Shirika la Afya Duniani (WHO) na kituo cha udhibiti wa magonjwa barani Afrika (CDC) yametangaza kuwa, yameanzisha juhudi kuangalia uwezekano wa madawa ya mitishamba katika kupambana na janga la virusi vya corona.
Jopo hilo jipya la ushauri litaunga mkono nchi katika majaribio ya kitabibu, utafiti mwingine na utengenezaji wa dawa nyingine za kienyeji wakati hivi sasa janga la Corona likisambaa kwa kasi katika baadhi ya sehemu za bara la Afrika.
Kesi zilizothibitishwa katika bara hilo zimepindukia 750,000, zaidi ya nusu zikiorodheshwa nchini Afrika Kusini.
Taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) imesema kuwa, dawa za asili na mitishamba, zina faida nyingi na bara hilo lina historia ndefu ya matumizi yake. Mkuu wa WHO barani Afrika, Matshidiso Moeti, amesema utafiti unapaswa kuwekwa katika misingi ya kisayansi.
Maambukizi ya virusi vya corona duniani yameongezeka na kukaribia milioni m15 na nusu.
Marekani imeendelea kuwa mhanga mkuu wa virusi vya Corona ulimwenguni ambapo hadi sasa zaidi ya watu milioni nne wameambukizwa virusi hivyo nchini humo huku karibu watu laki moja na nusu wakiwa wameshafariki dunia. Ripoti ya Kituo cha Udhibiti na Kinga ya Maradhi cha Marekani CDC imeeleza kuwa, kuna uwezekano idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona nchini humo ikawa mara 10 zaidi ya takwimu rasmi zinazotolewa na serikali.
Huku kukitolewa indhari mbalimbali za kuendelea kushuhudiwa maambukizo ya virusi vya corona duniani katika siku za usoni, hadi sasa wataalamu bado hawajafanikiwa kugundua chanjo au dawa ya kutibu maradhi ya COVID-19 yanayosababishwa na virusi vya corona.