Rais wa Marekani, Donald Trump kwa mara nyingine ametetea matumizi ya hydroxychloroquine kupambana na virusi vya corona, akiwachanganya maafisa wake wa afya. |
Amedai kuwa dawa hiyo ya kutibu malaria ilikataliwa kutibu Covid- 19 kwa kuwa tu yeye ndiye aliyeipendekeza.
Kauli yake imekuja baada ya Twitter kumfungia mtoto wake mkubwa kwa kuchapisha taarifa kuhusu kutumia hydroxychloroquine.
Hakuna ushahidi kuwa dawa hiyo inaweza kupambana na virusi na wadhibiti wa dawa wanatahadharisha kuwa inaweza kusababisha matatizo ya moyo.
Mwezi uliopita, mamlaka ya chakula na dawa nchini Marekani (FDA) ilitahadharisha kuhusu matumizi ya dawa kwa ajili ya tiba ya virusi vya corona, baada ya ripoti kuhusu ''matatizo makubwa ya moyo'' na masuala mengine ya kiafya.
Mamlaka hiyo ilisitisha matumizi ya dharura ya dawa hiyo kutibu Covid-19. Shirika la afya duniani (WHO) limesema kuwa ''mpaka sasa hakuna ushahidi'' kuwa dawa hiyo ina ufanisi kutibu au kuzuia virusi vya corona.
Rais Trump na mtalamu wa kupambana na virusi vya corona nchini Marekani Dkt Anthony Fauci wamekua wakitofautiana juu ya njia za kupamabana na usambaaji wa virusi vya corona mkiwemo matumizi ya dawa ya hydroxychloroquine kama tiba inayopigiwa debe na Trump.
Rais Trump na mtalamu wa kupambana na virusi vya corona nchini Marekani Dkt Anthony Fauci wamekua wakitofautiana juu ya njia za kupamabana na usambaaji wa virusi vya corona mkiwemo matumizi ya dawa ya hydroxychloroquine kama tiba inayopigiwa debe na Trump
Tafiti zilizofanywa na WHO, na Taasisi za kitaifa za masuala ya afya na watafiti wengine hazijapata ushahidi kuwa hydroxychloroquine zinapotumika na dawa ya azithromycin au bila dawa hiyo kama ilivyoelezwa na Trump inasaidia kutibu virusi vya corona.
Trump alianza ushawishi wa dawa hiyo kwa mara ya kwanza mwezi Machi. Aliwaambia wanahabari siku ya Jumanne: ''Ninapopendekeza jambo, wanapenda kusema 'usitumie' ''
Trump, 74, aliwashangaza waandishi wa habari mwezi mwezi aliposema kuwa alianza kutumia dawa hiyo ambayo haijathibitishwa kutibu corona.
Siku ya Jumanne, alisema: ''Ninaweza kusema hivyo kwa kutegemea machapisho mengi niliyoyasoma kuhusu suala hili, ninafikiri inaweza kuwa na matokeo chanya katika hatua za mwanzoni.
''Sifikiri kama unapoteza chochote kwa kufanya hivyo, inaonekana tu kuwa si maarufu sana.''
Rais Trump na mtoto wake Donald Trump Jr. ni miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii waliosambaza video siku ya Jumatatu ya jumuia ya madaktari wajiitao American Frontline Doctors, wanaohamasisha kuwa hydroxychloroquine ni tiba ta Covid-19.
Facebook na Twitter waliondoa maudhui hayo, wakisema kwamba ni taarifa za kupotosha.
Twitter pia ilimfungia mtoto wa Trump kwa saa 12 kama adhabu kwa kusambaza kipande hicho cha video.