ZEC Kutangaza siku ya Uchaguzi


TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) siku ya Alhamis Julai 30 mwaka huu inatarajiwa kutangaza rasmi tarehe na siku ya Uchaguzi mkuu pamoja na kutangaza ratiba nzima ya uchukuaji wa fomu kwa wagombea na siku ya kuanza na kumaliza kampeni za uchaguzi.



Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Thabit Idarous Faina wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Maisara mjini Unguja ambapo alisema kuwa Tume imedhamira kuweka wazi tarehe ya uchaguzi pamoja na kuweka wazi mambo yote muhimu kuelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.



“Mimi nataka kuwaambiwa ndugu waandishi wa Habari siku ya Alhamis ndio siku ambayo kila kitu kitawekwa wazi tarehe ya  Uchaguzi, tarehe ya uchukuaji wa fomu,tarehe ya kuanza na kumaliza kampeni pamoja na mambo yote muhimu yanayopaswa kufikia siku ya uchaguzi”alisema Mkurugenzi.



Pia alisema kuwa siku hiyo Tume itatangaza idadi kamili ya wananachi ambao wamejitokeza kwa mara ya kwanza kujiandikisha pamoja na wale wote ambao walihakiki taarifa zao kwa mara ya pili katika daftari la kudumu la wapiga kura.



“Tutangaza Idadi kamili ya wapiga kura ambao wanatarajiwa kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka huu kwa wale wote wapya pamoja na wapiga kura ambao ni wazamani walihakiki taarifa zao na kukidhi vigezo”alisema Thabit Idarous Faina.



Mkurugenzi huyo alisema zoezi ambalo limeendeshwa hivi karibuni la kuwapatia vitambulisho vya kupigia kura limekwenda limefanikiwa kwa kiasi kikubwa ambapo wananchi waliojitokeza wamepatia vitambulisho vyao licha ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto.



“Nataka kuwaambia kuwa zoezi hili ni endelevu kwa wale ambao hawakupata vitambulisho katika vituo tulivyovipanga basi wantakiwa kujitokeza katika ofisi zetu za wilaya kwenda kuchukua vitambulisho vyao”Alisema Mkurugenzi huyo.



Katika maelezo yake Mkurugenzi huyo aliwataka Wananchi kutunza vitambulisho vya kupiga kura walivyopatiwa na Tume ili kuepusha usumbufu ambao unaweza kujitokeza wakati wa zoezi la kupiga kura.



“Mimi nataka kuwasisitiza wananchi kwamba jambo la kutunza vitambulisho vyao ni jambo la lazima ili kuepusha usumbufu unaweza kujitokeza kwa wale ambao wamefika vituo na walipoteza vitambulisho vya zamani pamoja risiti wametakiwa kulipa shilingi 5000”alieleza Mkurugenzi huyo.



Alieleza  hapo awali Tume iliwatoza Wananchi shilingi elfu kwa wale waliopoteza vitambulisho pamoja risiti walizopatiwa na Tume hivyo kwa wale ambao hawakupatiwa risiti za mlipo ya fedha hizo wanatakiwa kufika katika ofisi za Tume Wilaya.



“Hadi sasa tumekusanya jumla ya Shilingi Milioni 30 kwa wananchi ambao wamepoteza Vitambulisho vya zamani na risiti zao, hivyo nataka kuwaambia kwamba wale ambao walitoa fedha hizo na hawakupatiwa risiti zao wafike katika ofisi za Tume wilaya”alieleza Mkurugenzi huyo.



Hata hivyo alisema kuwa jumla ya Taasisi 26 zimejitokeza kuomba kutoa elimu ya wapiga kura kwa wananchi Unguja na Pemba ambapo hivi karibuni Tume itatangaza taasisi ambazo zimekidhi vigezo kutoa elimu ya wapiga kura.



“Tumepokea Jumla ya taasisi 26 ambazo zimehitaji kutoa elimu kwa wananchi hivyo baada ya kikao kinachofuata tutatoa taasisi ambazo zimekidhi vigezo vya utoaji wa Elimu kwa wananchi na tutaweka rasmi wazi taasisi hizo”alisema.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad