NAIBU Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amemsimamisha kazi Ofisa Madini Athumani Massawe kwa tuhuma za kujihusisha kuchukua asilimia 10 ya fedha kutoka kwa wanunuzi wa madini kinyume na taratibu za Serikali .
Agizo la kusimamishwa kazi kwa ofisa huyo, alilitoa jana wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakati akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa sekta hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanunuzi wa madini.
Akiwa kwenye mkutano huo Naibu Waziri Nyongo, baada ya kusikia malalamiko hayo alisema kuwa Serikali haiwezi kumvumilia mtumishi yeyote ambaye anakwenda kinyume na taratibu na kusababisha mapato ya Serikali kupotea bila utaratibu kwa masilahi ya mtu binafsi.
“Natoa magizo Ofisa Madini Athumani Massawe wa kituo hiki cha soko la Tunduru asimame kazi ili kupisha uchunguzi na akibainika kuwa tuhuma ni za kweli sheria ichukue mkondo wake.
“Ninyi wenyewe wachimbaji wadogo ni mashaidi Rais Dk. John Magufuli amekuwa akihangaika namna ya kuwasaidia wachimbaji wadogo na leo hii mnathaminiwa na hakuna anaye wanyanyasa, hivyo muendelee kufuata taratibu zilizowekwa ikiwemo madini yenu kuuzia sokoni na siyo vichochoroni,” alisema Nyongo
Alisema kuwa ofisa huyo inadaiwa alikuwa akifanya mchezo huo kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa Chama cha Wachimbaji Wadogo (Ruvrema), ambao ofisi zao zipo kwenye jengo la soko hilo.
Aidha alisema kuwa Wizara ya Madini imefungua masoko hapa nchini takribani 28 na kati masoko yanayotegemewa licha ya kuwa yaliyopo Arusha na Mererani pia Serikali hutegemea Soko la Wilaya ya Tunduru ambalo hutoa madini aina ya Safaya (Vito)ambayo yanachimbwa katika eneo la Mto Mhuwesi wilayani humo.
Awali akizungumzia katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro alisema kuwa kumekuwepo na changamoto ya kukosa mawasiliano baina ya ofisi yake pamoja na wachimba madini hao jambo ambalo limekuwa likisababisha baadhi ya watumishi ufanya kazi kinyume cha taratibu na sheria zilizopo.
Kutokana na hali hiyo alisema kuwa kuanzia sasa ofisi ya Chama cha Wachimbaji Wadogo (Ruvrema), ihamishwe katika jengo hilo na kuziacha ofisi za manunuzi pekee ili kuondoa dhana ya kuingiliana katika majukumu ya utendaji wa kazi.
Naye Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo, Isaack Ngerangera, alisema kuwa chama hicho kimeshachukua hatua ya kuwasimamisha viongozi watatu ngazi ya wilaya wanaodaiwa kujiingiza kwenye tuhuma hizo, huku wakimuomba Mkuu wa Wilaya, Mtatiro kuwa ofisi yao ibakie kwenye jengo hilo kwa kuwa ipo nje ya soko la manunuzi.
Akitoa malalamiko yao kwa Naibu Waziri wa Madini, mmoja wa wachimbaji wadogo, Shakina Maya alisema kuwa vitendo vya asilima 10 vimekidhiri katika soko hilo hasa kwa wanunuzi wa kutoka Thailand na Sri Lanka ambapo alidai wamekuwa wakionewa kiasi cha kutaka kususia shughuli hiyo.