Yanga Yampandisha Ndege Muuaji wa Simba



YANGA imeonekana imepania kuendeleza ubabe kwa mtani wake wa jadi, Simba baada ya jana kumpandisha ndege kiungo wake mchezeshaji fundi, Issa Mohammed ‘Banka’ kwa ajili ya kuiwahi kambi ya timu hiyo huko Bukoba.

 

Yanga ipo Bukoba tangu juzi Jumatatu ilipofika kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa leo Jumatano kwenye Uwanja wa Kaitaba huko Kagera.

 

Kiungo huyo yupo nje ya timu hiyo kwa muda mrefu akidai kumaliziwa fedha zake za usajili alizotakiwa kumaliziwa mwanzoni mwa msimu huu kabla ya kujiondoa kwenye kambi ya timu hiyo na kwenda kujichimbia kwao Zanzibar.



Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, kiungo huyo juzi alitumiwa tiketi ya ndege aina ya Air Tanzania na jana Jumanne aliondoka kuwahi kambi hiyo kwa ajili ya kuuwahi mchezo mgumu dhidi ya Kagera, lakini tageti ikiwa mechi ya Simba.

 

Mtoa taarifa huyo alisema Banka amekubali kupanda ndege hiyo kwenda Kagera baada ya kufikia makubaliano mazuri na uongozi wa Yanga ambao umekubali kummalizia madai yake ya fedha anazoidai klabu hiyo.

 

 

Aliongeza kuwa uongozi umemjumuisha kiungo huyo kwenye kambi hiyo kutokana na kuingia hofu ya kiungo wao fundi Mnyarwanda, Haruna Niyonzima ambaye alipata majeraha ya goti kwenye mchezo uliopita wa ligi na Biashara United kuwa atakosa mechi ya Simba.

 

“Uongozi umechukua tahadhari ya haraka ya kumrejesha kikosini Banka ambaye yeye aliuomba radhi uongozi kabla ya kumtumia tiketi ya ndege ya kwenda kujiunga na kambi ya timu iliyokuwepo Bukoba ikijiandaa na michezo miwili dhidi ya Kagera na Simba.

 

“Katika mchezo wa kesho (leo) Niyonzima hatakuwepo sehemu ya kikosi chetu baada ya kocha kupendekeza kupumzika ili asijitoneshe katika kuelekea mchezo wetu wa watani wa jadi, Simba ili awepo uwanjani kuwakabili, ingawa bado kuna hofu kama atacheza,”alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Frederick Mwakalebela ambaye ndiye mkuu wa msafara alisema kuwa “Banka leo (jana) anatarajiwa kujiunga na kambi ya pamoja ya timu hapa Bukoba.

 

“Kama unavyofahamu timu yetu hivi sasa inaandamwa na majeruhi katika kikosi chetu, hivyo tumeona tumuwahishe Banka hapa Bukoba kwa ajili ya kukiongezea nguvu kikosi chetu kinachokabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Simba,”alisema Mwakalebela.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad