Wachimbaji Madini Wafia Mgodini kwa Kukosa Hewa safi
0
July 26, 2020
WACHIMBAJI wadogo wawili wamefariki dunia ndani ya mgodi, baada ya kukosa hewa safi walipokuwa kwenye shimo lenye urefu wa Mmita 21.5 na kuamua kuwasha mashine maalumu ya kutoa maji ndani ya mgodi huo ili waweze kuendelea na kazi ya kutafuta madini.
Tukio hilo lilitokea Julai 23, saa 9:30 alasiri, katika Kijiji cha Kalundi, Kata ya Kipande, Tarafa ya Kate Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.
Waliofariki ni Justine Salawa (27) mkazi wa Kijiji cha Kalundi na Fredy Agustino Mkazi wa Kijiji cha Kaoze wilayani Sumbawanga.
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ralph Meela alisema wachimbaji hao waliingia kwenye shimo hilo wakiwa watatu na ghafla maji yalIibuka hali iliyosababisha kushindwa kuendelea na kazi hiyo, hivyo wakaamua kuwasha mashine ili kutoa maji hayo.
Alisema baada ya kuwasha mashine hiyo, moshi ulitanda katika shimo hilo, hali iyosababisha kukosa hewa safi na kuzidiwa na hewa ukaa lakini mmoja wao alifanikiwa kutoka nje na kuokoa maisha yake, huku wengine wakishindwa kupata msaada wa haraka na kufariki dunia.
Meela alisema baada ya tukio hilo, jeshi la zimamoto na uokoaji lilifika katika eneo la tukio lakini kutokana na umbali walichelewa na walikuta watu hao wamefariki dunia na kufanikiwa kuitoa miili hiyo ndani ya mgodi huo kisha kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kukabidhiwa kwa ndugu kwaajili ya maziko.
Alisema kuwa jeshi la polisi linamshikiria mmiliki wa mgodi huo kwa kosa la kuanzisha mgodi huo na kufanya uchimbaji wa madini bila kuwa na kibali.
Alitoa wito kwa wananchi wanaomiliki migodi na maeneo ya machimbo ya madini kufuata taratibu na kuwa na vibali kwani Serikali itakuwa inawafanyia ukaguzi na kuwapa taratibu za kufanya shughuli zao bila kutokea kwa maafa yanayo epukika.
Tags