Maelfu ya Wasudani wamefanya maandamano wakipinga marekebisho ya sheria za nchi yaliyofanywa na serikali ya mpito ya nchi hiyo na kupiga nara zinazoipinga serikali hiyo.
Waandamanaji hao wametoa wito wa kuondolewa madarakani serikali ya sasa ya Sudan.
Waandamanaji hao pia wametaka kutekelezwa sheria za dini, kufutwa marekebisho yaliyofanywa na Serikali ya Mpito kuhusiana na sheria za murtadi, kuhalalisha pombe kwa wasio Waislamu nchini Sudan na ukahaba na kuboreshwa hali ya maisha ya wananchi.
Maandamano ya sasa ya Wasudan ni ya pili kufanwa katika kipindi cha siku saba zilizopita dhidi ya serikali ya Waziri Mkuu wa Serikali ya Mpito ya nchi hiyo, Abullah Hamdok.
Wasudani wanasema marekebisho ya sheria yaliyofanywa na serikali ya sasa ya Khartoum yanapingana na mafundisho ya Uislamu na kwenda sambamba na matakwa ya wasekulari.
Wakati huo huo raia 20 wameuawa katika shambulizi lililofanywa na kundi moja la wanamgambo katika eneo la Darfur huko magharibi mwa Sudan.
Maafisa wa serikali za mitaa wametangaza kuwa kundi hilo la wanamgambo wasiojulikana limewafyatulia risasi raia katika kijiji kimoja cha kusini mwa Darfur na kuua watu 20 na kwamba wengine 22 wamejeruhiwa.