MWENYEKITI wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu, Semistocles Kaijage, amewataka wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha wanazingatia maadili na kuepuka dosari ambazo zinaweza kuathiri Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, huku akisema wapiga kura walio kwenye daftari ni milioni 29.
Akifungua kikao kazi cha wasimamizi wa uchaguzi jijini Dodoma juzi, aliwataka kuzingatia sheria, maadili ya uchaguzi na maelekezo ya tume na watakaokiuka watakuwa wametenda kosa la jina kwa mujibu wa kifungu 98 cha Sheria ya Uchaguzi.
Pia alisema pamoja na wajibu wao wa kusimamia uchaguzi, wanatakiwa kujua jiografia, mazingia na maeneo wanayosimamia na wana wajibu wa kusimamia watendaji wa uchaguzi waliopo chini yao ili watekeleze majukumu yao kwa weledi na umakini.
“Wasimamizi wa uchaguzi hii ni nafasi ya kubadilishana na kupeana uzoefu wa utekelezaji shughuli za uchaguzi ili kuhakikisha tunaepusha dosari ambazo zinaweza kujitokeza na kuathiri shughuli za uchaguzi,” alisema Kaijage.
Kaijage alisema tume ilianza kujiandaa kwa uchaguzi huo siku nyingi kwa kufanya shughuli nyingi zikiwemo za kukamilisha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura ambao umefanyika mara mbili. Awamu ya kwanza ilifanyika Julai 18, 2019 hadi Februari 23, 2020 na awamu ya pili Aprili 17 hadi Mei 04, 2020.
“Awamu ya pili ya uboreshaji ilifanyika pamoja na uwekezaji wazi wa daftari la awamu ya kwanza katika vituo 37,814 vilivyotumika katika uboreshaji awamu ya kwanza,” alisema.
Kaijage alisema uwekaji wazi wa daftari awamu ya pili ulifanyika Juni 17-20, mwaka huu ambapo daftari la wapigakura lilibandikwa katika vituo vyote vilivyotumika wakati wa uandikishaji awamu ya kwanza.
Kaijage alisema katika uboreshaji wa daftari hilo awamu zote mbili, waliandikisha wapigakura wapya 7,326,552 sawa na asilimia 31.63 ya wapigakura 23,161,440 walioandikishwa mwaka 2015.
Aidha, wapiga kura 3,548,846 walioboreshewa taarifa zao na wapigakura 30,487 waliondolewa kwenye daftari kwa kukosa sifa na hivyo daftari lina wapigakura takaribani milioni 29.
Kaijange aliwataka wasimamizi hao kuwa makini na matumizi ya fedha zinazotumwa kwao kwa kuzingatia sheria za fedha za umma, ya manunuzi ya umma, ya uchaguzi na maelekezo yanayotolewa na tume wakati wa matumizi ya fedha hizo ambazo awamu ya kwanza zimeshatumwa.
Alisema katika uchaguzi wa mwaka huu, hakuna marekebisho ya sheria za uchaguzi, lakini tume imefanya marekebisho kanuni za uchaguzi wa rais na wabunge na kanuni za uchaguzi wa serikali za mtaa zote za mwaka huu na maboresho ya maelekezo kwa ajili ya wadau na watendaji yamekamilika.
Kaijage alisema tume kwa kushirikiana na Serikali na vyama vya siasa iliandaa maadili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ambayo yalisainiwa Mei 27, 2020 yameainisha mambo yanayotakiwa kuzingatiwa na tume, vyama na serikali. Hivyo wasimamizi wa uchaguzi ambao watakuwa wenyeviti wa kamati za maadili katika majimbo wanayosimamia, wayasome na kuyaelewa vizuri ili kuyasimamia vizuri.
Kaijage alisema kanuni zilizorekebishwa zinaelekeza uteuzi wa wagombea, upigaji kura na mchakato mzima wa uchaguzi na hivyo watendaji wa tume wanatakiwa wakato wote kuwepo katika maeneo ya kazi, kwani uzoefu unaonesha wamekuwa wakikiuka maadili kwa kutokaa vitutoni na hivyo kusababisha malalamiko.
Tume imeshanunua baadhi ya vifaa vya uchaguzi pamoja na kuchapisha fomu, sheria za uchaguzi, kanuni na maelekezo na baadhi vimeshaanza kupokelewa bohari kuu ya tume, hivyo vikisambazwa kwao wasimamizi mnatakiwa kuvipokea, kuvihifadhi katika hali ya usalama.
Tayari tume imeshatoa vibali 97 kwa ajili ya watazamajini wa uchaguzi mkuu wa ndani na tayari imewasilisha mwaliko kwa wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika mashariki kuruhusu watazamaji wa kimataifa kuja nchini kuangalia uchaguzi huo.
Pia Tume imetoa vibali kwa asali 245 Tanzania Bara na asasi saba za kiraia Zanzibar kwa ajili ya kutoa elimu kwa wapigakura wakati wa uchaguzi, hivyo wasimamizi wanatakiwa kuhakikisha elimu inayotolewa katika maeneo yao inazingatia mwongozo wa utoaji elimu uliotolewa na tume.
Pia aliwataka wasimamizi hao kuhakikisha mawakala wa vyama wanaruhusiwa kuwepo vituoni, kwani kitendo hicho kioongeza uwazi lakini watakuwa na vitambulisho vinavyotambulisha.
Alisema kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo vituoni jambo ambalo linasahdia kudhihirisha uwazi katika uchaguzi huo, ni wajibu wao kuhakikisha wanakuwa na vitambulisho na wakati wakiangalia utekelezwaji wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi.
Katika kufanikisha uchaguzi huo tume imeteua watendaji wake wakiwemo waratibu 28, wasimamizi wa uchaguzi 194, wasimamizi wasaidizi wa majimbo 742 na wasimamizi wasaizidi katika kata 7,912.