Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imezipongeza nchi za Tanzania na Mauritius kwa kufanikiwa kuingia katika uchumi wa kati na juu licha ya changamoto mbalimbali za kiuchumi zilizoikumba Jumuiya hiyo.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mussa Azzan Zungu alipofungua Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa nchi za SADC kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango, uliofanyika kwa njia ya mtandao katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Zungu alisema kuwa Tanzania ilitangazwa na Benki ya Dunia kuwa nchi yenye hadhi ya kipato cha kati na Mauritius imepanda daraja na kuwa nchi yenye hadhi ya kipato cha juu kutokana na kuongezeka kwa pato la mtu mmoja mmoja.
“Kwa Tanzania pato la mtu mmoja mmoja limeongezeka kutoka dola za Marekani 1,020 kwa mwaka 2018 na kufikia dola za Marekani 1,080 kwa mwaka 2019 na Mauritius pato la mtu mmoja mmoja limeongezeka hadi kufikia dola za Marekani 12,740 kwa mwaka 2019 kutoka na dola za Marekani 12,050 mwaka 2018”, alifafanua.
Mhe. Zungu alisema pamoja na nchi kupanda daraja hakuna nchi mwanachama ambayo imeshuka daraja na kuzishauri nchi wanachama kuyatumia mafanikio hayo kama chachu ya kujitathmini na kuangalia uwezekano wa kuleta maendeleo zaidi ya kiuchumi na kuchukua tahadhali ili chumi zisiweze kushuka hadhi.
Pamoja na mafanikio hayo, alizisihi nchi wanachama kuendelea kuchukua hatua za kukabiliana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) bila kuathiri shughuli za kiuchumi kwa kuwa ugonjwa huo ni changamoto nyingine ya uchumi wa Jumuiya hiyo.
Alisema kuwa athari za ugonjwa huo zinatajwa kusababisha chumi za nchi nyingi duniani kuporomoka kutokana na kusimama kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii ambazo kwa kiasi kikubwa zimeathiri sekta ya huduma zinazochangia zaidi ya robo ya ajira zote katika chumi za nchi wanachama wa SADC.
“Matokeo ya uchambuzi wa athari za ugonjwa wa COVID-19 kwenye viashiria vya muunganiko wa uchumi mpana kwa nchi za SADC yameonesha nchi wanachama zinatarajia kushuhudia ukuaji mdogo wa uchumi, kuongezeka kwa nakisi ya bajeti ya Serikali na kuongezeka kwa madeni”,alisema Mhe. Zungu.
Mhe. Zungu amezishauri nchi wanachama wa SADC kutafuta fedha kutoka vyanzo vyenye masharti nafuu ili kuchochea shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijami ambazo ziliatharika na COVID-19 pamoja na kupunguza mzigo wa madeni.
Aidha, aliipongeza Sekretarieti ya SADC kupitia kamati zake ndogondogo kwa kazi wanayoifanya kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kutafuta njia mbalimbali zenye ubunifu katika kugharamia miradi ya maendeleo kwa kuangalia namna bora ya uendeshaji wa Mfuko wa Maendeleo wa Kikanda na Mfuko wa Kugharamia Miradi ya Miundombinu ya Usafirishaji wa Nishati ya Umeme.
Alisema matokea ya kazi zao yatatoa fursa kwa nchi wanachama kutoa maamuzi ambayo yatapelekea kufikia malengo ya Jumuiya na kusaidia kuboresha mazingira ya kuvutia uwekezaji.
Alisisitiza kuwa Mfuko wa Kugharamia Miradi ya Miundombinu ya Usafirishaji wa Nishati ya Umeme utasaidia kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji ndani ya Jumuiya kwa kuwa suala la upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika ni sehemu muhimu itakayoiwezesha Jumuiya kufikia malengo yake ya uchumi wa viwanda.
Katika hatua nyingine, Mhe. Zungu aliihakikishia Jumuiya hiyo kuwa uchaguzi mkuu wa Tanzania unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, 2020 utakuwa huru, wa amani na utulivu utakaozingatia misingi ya demokrasia huku akizipongeza nchi za Botswana na Malawi kwa kufanya uchaguzi wao mkuu kwa amani na utulivu.