Wizara Ya Mifugo Na Uvuvi Yadhamiria Kufikia Malengo Ya Kisekta Katika Uchumi Wa Kati.



Na. Edward Kondela
Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendeleza jitihada za kuhakikisha inafikia malengo ya kisekta baada ya Tanzania kuorodhesha na Benki ya Dunia hivi karibuni kuwa moja ya nchi zilizoingia katika uchumi wakati ulioainishwa katika dira ya taifa ya mwaka 2020-2025.

Akizungumza leo (08.07.2020) wakati wa mafunzo rejea yanayotolewa na Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) iliyo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwa wafugaji katika Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mhandisi Mshamu Munde, ameipongeza LITA kwa kutoa mafunzo hayo yenye lengo la kuifanya wilaya hiyo kuwa na shughuli nyingi za kiuchumi ukiwemo ufugaji wa kuku kibiashara.

“Sisi siyo wafugaji, sasa katika kupanua wigo wa shughuli za kiuchumi mwisho wa siku tunakuwa na shughuli nyingi za kiuchumi kikiwemo kilimo na uvuvi ambavyo tumeshavizoea sasa tunataka kwenda kwenye ufugaji, ufugaji wa wanyama na ndege wafugwao kwa maana ya kuku, wengi wenu mnafuga kuku wa kienyeji ambao siyo wa kibiashara tunapoongelea uchumi tunataka chakula lakini pia kupata kipato kwa ajili ya matumizi mengine.”  Amesema Mhandisi Munde

Mhandisi Munde amefafanua kuwa kupitia mafunzo hayo wanafunzi pia watajifunza kwa vitendo ufugaji wa kuku na hatimaye kufundisha jamii inayowazunguka, kutokana na mafunzo hayo kujumuisha walimu kutoka shule tano za msingi zilizopo Wilayani Mkuranga ambazo pia zitapatiwa vifaranga vya kuku aina ya kroiler vikiwa na umri wa wiki tatu.

Aidha ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia kwa naibu waziri wa wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega kwa kuhamasisha ufugaji wa kuku kibiashara katika maeneo mbalimbali nchini ili wananchi wajikwamue kiuchumi ikiwemo Wilaya ya Mkuranga, ambapo Oktoba 4, Mwaka 2019 Mhe. Ulega aliahidi kutoa vifaranga vya kuku aina ya kroiler kwa vikundi 25 vya wilaya hiyo vilivyohudhuria mafunzo kipindi hicho.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Angello Mwilawa akizungumza kwenye mafunzo rejea kwa wafugaji Wilayani Mkuranga, amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya mapinduzi makubwa katika sekta za mifugo na uvuvi kwa kuhamaisha ufugaji endelevu na ufugaji bora kote nchini.

Dkt. Mwilawa amesema wizara imekuwa ikifanya mkakati wa kuboresha uzalishaji na biashara ya ndege wafugwao wakiwemo kuku, kwa kuwa kaya nyingi nchini zimekuwa zikitegemea ufugaji wa kuku ambao umekuwa na faida kwa pato la taifa kwa jumla na ngazi ya kaya kwa kuboresha lishe na hivyo wizara kuhimiza ufugaji wa kuku kwa kuwa mtaji wake ni mdogo.

 “Sisi kama wizara tunahimiza wafugaji wetu wajikite katika ufugaji wa kuku kwa kuwa wanahitaji mtaji mdogo, lakini kadri wanavyojipanua hao kuku wanaweza kumuongezea mtaji kuwa mkubwa zaidi hasa kwa kumuongezea kipato na kuleta faida katika ngazi ya kaya na ukubwa wake katika ngazi ya taifa, sisi kama wizara kuku ana mchango mkubwa katika ngazi ya taifa na kaya endapo shughuli ya ufugaji ikifanyika katika ubora.”

Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Utafiti kutoka Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) Bw. Silaju Kapembe akitoa mafunzo kwa wafugaji hao amewataka kabla ya kuanza kufuga kuku ni muhimu kuandaa mazingira bora ili kuhakikisha vifaranga vinamudu mazingira ya awali huku mmoja wa wafugaji hao Bw. Nyanza Mwinshehe akiishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuandaa mafunzo ya ufugaji bora wa kuku na kuiomba wizara hiyo kuweka mkazo zaidi wa shughuli za ufugaji katika Wilaya ya Mkuranga ili kuongeza wigo wa vyanzo vya kiuchumi.

LITA imekuwa na malengo makuu ya kutoa mafunzo kwa wafugaji wakiwemo wa kuku katika Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani ili kuondokana na ufugaji wa mazoea na kwenda kwenye ufugaji wenye tija na endelevu

Pia kuyaongezea thamani mazao yanayotokana na mifugo ili kuwa na kipato kikubwa zaidi pamoja na kuongeza lishe katika familia.

Wafugaji hao ambao wanapatiwa mafunzo na LITA ambayo iko chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi wanatokana na ahadi waliyopatiwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega Oktoba 4, Mwaka 2019 wakati wa mafunzo rejea Wilayani Mkuranga ambapo wanatarajia kesho (09.07.2020) kukabidhiwa vifaranga vya kuku aina ya kroiler vyenye umri wa wiki tatu kupitia katika vikundi 25.

Mwisho
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad