa na unaishia kujipa moyo kuwa wale ni mafisadi, au wanahongwa, wazazi wao wana pesa, lakini pia unasema wanaenda kwa waganga kwani wewe pesa yako huoni inaenda wapi.
Labda sasa nikuambie ni kwanini wewe pesa haionekani katika mambo ya maendeleo.
(1) Huna Malengo
Hii ndiyo sababu ya kwanza na kukosekana kwa malengo basi kunasababisha mambo mengine yote ambayo nitayataja. Kwamba unapata pesa lakini hujapanga kuwa unataka uzitumie kwenye mambo gani, hii hukufanya kuwa na matumizi ya hovyo ambayo hayana misingi kwako.
Kuwa na pesa bila malengo ni sawa na kuwa na nauli ukiwa hujui unaenda wapi, utapanda kila basi lakini hutafika. Ni lazima uwe na malengo ili ukipata pesa kidogo tu unajua unazipeleka wapi, unailazimisha akili yako kutafuta pesa na kuzipeleka sehemu husika.
(2) Unataka Kufanya Kila Kitu Kwa Wakati Mmoja
Ndiyo hili ni tatizo kubwa, una pesa kweli lakini kwakuwa huna malengo na unataka kufanikiwa basi unaangalia watu waliofanikiwa na unajaribu kufanya kama wao. Kila siku ukiona biashara mpya unafanya, ukiona flani kanunua gari na wewe unataka.
Ukiona flani anajenga unaanza kujenga, kanunua kiwanja na wewe unanunua. Yaani hutulii na kufanya kitu kimoja, unafanya biashara tano na zote hazina hata uelekeo. Yaani ni kama unataka mtoto wa Chuo Kikuu hivyo unazaa wengi ukidhani ndiyo watafika chuo kikuu mapema, unapoteza uelekeo na unakuta pesa zako zinaishia katikati kwa kila kitu.
(3) Unatoa Zaidi Kuliko Uwezo Wako
Kama wewe ni yule mtu ambaye kila mtu akipata shida basi mtu wa kwanza kukufikiria ni wewe basi una tatizo, inawezekana unaona ni jambo jema na ni kweli kiubinadamu ni jambo jema lakini kiuchumi nikuwa unawafanyia kazi wengine.
Inawezekana hata huwapi misaada, wanakopa lakini jua wao hukopa kufanyia mambo yao ina maana wakati huo wewe hufanyi ya kwako. Unakua kama benki lakini bila riba. Kwamba wewe huna kazi ya kuzifanyia pesa zako hivyo unawapa wakazifanyie, zipo tu, watakulipa lakini watakulipa zikiwa hazina maana tena kwako.
(4) Una matumizi Ya Hovyo
Ndiyo unanunua vitu vya hovyo, kwa kuwa huna malengo kwamba hujapanga nikipata pesa nazipeleka wapi, unajikuta unakua na pesa nyingi ambazo ni cash kila siku. Kisaikolojia unajiona kama una hela nyingi, unajikuta unanunua vitu ambavyo hata ulikua huvihitaji.
Sehemu ya kutembea unapanda Bajaji kwakua una buku ipo tu, umeshiba lakini una mia mbili unanunua karanga. Huhitaji shati lakini una laki mfukoni na huna pa kuipeleka, unanunua vitu vingiii ambavyo hata huvihitaji. Pesa yako inaenda huko, lakini ungekua na malengo ungezipeleka kwenye malengo yako na si kununua hivyo.
(5) Unabeba Majukumu Ya Watu
Ndiyo unachukulia matatizo ya watu kama vile ni yako na unajipa wajibu wa kuyasuluhisha, ndugu wakikwama unajitwisha, marafiki, na kila mtu. Hapa sizungumzii kusaidia hapana bali unafanya mambo kama vile ni yako.
Baada ya muda unajikuta una majukumu mengi kuliko uwezo wako, kuna mtoto wa mjomba, shangazi, sijui nani na kila mtu anakuangalia wewe. Kinachotokea ni kuwa wewe unayachukua yale majukumu, yanakua yako na yanakua ndiyo malengo yako, kuwasaidia wahusika kuyatatua.
Lakini wale ambao unawasaidia nao wanalemaa, kwakua upo wanazilazimisha akili zao kuamini kuwa sio msaada bali ni majukumu yako. Wanakua wavivu na kuacha kutimiza wajibu wao wakijua upo. Wakati mwingine hata ukikosa wanalaumu kana kwamba ni wajibu wako.
Kama una tabia hizi ni muhimu kuanza kubadilika. Anza kwa kutambua tatizo lako, weka malengo yako ya kimaisha. Kuwa na malengo kutakuzuia kufanya mambo mengine yote haya ya kukumalizia pesa. Kutakufanya kuwa na nidhamu ya pesa na kuzitumia kutokana na malengo uliyojiwekea.
It is your time now to stand alone(Ni muda wako wa kusimama peke yako)
By Joseverest
SABABU Tano(5) Kwanini Unapata Pesa Lakini Huna Maendeleo
0
July 26, 2020
Tags