NAHODHA wa Yanga, Papy Tshishimbi amesema kuwa kuhusu kubaki ndani ya Yanga msimu ujao anamwachia Mungu.
Mkataba wa Yanga na Papy Tshishimbi unafika tamati mwezi Agosti ambao kwa sasa umebakiza siku moja kwa kuwa leo ni Julai 31, kesho ni Agosti Mosi kabla ya nyota huyo kufikia siku yake aliyosaini kuwa mchezaji huru.
Kumekuwa na mvutano mkubwa wa nyota huyo na Yanga kuhusu suala lake la kuongeza kandarasi mpya hali ambayo imemfanya nyota huyo kutomwaga saini mpaka sasa licha ya kupewa mkataba.
"Suala la mimi kubaki ndani ya Yanga kwa msimu ujao ninamuachia Mungu kwani nimekuwa nikiskia habari nyingi ambazo zinanizungumzia mimi lakini hazina ukweli.
"Naona viongozi wameanza kufanya mambo ambayo sio mazuri kwa kuzungumza kwamba wamenipa mkataba na kunipa siku za kusaini jambo ambalo sio sawa unapozungumzia mkataba sio jambo la kuzungumza kwenye vyombo vya habari.
"Kwa sasa sina furaha ndani ya Yanga kwa kuwa hakuna ambacho tumeweza kufanikiwa hakuna taji tulilochukua wala hakuna hatua ambayo tumepiga zaidi ya kuwa na maumivu tu.
"Sijacheza mechi nyingi nilikuwa nje hivyo kwa kushindwa kufikia mafanikio kwa mchezaji hawezi kuwa na furaha ila ninamuachia Mungu," amesema.
Fredrick Mwakalebela, Makamu Mwenyekiti wa Yanga amesema kuwa bado wanaendelea kufanya mazungumzo na Tshishimbi ili aongeze mkataba.