Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam Yuda Ruwa’ichi, ameagiza sadaka itakayopatikana kwenye shughuli ya kumuaga Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Benjamin William Mkapa, zitumike kukarabati nyumba ya mapadri wa Lupaso, mkoani Mtwara.
Kauli hiyo imetolewa leo Julai 26, 2020, wakati wa ibada ya kuagwa katika viwanja vya Uhuru jijini Dar es Salaam, ambapo kupitia taarifa hiyo imeeleza namna kiongozi huyo alivyokuwa akilitumikia Kanisa hilo enzi za uhai wake.
“Mhasham Baba Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki Dar es salaam, Yuda Rua’ichi kwa niaba ya Baraza la Maaskogu Tanzania, ameagiza sadaka hii ya leo itatumika kumuenzi Mzee wetu kwa kukarabati nyumba ya Mapadri Lupaso”.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, “Mzee Mkapa alikuwa na nia ya kukarabati nyumba hiyo na ukarabati huo unakadiriwa kutumia si chini ya shilingi milioni 20, pia haijawahi kukarabatiwa toka ilivyojengwa na wamisionari wa kwanza”.
Mwili wa Rais huyo Mstaafu utaagwa kwa siku tatu kuanzia leo Julai 26 hadi 28 na atazikwa kijijini kwao Lupaso, wilayani Masasi mkoani Mtwara Julai 29.