Mahakama ya Uganda imemuhukumu mwanaume mmoja kifungo cha miaka kumi na moja kwa kuua sokwe mwenye mgongo wa rangi ya fedha(silver) mwezi Juni.
Sokwe huyo aliyekuwa akiitwa Rafiki -alikuwa kiongozi wa kundi wa sokwe ambao hupatikana kwa nadra katika hifadhi ya sokwe nchini humo.
Rafiki alikutwa amefariki mapema mwezi Juni, akiwa na jeraha tumboni.
Felix Byamukama,alikiri mahakamani kuhusika katika kesi tatu za hifadhi ya wanyama kwa kumuua swala na nguruwe pori pia.
Wahifadhi wanyama walikuwa wanahofia kuwa kundi la wanyama hao ambao wamewazoea binadamu, wataacha mahusiano hayo.
Lakini mamlaka ya wanyama pori nchini humo inasema wamethibitisha kuwa kundi la sokwe kumi na moja bado wanaishi kama familia.
Kulikuwa na zaidi ya sokwe 1,000 ambao walikuwa katika hifadhi za wanyama nchini Uganda, Rwanda na DRC. Mataifa hayo matatu yanategemea utalii wa wanyama hao kuwaingizia kipato.
Mamlaka ya wanyama pori hivi karibuni ilieleza wasiwasi wa kuongezeka kwa ujangiri , kwa zaidi ya matukio 300 kurikodia kwa miezi kadhaa wakati marufuku ya kutoka nje utalii ulikuwa umesitishwa pia.