Ofisi ya Mkuu wa Mashtaka Sudan imesema, imegundua kaburi la halaiki ambalo inaaminika lina mabaki ya miili ya maafisa 28 wa jeshi waliouliwa mwaka 1990 kwa tuhuma za kuandaa mapinduzi ya kijeshi dhidi ya utawala wa rais wa wakati huo Omar Hassan al-Bashir.
Maafisa hao wa jeshi waliuliwa katika mazingira ya kutatanisha baada ya kesi yao kuendeshwa harakaharaka, ikiwa ni mwaka mmoja tu tangu al-Bashir mwenyewe aliposhika madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1989. Mahali walipokuwa wamezikwa watu hao palibaki kuwa siri kwa miongo kadhaa.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Mkuu wa Mashtaka wa Sudan imesema: Ofisi hiyo imefanikiwa kugundua kaburi mola la umati ambalo inavyoonekana litakuwa ni mahali walimozikwa maafisa waliouliwa na kuzikwa kikatili.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa timu ya wataalamu 23 imefikia hitimisho hilo baada ya juhudi ilizofanya kwa muda wa wiki tatu na kwamba uchunguzi zaidi utafanyika na hatua zaidi za kitafiti zitachukuliwa kuhusiana na kaburi hilo la halaiki.
Mkuu wa Mashtaka wa Serikali ya Sudan amezihakikishia familia za maafisa hao wa jeshi waliouliwa katika utawala wa al-Bashir kwamba "jinai kama hizo hazitaachwa zipite bila ya kuendeshwa kesi ya haki na uadilifu."
Omar al-Bashir alifikishwa tena mahakamani siku ya Jumanne katika ufunguzi wa kesi yake ya kuongoza mapinduzi ya kjeshi yaliyomweka madarakani ya mwaka 1989. Endapo atapatikana na hatia anaweza kuhukumiwa kifo.
Mtawala huyo wa muda wa mrefu nchini Sudan aliondolewa madarakani na jeshi Aprili 2019 baada ya miezi kadhaa ya maandamano makubwa ya upinzani ya wananchi.
Mwezi Desemba mwaka jana, mahakama ya Sudan ilimhukumu Omar al-Bashir kifungo cha miaka miwili jela kwa makosa ya ufisadi, akiwa anakabiliwa pia na kesi kesi kadhaa na uchunguzi kuhusiana na mauaji ya waandamanaji...