Tundu Lissu Awaaga Watanzania Waishio Ubelgiji...Tayari Kurejea Tanzania
0
July 26, 2020
#PICHANI: Makamu Mwenyekiti wa @ChademaTz Mhe.Tundu Lissu akiagana na Watanzania walioko Beligium tayari kwa safari ya kurudi Tanzania ambapo anatarajiwa kuwasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jumatatu saa saba mchana.
Mwanasiasa huyo aliyabainisha hayo siku ya Jumanne tarehe 21 Julai 2020 wakati akizungumza kwa njia ya mtandao safari yake ya kurejea Tanzania kutoka nchini Ubelgiji.
Lissu amekuwa nje ya Tanzania tangu tarehe 7 Septemba, 2017 aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana akiwa nje ya makazi yake Area D jijini Dodoma.
Alifikwa na mkasa huo mchana wakati akitoka kuhudhuria mkutano wa Bunge uliokuwa ukiendelea.
Baada ya kushambuliwa, Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali na usiku huo huo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya.
Lissu alipata matibabu hospitalini hapo hadi tarehe 6 Januari 2018 alipohamishiwa nchini Ubelgiji kwa matibabu na tayari amekwisha kueleza yeye mwenyewe amepona.
Katika mazungumzo yake hayo, Lissu amerejea kuwashukuru Watanzania, Wakenya na Wabelgiji na watu mbalimbali waliojitolea kumsaidia kuhakikisha anapona akisema hatowasahau.
Lissu ni miongoni mwa wanachama saba wa Chadema waliochukua na kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020.
Amesema, amekaa Ubelgiji kwa miaka miwili na nusu huku akiwashukuru majirani zake kwa kumhifadhi kwa kipindi chote.
Tags