Je, wewe uko kwenye kundi lipi?
Hiki ndicho ninachotaka kuwasaidia siku ya leo.
Lakini leo ningependa kuwazungumzia watu wenye haiba ya ukamilifu. Hawa ni wale watu ambao wanaamini kwamba, hawapaswi kukosea. Kwao, wanaamini kuwa, mtu anatakiwa afanye kwa usahihi na ukamilifu na kukosea kuna maaana ya udhaifu mkubwa na unyonge.
Nguvu kubwa ya watu hawa iko kwenye usahihi, ukamilifu na kurekebisha makosa. Iko kwenye kufanya ambavyo mtu angetakiwa kufanya, na kufanya mambo kwa usahihi.
Watu hawa wenye haiba ya usahihi huko ndani mwao kuna sauti (little voices) ambazo zina nguvu sana kwao, zenye kuwaamuru wafanye mambo bila kukosea. Lakini, sauti hizi zinakosoa na kuwadhibiti wahusika kwa njia yenye kuwaumiza. Huwa ni sauti zenye kuzalisha mashaka. Kushtakiwa na dhamira na hofu.
Kwa sababu ni watu wanaoamini katika “nzuri na sahihi,” inakuwa ni vigumu sana kwao kuishi na watu wengine kwa amani. Mbaya zaidi ni kwamba, wapenzi wao hupata shida sana kuendana nao. Hii ni kwa sababu, wanataka mambo yaende kwa njia yao, yawe sahihi. Kuna, “ingetakiwa iwe hivi,” nyingi sana.
Watu hawa huwafanya wengine wanaohusiana nao kuhisi kama vile wanatembea juu ya maganda ya mayai.
Kwa nini?
Ni kwa sababu hawa watu wenye haiba hii, hujiona wanaweza kuliko wengine na wanastahili kuliko wengine. Watu hawa wana tabia ya kusema au kumwambia mtu ukweli moja kwa moja kwa njia yenye kukera sana. Hali hii huwasononesha watu wanaoambiwa ukweli.
Watu ambao wameoa au kuolewa na wenye haiba hii, huwa wanatamani kuona mambo yakiwa tofauti kidogo. Wanajihisi kufungwa pumzi, kukaliwa kooni, kufungiwa kwenye dema na kushindwa kuona nafasi yao kama watu huru. Huhisi kuwa wao ni watoto, wanaokosea kila kitu, kwani ndivyo sauti za wapenzi wao zinavyowaambia kila wakati.
Inabidi mtu wa haiba hii ajifunze kukubali makosa, kwamba, kukosea siyo udhaifu, bali kujifunza. Ajue kwamba, kuna njia nyingi za kujifunza mambo, siyo njia moja tu ya “usahihi.” Kuna ya kukosea na kujifunza makosa, halafu ndiyo usahihi ufuate.