Watanzania Wanaoishi Nchini Marekani Wampongeza Rais Magufuli Alivyopambana na Corona



JUMUIYA ya Watanzania wanaoishi nchini Marekani (ATC) wamempongeza Rais John Magufuli, kwa namna alivyofanikiwa kupambana na mlipuko wa virusi vya corona.

Pamoja na pongezi hizo wametoa msaada wa vifaa mbalimbali vya kujikinga na ugonjwa wa Covid-19, vyenye thamani ya Sh milioni 7.4.

Akizungumza juzi wakati wa makabidhiano ya msaada huo kwa Mkuu wa wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, mwakilishi wa watanzania hao Amos Lwiza, alisema msaada huo ni sehemu ya kuunga juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya virusi vya corona.

Lwiza alisema kuwa Watanzania wanaoishi Marekani, katika majimbo ya Washington DC, Maryland na Virginia (DMV), wanajiona fahari kwa namna Rais Magufuli, alivyofanikisha ushindi dhidi ya mapambano ya virusi vya corona nchini.

“Sisi Watanzania tunaona fahari kubwa sana kwetu na tunatembea kifua mbele hivi sasa kutokana na rais alivyofanikisha mapambano haya ya corona na tumeamua kumuunga mkono katika juhudi hizo kwa kutoa msaada huu wa vifaa vya kujikinga na corona,”alisema.

Alisema vifaa walivyotoa ni sabuni, vitakasa mikono pamoja na glovu ambazo zitasambazwa katika zahanati, vituo vya afya pamoja na hospitali zilizopo wilayani Chamwino. Mkuu wa wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga, alisema wanashukuru kwa msaada huo ambao utasaidia kuendeleza mapambano dhidi ya virusi vya corona.

“Corona bado ipo hivyo hatuna budi kuendelea kuchukua tahadhari zote zinazotolewa na wizara ya afya, hivyo kwa kupata vifaa hivi tutahakikisha kuwa tunavipeleka katika maeneo yote yenye uhitaji,”alisema.

Aidha alitoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza kutoa misaada kutokana na hivi sasa mahitaji kuwa juu kutokana na shule zote kufunguliwa.

“Shule zote zimefunguliwa na mpaka sasa hali siyo mbaya lakini pia bado juhudi zinahitaji kwani watoto wetu shuleni hivi sasa wanahitaji maji, sabuni pamoja na vitakasa mikono ili kuweza kuendelea kujikinga na virusi vya corona,”alisema Nyamoga Naye Mganga mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Dk Kessy Eusebi alisema kuwa vifaa hivyo watavigawa katika zahanati na vituo vya afya mbalimbali ambavyo vinamahitaji.


Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Magufuli ni Fahari yetu Ughaibuni.
    Tumepata hheshima na tunaendelea kuipata, ukiangalia miaka 8-9 iliyopita
    wala hawakuwa na habari na sisi Leo
    wanataka kuijua Tz na Watanzania kwa
    Heshma na Adabu.

    Endelea Baba waambieni Mabalozi tutampigiaje kura zetuwa Ughaibuni kadi zetu za mpiga kura tunazo Kabudi
    you need to ensure our constitutional
    right is being meet .

    Hongere Jemedari wetu JPM.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad