LICHA ya Simba kukabiliwa na mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam mbele ya Namungo, lakini mabosi wa timu hiyo wamefunguka kwamba hawana habari hata kidogo na fainali hiyo.
Mabosi hao wameongeza kwamba wameiweka pembeni fainali hiyo ambayo itapigwa Agosti 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Nelson Mandela uliopo Sumbawanga mkoani Rukwa, huku wakisema akili zao zote ni juu ya mechi mbili za kumaliza ligi ambapo wanataka kumaliza kwa kishindo kwa kucheza dhidi ya Coastal Union na Polisi Tanzania.
Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa ameliambia Spoti Xtra, kuwa: “Kitu kikubwa ambacho tumekiweka mbele na nguvu zetu tunaelekeza huko ni kuangalia tunamaliza vizuri mechi zetu hizi mbili za ligi.
“Hatufikirii sana kuhusu fainali ya Shirikisho, kilicho mbele yetu kwa sasa ni ligi kisha baada ya kumalizika ndipo tutaangalia maandalizi ya kwenda katika fainali hiyo ambayo tunataka kubeba ubingwa.
”Wakati Simba wakisema hivyo, mshambuliaji wa Namungo, Reliants Lusajo, amesema mechi yao ya fainali dhidi ya Simba haina mwenyewe, hivyo atakayefanya maandalizi mazuri ana nafasi kubwa ya kushinda.
“Fainali siku zote haina mwenyewe, yeyote atakayejipanga vizuri anakuwa na nafasi kubwa ya kushinda. Kwa upande wetu tumedhamiria kuibuka na ushindi kwenye mechi hiyo na sapoti kubwa tunayoipata ndani ya timu kwa kiasi kikubwa inatupa morali ya kupambana zaidi.”