Ndugu zetu waislam hivi karibuni watakuwa wakiingie kwanye mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani ambapo mara nyingi soko la tende limekuwa likiongezeka sasa hapa naomba tufahamu kwanini tende hutumika zaidi katika kipindi hiki.
Ikumbukwe kwamba Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, alisema, “Fungueni swaumu zenu kwa tende, au, vinginevyo, basi fungueni kwa maji, kwani ni twahara.” (Abu Dawud na Tirmidh).
Hivyo chakula kilichozoeleka zaidi kwa futari ni tende. Hii inaendana na Sunna ya Mtume, swallalllahu alayhi wa Sallam. Baada ya kushinda kutwa nzima na swaumu, kiwango cha sukari ya mwili hupungua na hivyo huhitajika kurejeshwa upya.
Ingawaje tende si chakula cha kushibisha kwa upesi, lakini huaminika kuwa ndicho chakula kisicho na mafuta, na ni chanzo madhubuti cha sukari na hivyo kurejesha kwa haraka sukari iliyopungua mwilini.
Ifahamike kuwa nusu ya sukari zitolewazo na tende ni kwa ajili ya glukosi pekee, lakini mbali ya glukosi, tende pia ni chanzo kizuri cha nyuzinyuzi ambazo husaidia kuboresha michakato mzima wa umeng’enyaji chakula mwilini.
Pamoja na hayo, tende ni chanzo kizuri cha madini ya potasiamu ambayo ni muhimu kwa usawazishaji wa maji ndani ya mwilini.