Waziri wa Elimu nchini Kenya Atangaza Vyuo Vikuu vyote Kufunguliwa Januari 2021



Waziri wa elimu nchini Kenya Profesa George Magoha ametangaza vyuo vikuu vyote nchini humo kufunguliwa Januari 2021.

Hatua hiyo imekuja baada ya kubainika kuwa havijaweza kuweka mikakati madhubuti inayohitajika kuambatana na muongozo wa wizara ya afya kudhibiti maambukizi ya Covid 19.

Katika taarifa kwa waandishi wa habari Profesa Magoha amesema uchunguzi wao umebaini kuwa ni asasi chache mno zilizochukua hatua stahiki za kuwalinda wanafunzi, wahadhiri na wafanyakazi wengine wa vyuo dhidi ya virusi vya Corona.

Mapema mwezi huu, wizara ya elimu ilikuwa imetangaza kuwa vyuo vingefunguliwa tena mwezi Septemba mwaka huu.

Huku shule za msingi na za upili zikitarajiwa kufunguliwa tena Januari mwaka ujao kutokana na tishio la maambukizi ya Corona.

Taasisi za elimu zilifungwa mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, kwa hofu ya watoto kuambukizwa virusi vya Corona shuleni.

Wizara ya elimu imesema vyuo vikuu vinapaswa kuendelea kutoa mafunzo, mitihani na hata kuandaa shughuli za mahafali kupitia mitandao, huku kipaumbele kiwe wanafunzi walio katika mwaka wao wa mwisho wa masomo.

Wizara ya afya inazitaka taasisi za elimu kuwa na maeneo ya kutosha ya kunawa mikono kwa maji tiririka, vitakasa mikono, mashine za kupima joto, maeneo ya kuwatenga wanafunzi wanaoshukiwa kuathirika na kutoa barakoa.

Hali kadhalika, taasisi hizo zinahitajika kunyunyiza dawa wadudu mara kwa mara katika majengo na usafi kuzingatiwa katika maeneo yanayoguswa mara kwa mara, mbali na kuhakikisha hakuna kukaribiana kwa wanafunzi, walimu na wafanayakazi wengine.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad